bayyinaat

Published time: 07 ,March ,2017      22:23:35
Katika aya hii tunafahamu ya kwamba husuda ni katika sifa mbaya mno, na ndio maana Mwenyezi Mungu ameiweka miongoni mwa mambo ambayo tunatakiwa tujikinge nayo. Imepokelewa riwaya kutoka kwa Imamu Sadiq as akisema “ hakika husuda humaliza imani ya mja kama ambavyo moto humaliza kuni ziwakazo”......
News ID: 46

Surat Falaq

(asubuhi)

Ina aya 5 na imeteremshwa Makka

Mambo yaliyokusanywa na sura hii

Sura hii nayo ni kama ambavyo tuliona katika surat Nass, kwamba ni sura ambazo ziliteremshwa kwa Mtume (saww) kwa lengo la kumpa mafundisho yeye na umma wake jinsi ya kujikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shari za ulimwengu huu, hivyo basi sura hii pia inaingia katika mfumo wa sura ambazo ni kinga.

Na sura yenyewe ni kama ifuatavyo:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

"Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu”

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ (1)

(1)  "Sema ewe Mtume kwamba unajilinda kwa mola wa asubuhi”.

Neno "falaq” katika lugha ya Kiarabu lina maana ya kuchambua na kutenganisha kitu, lakini tunaona hapa Mwenyezi Mungu analitumia neno hili kwa kumaanisha asubuhi, hii ni kutokana kwamba asubuhi kama tunavyojua kuwa ndio ambayo inapasua giza na kuweza kudhihiri, hivyo basi ni maana ambazo zinaendana kwa karibu.

مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ (2)

(2) "Unajilinda kutokana na shari ya alichokiumba”

 

Kwamba unaelekea kwa mola wako kutokana na shari ya viumbe vyake, viwe ni watu au majini. Lakini hii haina maana kwamba Mwenyezi Mungu ameumba mambo ambayo ni shari mpaka sisi tuwe ni wenye kujikinga nayo kwake, hapa ni lazima kwanza tuelewe maana ya kuumba kisha ndio tujue kwamba Mwenyezi Mungu hakuumba shari. Kuumba kama inavyoelezewa kwamba ni kuleta kitu katika uwepo baada ya kuwa hakikuwepo, na kwa maana hii bila shaka ni jambo la heri ila tu shari itakuja kwa kitu kile baada ya kuwa kimeumbwa na kimechukua vipi nafasi yake katika utekelezaji. Kama kitabakia katika asili yake basi kitaendelea kuwa heri, na kama kitatoka katika mfumo sahihi basi kitakuwa shari.

وَمِنْ شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ (3)

(3) Na pia unajilinda na shari ya usiku mzito unapoingia”

 

Na hii ni kutokana kwamba viumbe wabaya mara nyingi sana wamekuwa wakitumia usiku kama ngao ya kufanya mabaya yao. Hivyo basi unajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shari za hawa viumbe ambao huwa na tabia kama hizi.

 

وَمِنْ شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ (4)

(4)  "Na pia unajilinda na shari za wenye kupuliza katika mafundo”

 

Ni nani ambao hupuliza katika mafundo?

Wafasiri wengi wa Quran wameeleza kwamba maana halisi ya wenye kupuliza kwenye mafundo ni wanawake ambao hufanya kazi za kuroga na uchawi. Lakini pia maana ya neno "wenye kupuliza katika mafundo” inaweza kuwa pana zaidi ya kuishia tu kwa wachawi, kwani hata ambao wanakuwa na nia ya kuchonganisha au umbea na kutenganisha baina ya walioungana pia wanaingia katika maana ya neno hili, hivyo basi hakuna kizuizi kama itakuwa kwamba tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kila ambaye anakuwa na lengo baya kwetu.

 

 

وَمِنْ شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ (5)

(5) "Na pia unajilinda kuokana na shari ya hasidi anapofanya husuda zake”

 

Katika aya hii tunafahamu ya kwamba husuda ni katika sifa mbaya mno, na ndio maana Mwenyezi Mungu ameiweka miongoni mwa mambo ambayo tunatakiwa tujikinge nayo.

Imepokelewa riwaya kutoka kwa Imamu Sadiq as akisema " hakika husuda humaliza imani ya mja kama ambavyo moto humaliza kuni ziwakazo”

Mwenyezi Mungu atulinde na kila shari ambazo zinakuwa zinatuzunguka katika maisha yetu.

 

Sh Abdul Razaq Rashid.

non-publishable: 0
Under Review: 0
Published: 1
2640/01/11 - 09:37
|
Tanzania, United Republic of
|
Anonymous
0
0
Allah akulipe pepo sheikh kwa kutuelimisha na usisite kutuelimisha kwa lile Allah alilokujalia kulijua
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: