bayyinaat

Published time: 19 ,December ,2018      19:19:36
News ID: 378

Imamu akasema: "...Basi mtakaporudi kwa mwalimu wenu, mmoja wenu amwendee kwa kila aina ya heshima, mpaka ahakikishe kwamba mazingira ya kuzungumza naye ni mazuri, kisha amwambie kuwa kuna jambo ambalo limemjia katika mawazo yake na hakuna mwingine ambaye anaweza kujibu isipokuwa yeye tu (yaani mwalimu ambaye ni Al Kndiy), na jambo lenyewe ni kwamba, hivi haiwezekani ikawa huyu ambaye ametamka Quran akawa na makusudia na maana tofauti na ambazo wewe kama mwalimu unazidhania?, bila shaka atakujibu kwa kusema bila shaka linawezekana hilo. Akikujibu hivyo sasa muulize, sasa unajua vipi kwamba msemaji wa Quran alikuwa na maana nyingine tofauti na hiyo ambayo wewe unadhania (mpaka ukafikia kuamini kwamba maana za Quran zinapingana)?, hauoni kwamba utakuwa ni wale ambao wanachukua maana katika neno ambalo halina maana ile?.....”.

Kisha Imamu akasema: "...Kwa hakika mwalimu wenu ni mwerevu, kwa nukta hii tu anaweza kurejea na kutambua makosa yake”.

Mwanafunzi yule baada ya hapo akarejea moja kwa moja mpaka kwa mwalimu wake na kufanya kama alivyoelekezwa na Imamu, ilipofikia hatua ya kuuliza swali Mwalimu wake akamuomba arudie tena swali lile, mwanafunzi akafanya kama alivyoombwa, lakini mwalimu akatambua kwamba mwanafunzi huyu hawezi kuwa na maswali kama haya, hivyo akamuomba amuelekeze ni nani hasa aliyempa fikra ile.

Mwanafunzi akakazana kumwambia mwalimu kwamba ni katika mawazo yake tu, mpaka ilipofikia kwamba mwalimu anataka kumuapiza mwanafunzi yule, ndipo mwanafunzi alipofunguka na kusema kuwa ni katika mawazo ya Abuu Muhammad Hassan Bin Ally (as).

Baada ya tukio hilo mwalimu Al Kindy akagundua makosa ya nadharia yake kunako Quran kupingana yenyewe kwa yenyewe, na akatoa amri kwamba uwashwe moto na kisha akachukua kila alichokuwa amekiandika kunako nadharia hiyo na kuchoma moto.[1]

Huu ni mfano mmoja tu katika kuonyesha namna ambavyo Imamu alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba dini ya Mwenyezi Mungu haifikiwi na pumba chafu ambazo zinaweza kuwa sababu ya watu kuingiwa na shaka.

1. Zama za kulea na kuandaa kizazi

Kama ilivyo katika akili ya mwanadamu ambaye ana malengo endelevu kwamba ni muhimu kufikiria kunako mwendelezo wa malengo yako baada ya kuondoka kwako, ndivyo ambavyo tunakuta Imamu Askari naye alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba hata baada ya kuondoka kwake bado kutakuwa na watu ambao wataendeleza gurudumu lake hasa katika swala zima la kuhakikisha kwamba Imamu Mahdi na mkombozi wa ulimwengu anabakia katika mikono salama.

Na hapa ndipo ambao unakuta Imamu alikuwa akidumu katika kuandaa umma ambao utakuwa mstari wa mbele katika kusimamia majukumu hayo, unakuta kwamba Imamu alikuwa akiwahadharisha sana kunako kunyeyekea utawala dhalimu, au mahala pengine unakuta anawahimiza baadhi ya masahaba wake kutozungumza kila jambo kwani kufanya kwao hivyo inaweza kuwa ni sababu ya wao kuangamia na gurudumu lake kushindwa kusonga mbele.

Na hiki ni kipindi ambacho tunaweza sema kuwa ni kipindi muhimu na kigumu sana katika maisha ya Imamu, na hii ni kutokana na uzito wa lengo ambalo lipo katika majukumu ya Imamu, kwa maana kuhakikisha kwamba Imamu Mahdi anazaliwa kwanza, kisha anakuwa bila ya kujulikana hilo na maadui, na mwisho kabisa kuhakikisha kwamba kunakuwa na watu ambao watakuwa ni wanusuru wake baada ya baba yake kuondoka.

Huyu ndiye Imamu Hassan Askari, baba wa Imamu wa 12, ambaye wakati tunafurahia siku ya kuzaliwa kwake basi ni vyema kukumbuka pia fadhila zake pamoja na kumomba Mwenyezi Mungu atujaalie taufiki ya kumfahamu na kumfuata Imamu huyu.

Sh Abdul Razaq Bilal (AbuuAsghar).[1] Almanaqib Juz 4 Uk 457-458


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: