bayyinaat

Published time: 19 ,December ,2018      19:44:52
“....Nyumba ambayo inadumisha muziki haiwi katika amani ya majanga, na dua kutoka humo hazijibiwi, na wala malaika hawaingii nyumba hiyo...”
News ID: 386

Athari ya Muziki kwa mtu mmoja mmoja:

Katika kubainisha jambo hili itatosha sana kauli ya Mtukufu Mtume aliposema:

"الغناء يُنْبت النِّفاق في القلب"

"....Muziki huleta unafiki nyoyoni...”[1]

Ni hii ni kutokana na kwamba muziki kama muziki haupatani kabisa na kumtii Mungu, Ibada, wala mambo mema kwa ujumla. Nandio maana katika nyoyo ambayo kumejaa muziki huwezi kukuta kuna athari za ibada na kumuogopa Mungu hata siku moja. Hii ni kutokana na mwenye kushikamana na muziki basi hufanya kama ndio Mungu wake na maisha yake kwa ujumla.

Unadhani mtu ambaye hamu yake yote ni kuhuisha sunna ya kijahili kama hii anaweza kweli kuhifadhi imani yake au sunna za watu wema?.

Pia ukiachana na athari ambayo tumeitaja hapo juu, kuna athari nyingine ambazo zinaweza kupatikana kwa mwenye kushikamana na muziki.

Mambo kama vile kukatika au kupungua kwa riziki ya mtu, kuwa mzito katika mambo ya ibada, bali katika baadhi ya riwaya imekuja kuwa muziki ni chimbuko la zinaa (Mungu atuepushe). Kama ambavyo pia imekuja kuwa sauti ya muziki ni sauti iliyolaaniwa duniani na akhera, pia inafanya moyo kuwa mgumu nk.

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Swadiq (as) kwamba alisema:

بيت الغناء لا تُؤمن فيه الفجيعة، ولا تُجاب فيه الدعوة، ولا يدخُلُه الملك

"....Nyumba ambayo inadumisha muziki haiwi katika amani ya majanga, na dua kutoka humo hazijibiwi, na wala malaika hawaingii nyumba hiyo...”

Hizi zote ni athari za kidunia na akhera ambazo zinamkumba mwenye kushikamana na muziki, kama ambavyo nyumba ambayo ndani yake kuna mambo hayo pia inakosa zile baraka za kutembelewa na malaika pia.

Balaa katika zama hizi:

Miongoni mwa mambo ambayo ni vyema kuyazungumzia katika makala hii na masikitiko ambayo tunaweza kuyaona katika zama hizi, hasa pale ambapo kuna baadhi ya kaswida za kumsifu Mtume kwa mfano zimegeuka na kuwa muziki. Kwa haraka haraka ukichunguza swala hili basi huwezi kutoka katika moja ya mambo yafuatayo:

1. Kutokujua

Kwa maana ya kwamba huyu ambaye anaimba kaswida hizi zenye kufanana na muziki hana elimu juu ya uharamu wa jambo hilo. Kwa maana endapo angekuwa na ujuzi juu ya hilo basi asingaliangukia katika janga hilo.

2. Kubebwa na hali halisi:

Kwamba mtu anajikuta anapenda kumsifu Mtume kwa njia ya mashairi na tungo, lakini katika jamii aliyopo ili uonekane kwamba umesifu na watu wakukubali basi ni lazima ufuate mfumo fulani. Na mfumo ambao umeenea katika jamii hiyo ni muziki na midundo. Basi na yeye anaathirika na kukuta anasifu kwa njia ya muziki na midundo.

3. Kuiga kwa malengo ya mali:

Wakati mwingine mtu anakuwa na elimu juu ya uharamu wa jambo lile, lakini kwa kuwa fulani amefanya na endapo nikifanya vile niytakuwa kama yule katika umaarufu na utajiri basi na yeye anafanya.

Hizi ni baadhi tu ya sababu ambazo kwa haraka zinaweza kuwa ni msukumo katika haya ambayo tunayaona leo, ya kwamba ni kaswida ya kumsifu Mtume kwa mfano, lakini njia ambayo imetumika ndani yake haiendani kabisa na mafunzo ya huyo unayemsifu.

Kama ambavyo pia ni masikitiko makubwa kuona kwamba kuna watu wanajua kabisa uharamu wa muziki, lakini kutaka kutoka katika shimo hilo wanakuja na njia mbadala na kusema kwamba endapo utakuwa muziki na ndani yake akatajwa Mwenyezi Mungu au mawalii basi uharamu unaondoka. Subhanallah!.

Huku ni kujaribu kucheza na mafundisho ya Mwenyezi Mungu (Swt), kama ambavyo pia ni kuichukulia wepesi dini kwa mujibu wa matakwa yako.

Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) akisema:

أخاف عليكم استخفافاً بالدين... وأن تتخذوا القرآن مزامير

"....Nahofia sana wakati ambapo dini mtaichukulia wepesi, na Quran ikawa ni mfano wa zumari (Nyimbo)..”[2]

· Kushajiisha muziki na waimbaji:

Miongoni mwa mambo ambayo pia katika Uislamu ni mambo yasiyofaa na inatakiwa watu kujiepusha nayo ni swala zima la kushajiisha na kusifu waimbaji wa muziki.

Kwani imepokelewa kuwa ni katika maneno mabaya mno kama ulivyo uongo, kusikika mmoja wetu akimwambia muimba muziki "ahsanta”, yaani safi sana na mfano wa hayo.

Tumalizie na kisa katika sehemu hii kwamba siku moja Imamu Swadiq alikuwa akipita na akamkuta jamaa mmoja akisikiliza muziki, Imamu akamwambia ".....Hebu inuka na ukaoge kisha uombe msamaha kwa mola wako, kwani ulichokuwa unakifanya ni kizito mno laiti kama ungalikufa katika hali hiyo, kwanza mshukuru Mungu wako kisha muombe msamaha, kwani Mwenyezi Mungu huchukia mabaya, hivyo nawe waachie mabaya watu wake, kwa sababu kila jambo lina watu wake...”

Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe ni wenye kuepukana na maovu aliyoyakataza, na tushikamane na kila mema aliyoyaamrisha.

Assalamu alaykum warahmatullah.

Imeandikwa na Sh Abdulrazaq Bilal (AbuuAsghar).[1] Mizanul Hikma hadithi ya 15085

[2] Wasailu shia Juz 12 Uk 229


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: