bayyinaat

Published time: 22 ,March ,2017      22:08:36
Baada ya tukio hilo Mtume aliyelekea nyumbani kwake na akamueleza mkewe (Bi Khadija) yote yaliyojiri, Bi Khadija (alikuwa ni mwanamke mwema mno) alimpongeza Mtume (s.a.w.w) kwa hilo, kisha akaamini utume wake, (kwa maana hii ni kwamba Bi Khadija ndiye mtu wa kwanza aliyeamini utume wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) kabla ya watu wengine kumuamini)...........
News ID: 60

1. Kipindi cha mwanzo wa Ujumbe

Mnamo tarehe 27 mwezi mtukufu wa Rajab, Mtukufu Mtume akiwa mkamilifu wa maumbile, na akiwa katika hali ya kusubiri ujumbe kutoka kwa Mola wake kwa ajili kuwaongoza watu kuelekea kwenye njia ya haki, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alipokuwa katika pango liitwalo (Hiraa) aliteremshiwa wahyi wa Aya tano za mwanzo wa Surat al Alaq ulioletwa na Malaika Jibril kutoka kwa Mola wake.

Jibril alimwambia Mtume soma.

Mtume akauliza: Nisome nini?

Jibril akasema:

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote!, Ambaye amefundisha kwa kalamu, Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui”.

Baada ya tukio hilo Mtume aliyelekea nyumbani kwake na akamueleza mkewe (Bi Khadija) yote yaliyojiri, Bi Khadija (alikuwa ni mwanamke mwema mno) alimpongeza Mtume (s.a.w.w) kwa hilo, kisha akaamini utume wake, (kwa maana hii ni kwamba Bi Khadija ndiye mtu wa kwanza aliyeamini utume wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) kabla ya watu wengine kumuamini).

Hivyo basi kuwepo kwa Bi Khadija karibu ya Mtume ilikuwa ni mchango mkubwa sana kwa Mtume wa kuweza kutangaza maamrisho aliyoshushiwa, kwani Bibi huyo alijitolea mali zake zote kwa ajili ya kutetea Uislamu na kuutangaza.

2. Mtume (s.a.w.w) kulingania watu kwa siri

Kwa kuwa mji wa Makka ulikuwa unaongozwa chini ya kivuli cha washirikina, na kwamba ulikuwa umechafuka na mila mbaya pamoja na potofu, Mtukufu Mtume aliona kutangaza Neno Allah moja kwa moja itakuwa si suala la kustahamilika, isipokuwa kwa watu wenye maarifa, hivyo alianza kutangaza dini tukufu kwa kuwalingania watu kwa njia ya siri, ili aweze kupata maandalizi na kuandaa mazingira ya kutangaza dini hiyo waziwazi.

Katika kipindi hiki cha daawa ya siri Mtume aliweza kufichua aibu na itikadi potofu za makafiri, na alipambana vikali dhidi ya dhulma na uonevu, Mtume aliendeleza daawa yake hii ya siri kwa muda miaka mitatu akiwa pamoja na mkewe Bi Khadija na Mtoto wa Ami yake Ali bin Abitalib (a.s).

Kulingana na maelezo ya Aya za mwanzo wa Surat : Hamd, Mudathir pamoja na Muzammil, zinaonyesha kuwa wadhifa wa kwanza katika daawa ya Mtume utakaowasaidia na kupeleka kufikia kwenye lengo la daawa ni kusimamisha Sala za wajibu, kwa sababu kufanya ibada mbalimbali ni sababu ya kustahamili masaibu na mikingamo.

3. Kuonya ukoo na ulinganiaji wa waziwazi

Kadri Mtume alivyokuwa akionya watu na kuwalingania kwa siri katika kipindi cha miaka mitatu, alipewa amri ya kuonya ukoo wake, na hapo Mtume akaalika ukoo wake kwenye chakula ambapo walihudhuria watu arobaini, alipotaka kuwahutubia, Abu lahab alisimama na kusema: Kwa hakika Muhammad amekurogeni, hapo watu wakatawanyika, lakini Mtume aliwaalika mara nyingine tena, na kabla hawajamaliza chakula, Mtume alisimama na kuanza kuwahutubia kwa kusema: Enyi wana wa AbdulMutalib, ninaapa kwa Allah ya kwamba hakuna kijana yeyote katika Waarabu aliyekuleteeni jambo bora kwa ajili ya masilahi ya duniani na akhera kama nililokuleteeni mimi, jambo ambalo ni kukulinganieni kumpwekesha Mwenyezi Mungu mtukufu. Hivyo ni yupi miongoni mwenu atakayenisaidia katika kuendeleza jambo hili?. Hakuna yeyote miongoni mwao aliyesimama na kumuunga mkono bwana Mtume zaidi ya Ali (a.s), Mtume akasema: huyu ndie atakayekuwa ndugu yangu na khalifa wangu baada yangu, hivyo mumtii na mumfuate.

Kwa kuongezea hilo ni kwamba Mtume kulingania kaumu yake ilikuwa ni hoja tosha kwa wengine na watakaotaka kujiunga na Uislamu, ili iwe ni kikomo kwa watoa sababu na visingizio ya kwamba Mtume ameruka mipaka, kabla ya kurekebisha na kulingania ukoo wake moja kwa moja ameanzia daawa yake nje ya ukoo wake.

4. Ulinganiaji jamii nzima

Mtume (s.a.w.w) katika hatua ya tatu ya daawa yake aliielekeza kwa jamii baada ya kupewa amri kutoka kwa Mola wake.

Na ilipokucha Mtume Alipanda juu ya mlima (wa Safaa) akaanza kunadi watu, hapo yakakusanyika makabila mbalimbali ili kumsikiliza ni jambo gani la muhimu analotaka kuwaeleza, Mtume alisema: Enyi watu, kwa hakika jambo hili ninalotaka kukuelezeni ni muhimu, hivyo maadui watalipinga na kulipiga vita, Je! Mpo tayari kulipokea na kunisaidia?. Walimjibu kwa kusema kwamba: Hakika sisi hatujawahi kusikia uwongo kutoka kwako.

Alisema: Hakika mimi ninakuonyeni kunako adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ninakuiteni mumuabudu Yeye pekee.

Abu lahab alimfanyia masihara juu ya daawa ya Mtume. Lakini Mwenyezi Mungu hakulifumbia macho suala hilo, hapo ndipo akashusha Suratul Masad, ikimkemea na kumfedhehesha.

Lengo la kutumwa Mtume

Mtume alitangaza daawa yake ambayo ilikuwa ni kuwatoa watu katika giza na kuwaongoza kuelekea kwenye mwanga na nuru, na aliwalingania kwa lengo la kumuabudu Mwenyezi Mungu pekee. Lakini makafiri hawakukomea hapo, na hapo ndipo yakajitokeza matabaka pinzani yaliyokuwa dhidi ya daawa ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ambayo ni haya yafuatayo:

1) Tabaka la kwanza lilikuwa linafuata mkumbo kwa amri ya viongozi wao

2) Tabaka lililokuwa limezoea mambo ya starehe za kidunia, hivyo walioona ikiwa watakubali dini ya Uislamu watakuwa wameachana na starehe hizo na watakuwa wamepungukiwa na mengi katika maisha yao.

3) Tabaka lililokuwa linajiona bora kuliko matabaka mengine katika jamii.

4) Tabaka lililokuwa na chuki ndani ya nyoyo zao na kutopenda maendeleo ya wengine.

5) Kundi ambalo nafsi zao zilizokuwa zimejaa uchafu wa kishirikina, ambapo lisingeweza kukubali na kufahamu thamani ya neema bora ya Allah (ambayo ni kumtuma Mtume wake kuja kuwalingania watu na kuwatoa katika giza na kuongoza kwenye mambo bora na adhimu duniani na pia akhera).

5. Sababu zilizopelekea washirikina kupinga daawa ya Mtume (s.a.w.w)

Baada ya kufahamu tabaka pinzani za washirikina wa mji wa Makka (waliopinga daawa ya Mtume na kumkadhibisha) na (kufahamu) sababu zilzopelekea kumpinga, pia hapa yalijitokeza makundi ya aina tatu, ambapo walikuwa:

ü Washirikina,

ü Wayahudi,

ü Na makafiri.

Na kabla ya kuelezea vitimbo vya washirikina dhidi ya Uislamu na Waislamu, ningependa kueleza kwanini walikuwa wakikhalifu daawa ya Nabii wa Mungu?!

Quran tukufu imeorodhesha sababu mbalimbali zilizopelekea washirikina wa Makka kutokubali Uislamu na kumpinga Mtume, sababu ambazo ni hizi zifuatazo:

Ø Kwanza walikuwa hawana matumaini ya Tawhid.

Ø Kwa sababu Mtume (s.a.w.w) alikuwa ni mwanadamu.

Ø Kwa sababu ya chuki waliokuwa nayo dhidi ya dini mpya (Uislamu).

Ø Kwa sababu kundi kubwa lililoanza kumuamini Mtume lilikuwa ni la watu mafukara na wanyonge.

Ø Walikuwa wakiitikadia jabr (ya kwamba kila walitendalo wamelazimisha na Muumba na hawana hiari ya kufanya lolote lile isipokuwa waliyokuwa wamelazimishwa kuyafanya).

Ø Walihofia kuporomoka nidhamu zao za kikabila.

Ø Wengi wao walikuwa wakitoa mambo yasiyokuwa na maana hata kidogo, na yasiyokuwa na uwezekano wa kulitekeleza.

6. Vitimbi vya washirikina wa Makka dhidi ya Uislamu na Waislamu

Kwa hakika kujitokeza dini mpya katika bara ya Waarabu ilikuwa ni mlio wa kengele wa hatari dhidi ya masilahi ya washirikina na waliokuwa wakiabudu masanamu, hivyo (washirikina hao) kwa kutaka kuendeleza mila zao na kutaka kuendelea kupata masilahi yao, walifanya juhudi kubwa sana na kuandaa mashambulizi makali ya kumpiga vita Mtukufu Mtume (s.a.w.w), pia walipanga mbinu za aina mbili dhidi ya Mjumbe wa Allah (s.a.w.w), ambayo ni haya yafuatayo:

1) Mbinu ya kwanza ni kumuangamiza Mtume na kumfanyia unyama kwa kila njia watakazoweza kuzitumia.

2) Kuzuia harakati za kimungu alizokuwa akizifanya, na kuzikomesha ili zisiendelee mbele.

Natija ya yote hayo ni kwamba:

Pamoja na vitimbi vyote hivyo, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu aliweza kuidhihirisha dini yake tukufu, na kuvifanya vitimbo vyao hivyo kuwa ni povu ndani ya maji. Na leo hii kila Mwislamu anajifaharisha na dini tukufu ya Kiislamu.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: