bayyinaat

Published time: 06 ,March ,2017      12:26:30
Kama jawabu litakuwa ndio inawezekana kukawa na vigawanyo hivi katika mambo, basi kwa urahisi tunafikia katika natija ya kwamba hawa mitume wao huja na mambo ambayo hayajulikani kwa watu na pia ni yenye kufikiwa na akili za hao watu, kwani ni kinyume cha malengo kwamba Mitume waje na mambo ambayo hayaendani wala hayafikiwi na akili ya mwanadamu.........
News ID: 38


Haja ya kuwepo viongozi wa Kimungu

miongoni mwa mambo ambayo yanakuwa yakiulizwa sana kutokana na sababu moja au nyingine ni kwamba je, kuna ulazima wowote wa Mwenyezi Mungu kutuma watu ambao ni kama sisi kwa ajili ya kuja kutufundisha?, kwani akili na uelewa wetu hautoshi kuweza kuyajua yale ambayo wao huja kutufundisha?, kwa sababu mambo ambayo Mitume wanakuja nayo hayatoki katika hali mbili zifuatazo:

(a)    Kwamba ni mambo ambayo akili zetu zinaweza kuyafikia na kuyatatua.

(b)   Ni mambo ambayo akili zetu haziwezi kuyafikia na kuyatatua.

Tukiichunguza hali ya kwanza bila shaka kuna natija ambayo tunafikia ambayo ni: kama haya mambo ambayo wanakuja nayo mitume kuna uwezekano wa akili yetu kuyafikia na kuyatatua, basi kuna faida gani ya wao kuja?.

Hali kadhalika hali ya pili pia kuna natija ambayo tunafikia ambayo ni : kama haya mambo ambayo wanakuja nayo hayawezi kufikiwa na akili zetu, basi kwanini waje nayo? Maana nafsi ya mwanadamu siku zote hupenda kitu ambacho inajua uhakika wake. Lakini mbali na hayo kuna jambo ambalo ndilo lenye kuumiza zaidi nyoyo za wanadamu, ambalo ni kwanini wanadamu wote wawe chini ya mamlaka ya mwanadamu mwenzao tena ambaye ni mmoja?.

Sasa ili kuweza kupata majibu ya maswali haya ni lazima kwanza tuchambue baadhi ya mambo ambayo ndio yatatupa mwangaza kwa kila ambacho kinaweza kuwa ni kizuizi au sababu ya kujiuliza maswali haya.

1.      Ni lazima kwanza tukubali kwamba elimu na hata akili zetu zina mapungufu makubwa sana katika kufahamu na kudiriki kila jambo, na aili kuthibitisha hili hebu tuangalie pamoja na kwamba ulimwengu umekuwa ni wenye kuendelea mno katika nyanja za elimu, lakini pamoja na hayo kama tutaamua kupima idadi ya mambo tunayoyajua na mambo tusiyoyajua, tutakuta kwamba idadi kubwa itaangukia katika mambo tusiyojua, hii ina maana kwamba mambo tunayoyajua ni machache kuliko mambo tusiyoyajua.

Kisha hebu tuwe wakweli na nafsi zetu, je ni sahihi kugawanya mambo katika vipengele viwili tu, yaani kusema kwamba mambo yote ima yawe ni yenye kufikiwa na akili au yasiyofikiwa na akili?, kwani hatuwezi kusema kwamba mambo yanagawanyika katika makundi matatu, kuna ambayo yanafikiwa na akili na yamejulikana, kisha kuna ambayo yanafikiwa na akili lakini bado hayajajulikana, na mwisho kuna ambayo hayajulikani kabisa kwamba yanafikiwa na akili au la?.

Kama jawabu litakuwa ndio inawezekana kukawa na vigawanyo hivi katika mambo, basi kwa urahisi tunafikia katika natija ya kwamba hawa mitume wao huja na mambo ambayo hayajulikani kwa watu na pia ni yenye kufikiwa na akili za hao watu, kwani  ni kinyume cha malengo kwamba Mitume waje na mambo ambayo hayaendani wala hayafikiwi  na akili ya mwanadamu, na kama itakuwa watu wanayaona ni kinyume na akili basi huu ni ule upungufu wao na wala si upungufu kwa Mtume au jambo lenyewe kama tutakavyokuja kubainisha hapo baadaye.

Kwa minajili hii basi, kila ambaye anasimama na kusema kwamba hakuna haja wala faida yeyote ya kuwepo Mitume (kama kundi la Barhama huko India na kwengineko) basi kwa uhakika itakuwa hawajafahamu kwamba akili na uelewa mwanadamu hauwezi kufikia na kuelewa kila jambo, na mfano wake ni mfano wa mwanafunzi wa chekechea ambaye ndio kwanza amejifunza silabi zote na kuona kwamba hana haja tena ya mwalimu kwani ameshajua.

2.      Kwa ambaye anaona kwamba swala la kuwepo Mitume litapelekea binadamu wote kuwa katika utawala na mamlaka ya binadamu mmoja, ni lazima atambue yafuatayo: tunapozungumzia mtume basi ni wazi kwamba tunazungumzia binadamu ambaye ana mahusiano ya karibu mno na Mwenyezi Mungu kuliko hao binadamu wengine, na kuwa kwetu chini yake basi ni kwa sababu tu ya hii sifa ambayo sisi hatuna, sasa je katika hali kama hii bado itabakia kwamba ni jambo baya?.

Kwa mantiki hii tunafikia katika natija ya kwamba kukataa uwepo wa Mitume kwa vigezo kwamba sisi wenyewe tunaweza kuyafikia hayo mambo ambayo wanakuja kutufundisha, au kwa kigezo kwamba kuja kwao kuna maanisha kwamba binadamu wote tutakuwa chini ya mtu mmoja, ni mambo ambayo hayana mashiko wala uhakika ndani yake. Na hii ni kutokana na kwamba siku zote akili ya mwanadamu haiwezi kufikia kila kitu, na hawa mitume ndio ambao wanakuja kumfunza asiyoyajua kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Pia kuwa chini ya watu kama hawa sio jambo baya, kwani wana kitu ambacho wanatuzidi na hatuna, nacho ni kwamba wao wapo karibu sana na muumba na wana elimu ambayo sisi hatuna, na nafsi ya mwanadamu inahukumu ubaya endapo tu itakuwa chini ya ambaye wanalingana kila kitu au amemzidi baadhi ya mambo.

                                                          Itaendelea......

 

 

LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: