bayyinaat

Published time: 25 ,March ,2017      23:48:33
Imepokelewa kutoka kwa Mtume saww kwamba aliwauliza masahaba zake “je, hivi inashindikana kila mmoja wenu kwa usiku mmoja akasoma theluthi ya Quran?”. Wakasema “ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ni nani atakayeweza jambo hili?”.
News ID: 62

Surat Ikhlas

Ni sura iliyoteremka Makka, ina aya 4.

Mambo yaliyokusanywa na sura hii

Hakuna jambo la muhimu katika maisha ya mwanadamu, kama kumtambua mola wake na sifa zake kwa ujumla, kwani huo ndio msingi wa kila kitu katika imani na maisha yake kwa ujumla.

Hivyo basi sura hii imekuja katika swala zima la kuzungumzia kunako msingi huu wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu (swt).

Fadhila za kusoma sura hii

Imepokelewa kutoka kwa Mtume saww kwamba aliwauliza masahaba zake "je, hivi inashindikana kila mmoja wenu kwa usiku mmoja akasoma theluthi ya Quran?”. Wakasema "ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ni nani atakayeweza jambo hili?”.

Mtume akawaambia "someni surat ikhlas tu”.

Kwa hivyo basi ni kwamba sura hii ina nafasi sawa na theluthi ya Quran, lakini hii ni kwa kuzingatia kile ambacho tunakisoma na sio tu kwa kutamka ulimini.

Na pia imepokelewa kutoka kwa Sahal bin Saad kwamba siku moja alishitakia kwa Mtume ufukara na ugumu wa maisha, Mtume akamwambia "kila unapoingia ndani kwako, kama kutakuwa na mtu basi msalimie, na kama hakutakuwa na mtu basi toa salamu na soma surat ikhlas mara moja”.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ (1)

(1)Sema (ewe Muhammad) kwamba Mwenyezi Mungu ni mmoja.

Hili lilikuwa ni jawabu kwa ambao walikuwa kila siku wakimuuliza Mtume juu ya uhakika wa mola wake, kwani wao kila siku walikuwa wakimuuliza Mtume na kusema kwamba, huyo mola wako yupo vipi? Maana sisi miungu yetu unaiona ipo vipi.

اللَّهُ الصَّمَدُ(2)

(2) Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuelekewa kwa kila haja.

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ(3)

(3) Hakuzaa wala hakuzaliwa.

Aya hii tukufu inaashiria kunako sifa moja ya muhimu sana kwa Mwenyezi Mungu, sifa ambayo huwezi kuikuta kwa asiyekuwa yeye. Kama ambavyo pia ni jawabu kwa kila ambaye alikuwa na itikadi inayopingana na sifa hii, kwani ni jambo ambalo lipo wazi kwamba kuna baadhi ya wanaoamini kwamba kuna viumbe ambavyo ni watoto wa Mwenyezi Mungu swt, mfano ni manaswara ambao wao wanaamini ya kwamba Issa (as) ni mtoto wa Mungu, au Wayahudi ambao wanaamini kwamba Uzair pia ni mtoto wa Mungu, au hata baadhi ya Waarabu ambao walikuwa wakiamini kwamba malaika wote ni mabinti za Mungu. Sasa aya hii imekuja kwa ajili ya kuvunja mfano wa itikadi kama hizi kwa ujumla.

وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ(4)

(4) Na wala hakuna hata mmoja anayefanana naye.

Na kwa aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu ameweza kubainisha kwamba ametukuka kutokana nakila mapungufu ambayo yanapatikana kwa viumbe, kwani hakuna hata kiumbe kimoja ambacho kinafanana naye ili kiweze kushirikiana naye katika sifa zake.

Na hii ndio maana ya Tawhid, kwamba unampwekesha Mwenyezi Mungu katika dhati yake, kisha unakuja unampwekesha katika sifa zake.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: