bayyinaat

Published time: 08 ,March ,2017      17:24:58
Ndugu zangu, kuwepo shetani katika ulimwengu huu ni jambo zuri, na ni kheri lakini uzuri au kheri inamrejea yeye mwenyewe (shetani). Na halikadhalika kila kilichopo (kama Malaika, majini binadamu, mimea, wanyama) bilashaka kuwepo kila kimoja katika hivyo vilivyotajwa ni kheri......
News ID: 48

Falsafa Ya Kuumbwa Shetani

Shetani ni kiumbe ambae analaaniwa misikitini na makanisani, na sehemu mbalimbali za ibada, na hajabahatika katika yake kupata watu wanaomuabudu kama ilivyo ng`ombe, moto, masanamu na mengineo. Na mara nyingi watu hujiuliza kwamba kuna haja gani Mungu kumuumba kuimbe huyu anayelaaniwa na kila mtu? Hali hiyo ndio imepelekea mimi kuchagua mada hii ili kuitolea ufafanuzi.

SHETANI

Kwa nini Mungu kamuumba Shetani?

Je kama Mungu asinge muumba Shetani hauoni kwamba ungekuwa wacha Mungu sana?

Je Mungu kamuumba shetani kwa kuwa anamuhitaji awepo au kwa kuwa anamuhitaji awepo au kwa kuwa  wanadamu wanamuhitajia?

JAWABU

Maswali kama haya yanatokana na watu kuitakidi kwamba kuwepo shetani ni jambo baya, na Mwenyezi Mungu hafanyi isipokuwa kheri na kuwepo shetani ni kinyume na itikadi yetu kuhusu Mungu.

Majibu ya mwaswali hayo ni mengi, na huu ni muhtasari:

1-Ndugu zangu, kuwepo shetani katika ulimwengu huu ni jambo zuri, na ni kheri lakini uzuri au kheri inamrejea yeye mwenyewe (shetani). Na halikadhalika kila kilichopo (kama Malaika, majini binadamu, mimea, wanyama) bilashaka kuwepo kila kimoja katika hivyo vilivyotajwa ni kheri kwake na kwa faida yake, kuliko kutokuwepo moja kwa moja.

Ama ubaya au uchafu utakaotokana na kuwepo kitu kile, utabakia kuwa ubaya vilevile, lakini bado asili inayotuhukumu, itaendelea kuwa ni ile tulioiashiria hapo kabla. Na mfano wa haraka kuthibitisha hilo ni kama ifuatavyo;

*Ni wanadamu wangapi wanaumbwa na baadaye kuwepo kwao kunahatarisha maisha ya wenzao, lakini haimaanishi kwamba asili ya kuwepo kwao ni ili waje kuwa na mazingira kama hayo. Na halikadhalika shetani kuwepo kwake ingawa ni hatari kwetu, lakini ni kheri kwake, na kwa sababu kama hiyo, ndio maana tunamkuta shetani alitumia fursa ya kuwepo kwake kujikamilisha, kwa kumuabudu sana Mwenyezi  Mungu , na alinufaika upande huo na huenda ibada aliyofanya hakuna yeyote katika wanadamu alimfikia isipokuwa wachache mno, kwa mfano, riwaya zinasema kwamba ,(Ibilisi) alisali rakaa mbili kwa muda wa miaka elfu moja ndipo alimaliza rakaa hizo. Mpaka Mwenyezi Mungu akampandisha cheo, akamfanya kuwa Malaika wa kweli, na kama hatutaamini hivyo basi Mungu alipowaamrisha Malaika wamsujudie Adam, kisha Ibilisi akakataa kusujudu, basi Mungu hana haki ya kumlaumu kwa amri iliotolewa iliwahusu Malaika na yeye si Malaika ni jini, kwa hiyo hatuna haki ya kumuita muasi, lakini kwa kuwa Mungu kutokana na ibada yake alimfanya kuwa Malaika wa kweli, ndio maana Ibilisi  mwenyewe hakusema hoja kama hiyo.

Tunarejea katika maudhui yetu, sasa mpaka hapo tunaona kwamba kama Ibilisi  asingekuwepo angewezaje kumuabudu Mungu kiasi hicho? Ukamilifu alioufikia mpaka Mungu kumfanya kuwa Malaika angefikaje kama angelikuwa hayupo? Mpaka hapo imethibiti kwamba Mungu haja umba kitu kibaya , na wala haja umba kwa lengo baya, kwa hiyo swali kwa nini alimuumba shetani? Jawabu kwa kuwa kuwepo ni kheri kwake kuliko kutokuwepo, kama tulivyobainisha.

Kwa nini Shetani aendelee kuwepo mpaka siku ya mwisho?

Jawabu:

*Kama atatokea mtu asali swala za usiku kwa lengo Mungu amfungulie milango ya riziki, siku ya Kiyama atamuuliza Mungu, ziko wapi thawabu za swala za usiku nilizo Sali duniani? Mungu atamjibu nilikufungulia milango ya riziki kama ulivyoniomba, na hizo ndio thawabu zako( yaani huna haki ya kunidai thawabu akhera maadamu lengo lako ulikusudia malipo ya duniani), na halikadhalika yeyote atakayefanya mema kisha akalenga kitu kingine tofauti na ridhaa ya Mungu au pepo, basi malipo yake ni kile anachokikusudia.

Na shetani pia alimuabudu sana Mwenyezi Mungu na siku hadi siku akawa akipanda daraja za ibada ( na ni wazi kwamba ibada zote hizo hakuzifanya bure pasi na malengo au madai yoyote kutoka kwa Mungu), kwa hiyo na yeye pia ana haki ya malipo kama vile yule aliyesali swala za usiku na malipo yake ikawa ni kufunguliwa milango ya riziki na kuendelea.

Kwa hivyo na shetani pia alimuomba Mungu, na Mungu akampa kama alivyowapa wengine.

Sasa madai au maombi ya shetani kutoka kwa Mungu ni nini?

Shetani alimuomba Mungu mambo mawili;

1)Alimuomba Mungu ampe umri mrefu, akisema;

Ewe Mola wangu! Nakuomba unipe kabakia (au kuwepo) mpaka siku ya ufufuo (Kiyama). Mungu akamjibu, hakika wewe utakuwa ni miongoni kwa watakaobakia mpaka siku hiyo iliyopagwa.

2)Kisha shetani alimuomba Mungu ruhusa ya kuichezea au kuimiliki mioyo ya binadamu na nafsi zao kama alivyosema;

(Mola wangu!) nitawarubuni wote kwa ujumla isipokuwa waja wako waliotakaswa. (Rejea surat Al_Hijiri, aya 30-36).

Kwa hiyo Mungu alimpa Ibilisi alioyataka kama malipo ya amali zake alizozifanya, na ni wazi kwamba alikuwa nastahiki kulipwa (kama tulivyosema hapo kabla) na Mungu alimpa kwa kiasi kile alichomuomba, na hayo uliyoyasikia ndio maombi yake. Kwa hiyo, hiyo ndio falsafa ya kuumwa shetani na kuendelea kuwepo mpaka siku ya Kiyama, na huu ni muhtasari mno.

Sh Swaleh Maulid

 

 

 

 

 

LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: