bayyinaat

Published time: 14 ,September ,2021      23:45:00
HIJAB - 001
Ulazima wa mwanamke kujihifadhi anapokabiliana na mwanaume ni miongoni mwa masuala muhimu mno katika dini tukufu ya Kiislamu. Hili ni jambo ambalo limezungumziwa kwa bayana katika Qurani tukufu. Hivyo basi, hili ni suala ambalo halina shaka kwa mtazamo wa Kiislamu.
News ID: 432

HIJABU

Kwa jina la Mwenyezi Mungu

UTANGULIZI

Ulazima wa mwanamke kujihifadhi anapokabiliana na mwanaume ni miongoni mwa masuala muhimu mno katika dini tukufu ya Kiislamu. Hili ni jambo ambalo limezungumziwa kwa bayana katika Qurani tukufu. Hivyo basi, hili ni suala ambalo halina shaka kwa mtazamo wa Kiislamu.

Kumhifadhi mkeo dhidi ya mwanaume ambaye sio maharimu[1] wake ni miongoni mwa udhihirisho wa ulazima wa kuweka mipaka baina ya wanaume na wanawake wasiokuwa na uhusiano wowote. Suala hili lazima lichambuliwe katika vipengele vitano vijavyo:

1- Je vazi la hijabu ni miongoni mwa sifa zinazotambulisha dini ya Uislamu na imeenezwa na Waislamu kwa wasiokuwa Waislamu baada ya kudhihiri kwa dini ya Uislamu? Au sio miongoni mwa sifa mahususi za dini ya Uislamu na Waislamu na ni kitu kilichokuwepo hata katika mataifa mengine kabla ya ujio wa Uislamu?

2- Ni nini sababu ya hijabu?

Kama tujuavyo, hakuna uhusiano wa kihalali au kiharamu katika wanyama wa kiume na wa kike, bali wanaishi pamoja kwa uhuru. Kanuni asili ya maisha ina hukumu pia wanadamu wanapaswa kuishi vivi hivi. Je, ni kipi kilisababisha uwepo wa mpaka baina ya mwanaume na mwanamke kwa mfumo wa hijabu ya mwanamke au mfumo mwingine ule? Suala hili halina mafungamano pekee na uvaaji, bali ni suala muhimu hata katika maadili ya kijinsia. Jambo hili pia linapatikana katika suala la kimaadili na uchamungu. Wanyama hawana aibu katika masuala ya kijinsia kinyume na wanadamu na haswa kwa wanawake.

3- Falsafa ya uvaaji kwa mtazamo wa Uislamu.

4- Kasoro na mapungufu

5- Kipimo cha mavazi katika Uislamu ni kipi?

Je, Uislamu unaunga mkono suala la mwanamke kujitenga au unaunga mkono mwanamke asitiri mwili wake mbele ya mwanaume asiyekuwa maharimu wake bila kulazimika kujitenga na jamii? Na katika suali la pili, je, ni kipi kipimo cha hijabu? Je, uso na mikono miwili hadi kwenye vifundo lazima pia vifunikwe au kando na uso na mikono, vingine vyote vifunikwe, au sio lazima kufunika uso na mikono yote hadi kwenye vifundo? Hata hivyo, je, suala la faragha lipo katika Uislamu au laa? Kwa ibara ya pili ni kuwa, je, katika Uislamu, kuna kitu kingine cha tatu ambacho sio (kujitenga kwa wanawake) na wala (wanawake kujichanganya na wanaume) au laa? Na kwa kauli nyingine, je, Uislamu unaunga mkono kutenganisha mikusanyiko ya wanaume na ya wanawake au laa? Haya ni maswali ambayo yatajibiwa katika kitabu hiki.[1] Maharimu ni mtu ambaye mna uhusiano wa kidamu ambaye huna ruhusa ya kumuoa. Mfano wake ni mama mzazi, dada, shangazi. [Mtarjumi] ☻☻

SEHEMU YA KWANZA: HISTORIA YA HIJABU

1- Je, suala la hijabu lilikuwepo katika mataifa ya hapo mbeleni?

2- Hali ya hijabu katika enzi za Jahiliya.

3- Hijabu katika kaumu ya Mayahudi.

4- Hijabu ya Iran katika zama za kale.

5- Hijabu ya India.

Historia ya hijabu

Elimu yangu kwa upande wa historia ya hijabu sio kamili. Elimu yetu katika historia itakamilika tu endapo tutaweza kutoa nadharia kuhusu mataifa yote kabla ya ujio wa Uislamu. Kilicho bayana ni kuwa kabla ya ujio wa Uislamu, suala la hijabu lilikuwepo kwa baadhi ya mataifa.

Kutokana na vitabu husika nilivyosoma, suala la hijabu lilikuwepo Iran katika zama za kale, katika kaumu ya Mayahudi na huenda pia nchini India. Hijabu ya mataifa haya ilikuwa shadidi hata kuliko kanuni ya hijabu iliyokuja katika Uislamu. Hata hivyo, suala la hijabu halikuwepo katika enzi za Jahiliya[1] na lililetwa na ujio wa Uislamu. katika kitabu chake,[2] Will Durant anaandika ifatavyo kuhusu kaumu ya Mayahudi: "Ikiwa mwanamke angekiuka kanuni ya Kiyahudi kwa mfano atembee miongoni mwa watu bila kufunika kichwa, au azungumze na wanaume wa kila aina, au apaze sauti yake kiasi cha kwamba akiwa kwake, majirani waweze kusikia anachosema, katika hali kama hiyo, mwanaume alikuwa na haki ya kumpa talaka bila ya kulipa mahari yake.”

Hijabu iliyokuwepo katika kaumu ya Mayahudi ilikuwa ni shadidi kuliko hijabu katika Uislamu, kama ambavyo tutabainisha hapo mbeleni. Mwandishi wa kitabu ‘Tamaduni ya Mayahudi’ asema ifatavyo kuhusu Wairani wa zamani: "Katika zama za Zartosht,[3] wanawake walikuwa na hadhi ya juu mno. Walikuwa na uhuru wa kujichanganya na watu…”[4]

Kisha anasema:

"Baada ya utawala wa Dario[5], hadhi ya wanawake ikashuka chini haswa katika tabaka la matajiri. Kutokana na kuwa wanawake mafakiri walilazimika kutafuta ajira, walilazimika kujichanganya na watu na hivyo basi, wakahifadhi uhuru wao. Lakini, wanawake wengine - kutokana na ulazima wa kujitenga kwao katika kipindi waonapo masiku yao ya mwezi – suala hili la kujitenga liliendelea hadi likawa ni kitu kilichozoeleka katika maisha yao ya kijamii. Na hili ni jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni msingi wa hijabu katika Uislamu. Wanawake wa tabaka la juu katika jamii (matajiri) walikosa ujasiri wa kutoka nje isipokuwa kwa kubebwa kwenye viti vya kifahari. Hata hivyo, hawakupewa ruhusa kamwe ya kuamiliana na wanaume waziwazi. Wanawake walioolewa hawakuwa na ruhusa ya kuonana na mwanamme yeyote hata baba na ndugu. Katika picha zilizobaki za Irani ya kale, hakuna sura ya mwanamke inayoonekana wala jina la mwanamke kutajwa…”

Kama uonavyo, suala la hijabu lilikuwa ni gumu na shadidi katika kipindi cha Iran ya kale kiasi cha kuwa hata baba na ndugu wa mwanamke aliyeolewa alikuwa amezuiwa kuonana naye. Kwa mtazamo wa Will Durant, kanuni shadidi ambazo kulingana na sharia na mila za kitambo za Majusi[6] zilikuwa zikitekelezwa kwa mwanamke aliyekuwa katika siku zake za mwezi – ambaye alikuwa akifungiwa chumbani kwake – na kila mtu kujitenga naye na kumuepuka katika hiki kipindi – ndiyo sababu kuu ya kupatikana kwa hijabu katika Iran ya kale. Kanuni zizi hizi pia zilikuwa zikitekelezwa katika kaumu ya Mayahudi.

Lakini, kauli yake: "Na hili jambo pia linachukuliwa kama msingi uliosababisha suala la hijabu katika Uislamu,” anakusidia nini?

Je, anakusudia kuwa kanuni hizo ngumu na shadidi zilizotekelezwa kwa mwanamke aliyekuwa katika siku zake ndizo chanzo cha hijabu katika Uislamu? Sote tunatambua fika kuwa kanuni hizi hazikuwepo na wala hazipo katika Uislamu. Katika Uislamu, mwanamke aliyekuwa katika siku zake ameondolewa ulazima wa kutekeleza baadhi za ibada kama vile kuswali na kufunga. Vile vile, kufanya tendo la ndoa ni haramu kwake. Lakini, mwanamke huyu hajakatazwa kuamiliana na watu wengine kiasi cha kumfanya ajitenge na kukaa kivyake.

Na iwapo anakusudia kuwa hijabu lililozoeleka miongoni mwa Waislamu ni ada ya Wairani walioieneza kwa Waislamu wengine baada ya kusilimu, bado kauli yake itakuwa sio sahihi. Hii ni kwa kuwa kabla ya Wairani hawajawa Waislamu, aya kuhusu hijabu zilikuwa zimeshateremshwa.

Kauli nyingine ya Will Durant inadhihirisha mambo haya mawili – yaani anadai kuwa hijabu ilienezwa kwa Waislamu baada ya Wairani kusilimu. Vile vile, anadai kuwa kutolala na mwanamke aliyekuwa katika siku zake ilikuwa na athari katika hijabu ya mwanamke au angalau katika kujitenga kwake.

Katika sehemu nyingine anasema:

"Uhusiano wa Waarabu na Iran ndiyo chanzo cha kuenea kwa hijabu na kulawiti katika jamii ya Waislamu. Waarabu waliogopa haiba ya mwanamke na walikuwa wakivunjwa moyo kila mara kutokana nayo. Nao walifidia ushawishi huo asili wa mwanamke kwa kudhihirisha shaka – ambayo ni kawaida ya wanaume – kuhusu wanawake kuwa bikira na wachamungu. Umar alikuwa akiambia watu wa kaumu yake, "Shaurianeni na wanawake lakini, tendeni kinyume na ushauri wao. Hata hivyo, katika karne ya kwanza, Uislamu haukuwa umemlazimisha mwanamke kuvaa hijabu. Wanawake na wanaume walikuwa wakiamiliana kwa uhuru na walitembea pamoja barabarani na pia kuswali pamoja misikitini. Hijabu na utowashi zilianza katika kipindi cha utawala wa Walid II[7] (126 H – 127 H). Kuanzia hapa ndipo mwanamke alilazimika kujitenga na wanaume katika siku zake za mwezi na siku za nifasi[8].”[9]

Katika sehemu nyingine anasema:

"Bwana Mtume (s) alikuwa amekataza watu kuvaa nguo pana lakini baadhi ya Waarabu walikuwa wakipuuza desturi hii. Tabaka zote zilikuwa na mapambo. Wanawake walikuwa wakijipamba kwa kuvaa mavazi mapana, marefu na zenye rangi ya kupendeza. Walifunga nywele zao kwa mitindo ya kupendeza au kuzichana kwa kuzigawa mara mbili kichwani. Wakati mwingine walizisuka kwa mitindo mbalimbali na waliimarisha muonekano wa nywele zao kwa kutumia nyuzi nyeusi za hariri. Mara nyingi, walijipamba kwa vito vya thamani na maua. Baada ya mwaka wa 97 H walianza kuficha uso zao chini ya nikabu. Kwanzia hapo, jambo hili likawa ni ada yao.”[10]

Kuhusu Wairani wa kale, Will Durant asema:

"Kufunga ndoa ya muta iliruhusiwa. Hawa wanawake wa muta walikuwa huru kama Masuria wa Kigiriki kujidhihirisha mbele za watu na kuhudhuria hafla za wanaume. Hata hivyo, wanawake wa ndoa walibaki nyumbani mara nyingi. Mila hii ya kitambo ya kiirani iliingizwa katika Uislamu.”[11]

Will Durant anazungumza kana kwamba katika zama za Bwana Mtume (s) hakukuwa na amri yoyote kuhusu hijabu ya mwanamke na kwamba mtume wetu alikuwa tu amekataza uvaaji wa mavazi mapana! Vile vile, wanawake wa Kiislamu walitembea bila hijabu kuanzia karne ya kwanza hadi mwanzoni mwa karne ya pili. Hata hivyo, hii ni kinyume na hali ilivyokuwa. Historia inathibitisha kinyume na kauli ya huyu Will Durant. Ipo wazi kuwa mwanamke katika zama za ujahili aliishi namna ambavyo Will Durant anasema lakini, ujio wa Uislamu ulibadilisha hali hiyo. Bi Aisha alikuwa akisifu wanawake wa Kianswari ifatavyo:

"Hongera kwa wanawake wa Kianswari. Pindi ambapo aya za surat al-Nur[12] zilipoteremshwa, hakuna hata mmoja wao aliyetoka nje kama hapo mbeleni (bila hijabu). Walikuwa wakifunika vichwa vyao kwa vitambaa vyeusi. Ni kana kwamba kunguru walikuwa wameketi kwenye vichwa vyao.”[13]

Suala hili limenukuliwa pia kutoka kwa Ummu Salamah lakini, tofauti ni kuwa Ummu Salamah anasema:

"Baada ya aya ya Surat al-Ahzaab kuteremshwa wanawake wa Kianswari walifanya hivi.”[14]

يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلَابِيبِهِنَّ

Wajifunike kwa hijabu (wanapokwenda nje) [15]

Katika kitabu chake cha ‘Miaka mitatu nikiwa Iran’, Joseph Gobineau anaamini hijabu shadidi katika kipindi cha dola la Sasania katika kipindi cha Uislamu imebaki miongoni mwa Wairani. Anaamini kuwa kilichokuwepo katika kipindi cha dola la Sasania, haikuwa ni hijabu kwa mwanamke pekee, bali ilikuwa ni kuficha wanawake. Anadai kuwa viongozi na wafalme katika zama hizo walikuwa na tabia mbaya kiasi cha kuwa lau mtu angekuwa na mwanamke mrembo nyumbani kwake, mtu huyo asingeruhusu mtu yeyote apate habari hiyo. Mtu huyo alitumia mbinu yoyote ile kumficha kwani lau ingejulikana kuna mwanamke mrembo nyumbani kwake, basi asingekuwa tena chini ya umiliki wake na wakati mwingine pia hata maisha yake yalikuwa hatarini.

Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa zamani wa India anaamini pia kuwa hijabu ilienezwa katika ulimwengu wa Kiislamu kutoka kwa mataifa yasiyokuwa ya Kiislamu ya Roma na Iran. Baada ya kusifu tamaduni ya Kiislamu katika kitabu chake, anaashiria mabadiliko yaliyotokea baadae ambapo anasema:

"Miongoni mwa mabadiliko makubwa na ya kuhuzunisha yaliyojiri taratibu ni katika hali ya wanawake. Mila na desturi ya hijabu haikuwepo katika jamii ya Waarabu. Wanawake wa Kiarabu hawakuwa wakijitenga wala kujificha kwa wanaume, bali walikuwa wakihudhuria katika sehemu za jumuiya ya watu. Walikwenda misikitini na walihudhuria vikao vya hotuba na hata wao walikuwa wakitoa hotuba. Lakini, kutokana na mafanikio, Waarabu pia walijifunza taratibu, kutoka kwa majirani zao (Ufalmwe wa Kirumi ya Mashariki na Kiajemi). Waarabu walishinda vita dhidi ya ufalme wa Kirumi na kusitisha ufalme wa Iran (Kiajemi). Lakini, waliiga mila na desturi mbovu kutoka kwa falme hizi mbili. Kulingana na kilichonukuliwa, kutokana na athari ya falme hizi mbili, ndipo chanzo cha hijabu na kujitenga kwa wanawake miongoni mwa Waarabu kulipoanzia. Mfumo wa kurahamisha mjumuiko wa wanaume na wanawake ulianza taratibu na wanaume wakatengwa na wanawake.”[16]

Hamna shaka kuwa mtazamo huu sio sahihi. Ni kutokana na kuamiliana kwa Waarabu Waislamu na watu waliosilimu ambao sio Waarabu ndipo hijabu ilikuwa shadidi kuliko katika zama za Bwana Mtume (s), na sio kwamba Uislamu haukupa hijabu umuhimu wowote. Maneno ya Jawaharlal Nehru yanadhihirisha kuwa Warumi pia (labda kutokana na athari ya Mayahudi) waliiga suala la hijabu na mila hii ikafikia viongozi wa Kiislamu kupitia Warumi na Wairani. Hii ni nukta ambayo imethibitishwa pia na watu wengine.

India pia suala la hijabu lilikuwa shadidi. Hata hivyo, haijulikani kama lilikuwepo kabla ya Uislamu kuenea India au baada yake na Wahindi wasiokuwa Waislamu wakaiga kutoka kwa Waislamu na haswa Wairani Waislamu. Kilicho bayana ni kuwa hijabu ya India ilikuwa ngumu na shadidi kama hijabu ya Iran ya kale. Katika kitabu cha Will Durant, jildi ya pili, inadhihirika kuwa hijabu ilienezwa India kupitia Wairani Waislamu.

Baada ya maneno tuliyonukuu kutoka kwa Jawaharlal Nehru, anasema:

"Kwa bahati mbaya, mila hii mbovu ikawa ni moja ya sifa mahususi za jamii za Kiislamu na Wahindi pia walijifunza kipindi Waislamu walipokwenda India.”

Kwa mtazamo wa Jawaharlal Nehru Jawar, hijabu ya India ilienezwa huko kupitia Waislamu. Lakini, tukichukulia kuwa suala la kutamani riyadha[17] na kuacha anasa na starehe za dunia ni moja ya sababu ya kupatikana kwa hijabu, basi ni lazima tukubali kuwa India ilikuwa imekubali suala la hijabu kuanzia kitambo sana. Hii ni kwa sababu India ilikuwa ni miongoni mwa makao makuu ya riyadha ulimwenguni.

Bertrand Russell anasema:

"Maadili ya kijinsia kama inavyoonekana katika jamii, imetokana na vitu viwili: Moja ni matamanio ya kuwa baba, na ya pili ni itikadi ya kitawa kuwa mapenzi ni kitu kibaya. Maadili ya kijinsia katika zama za kale kabla ya Ukristo na katika nchi za Mashariki ya mbali hadi leo hii imetokana na chanzo chake asili isipokuwa India na Iran ambapo suala la riyadha lilichipuka na kuenea kote ulimwenguni.”[18]

Kivyovyote vile, kilicho wazi ni kuwa kabla ya Uislamu, suala la hijabu lilikuwepo ulimwenguni na Uislamu sio chanzo chake. Wa ama suala la kipimo cha hijabu katika Uislamu kuwa sawa na hijabu katika mataifa mengine au laa, na pili, sababu ya Uislamu kulazimisha hijabu ndizo sababu za kulazimisha hijabu katika sehemu zingine ulimwenguni au laa, ni mambo ambayo tutazungumzia kinaga ubaga katika sehemu zijazo.[1] Enzi kabla ya ujio wa Uislamu unafahamika kama enzi ya Jahiliya (enzi ya ujahili). Jina hili linatokana na tabia na mila mbovu za kijahili zilizokuwa zimeenea katika Bara Arabu. Moja katika mila hizi ilikuwa ni kumzika mtoto wa kike akiwa hai kwa kuhofia baba kupatwa na aibu ya kupata mtoto wa kike. Mila hizi za kijahiliya ziliteketezwa na ujio wa Uislamu na ujio huu ndio ulisitisha enzi hii mbovu. [Mtarjumi]

[2] Tarikh-e Tamadun (tarjama ya Kifarsi): jildi: 30, uk. 12

[3] Zartosht (‘Zoroaster’ katika kimombo) ni mtume katika Iran ya kale aliyeleta dini ya Uzartoshti au ‘Zoroastianism’ katika kimombo. [Mtarjumi]

[4] Tarikh-e Tamadun (tarjama ya Kifarsi): jildi:1, uk. 552.

[5] Dario I, anayejulikana kama Dario Mkuu, alikuwa mfalme wa tatu wa wafalme wa Waajemi wa Dola la Akaemenid, akitawala kutoka 522 (Kabla ya Kristo) hadi kifo chake mnamo 486 (Kabla ya Kristo).

[6] Majusi ni dini ya kitambo ambayo bado ipo Iran ambayo wafuasi wake huabudu moto. Dini hii inaapatikana katika mikoa wa . [Mtarjumi]

[7] Walid ibn Yazid au Walid II alikuwa Khalifa wa Umayyad ambaye alitawala kutoka 743 hadi kuuawa kwake mnamo mwaka 744.

[8] Nifasi ni damu inayotoka ukeni kwa sababu ya kujifungua. Inakuja kwa kujifungua, baada ya kujifungua au siku mbili mpaka tatu kabla ya kujifungua sambamba na machungu. [Mtarjumi]

[9] Tamaduni za Mayahudi, jildi: 11, uk. 112

[10] Tamaduni za Mayahudi, jildi: 11, uk. 111

[11] Tamaduni za Mayahudi, jildi: 10, uk. 233

[12] Surat al-Nur: 31

[13] Al-Kashaaf, chini ya aya ya 31 ya Surat al-Nur

[14] Sunan Abu Dawud, jildi ya 2, uk. 382

[15] Surat al-Ahzaab: 33

[16] Historia ya Dunia (Tarikh-e Jahan), jildi ya 1, uk. 328.

[17] Hapa tunakusudia mazoezi kwa ajili ya kukomaza roho ya mwanadamu. Ni mazoezi ambayo wanairfani hufanya kwa ajili ya kukomaza roho zao ili kumfikia Mola wao. Mazoezi haya ni kama kufunga saumu kwa wingi, kukesha usiku kwa ibada na kuacha anasa na starehe zote za dunia. Ni mazoezi magumu na sio kila mtu anaweza. Inahitaji taufiki ya Mwenyezi Mungu (s.w.t). [Mtarjumi]

[18] Ndoa na Maadili (Zanashui va Akhlaq), uk. 135.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: