bayyinaat

Published time: 26 ,March ,2017      22:40:17
Kutokana na durusu mbalimbali juu ya mwanadamu kama mwanadamu, na pia baada ya kubainisha maana halisi ya neno tamaduni, tunafikia katika maana ambayo nimeifanya kuwa ni kama kichwa cha habari na pia ni jawabu la kubainisha sababu halisi ya kuzalika kwa tamaduni.
News ID: 65

"MWANADAMU NI MWANATAMADUNI KIMAUMBILE”

Kwa kuangalia tu kichwa cha habari unaweza kufahamu kwa mbali ni jambo gani ambalo nataka kulizungumza hapa, lakini hakuna tatizo kama pia nitaendelea kulizungumza ili tuweze kuwa na uhakika kwamba ni jambo hilo ambalo unalifikiria au la?.

Kutokana na durusu mbalimbali juu ya mwanadamu kama mwanadamu, na pia baada ya kubainisha maana halisi ya neno tamaduni, tunafikia katika maana ambayo nimeifanya kuwa ni kama kichwa cha habari na pia ni jawabu la kubainisha sababu halisi ya kuzalika kwa tamaduni.

Kwanini nafikia kusema hivi? Hebu twende pamoja katika kurejea tena maana halisi ya mwanadamu na tamaduni. Tunaelezwa kwamba mwanadamu kama mwanadamu ni kiumbe ambaye ameumbwa hali ya kuwa akiwa na hali ya kupenda kuwa katika jamii ya wenzake, kwa maana ya kwamba mwanadamu hapendi kuwa peke yake na kujitenga hata kama itakuwa ni wa aina gani, na ndio maana inapotokea mwanadamu huyu akatengwa na wenzake au hata yeye akajitenga na wenzake basi huhisi kwamba kuna kasoro fulani katika nafsi yake, na hali hii inakuwepo hata kama mwanadamu huyu hatopenda kuidhihirisha kutokana na sababu katika sababu zake, huenda labda kuidhihirisha kwake itapelekea ajione kwamba ni dhaifu mbele ya jamii anayoishi au sababu nyengine ambazo zinaweza kuwa kizuizi katika kudhihirisha hali ile ya kasoro, Huyu ndio mwanadamu kutokana na tafiti na durusu mbalimbali juu yake na jinsi gani ambavyo anajihisi katika nafsi yake kwamba anahitajia kuwa katika jamii ya wenzake.

Sasa njoo tena turejee katika maana halisi ya tamaduni ambayo tuliielezea hapo mwanzoni, tulifikia katika natija ya kwamba tamaduni ni mkusanyiko wa watu maalumu na namna ambavyo mkusanyiko huu unashiriki katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao, huku kukiwa na haja ya watu hawa kuwa na uelewa wa mambo ya watu waliopita.

Sasa tukijumuisha mambo haya mawili tunapata natija ya kwamba, kutokana na kwamba mwanadamu ni kiumbe ambaye ameumbwa katika hali ya kupenda kuwa katika mkusanyiko, na kwamba mkusanyiko ni lazima kutakuwa na changamoto ambazo wanakabiliana nazo, na katika kukabiliana nazo bila shaka kutakuwa na njia ambazo wanatumia, basi bila shaka mwanadamu huyu atakuwa ni mwenye maumbile ya tamaduni na jamii kwa ujumla. Kwa maana ya kwamba atakuwa ni mwenye hali ya kupenda siku zote kuwa ni mwenye kukabiliana na changamoto na pia mwenye hali ya kupenda kuwasilisha aliyo nayo kwa mwenzake, na hapa sasa ndio inakuja nafasi ya yale mambo ambayo tuliyataja mwanzoni na kusema kuwa sio sababu ya msingi katika kupatikana kwa tamaduni, kama vile lugha na shughuli nyinginezo ambazo anazisimamia mwanadamu.

Kwa mantiki hii ni kwamba sababu ya asili kabisa katika kupatikana tamaduni ipo ndani ya mwanadamu mwenyewe kwa anuani ya maumbile yake, na mwanadamu hawezi kuepukana na maumbile haya hata siku moja, kwani ni katika asili yake. Na ndipo ambapo tunakuta Mwenyezi Mungu anasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآياتٍ لِلْعَالِمِينَ

"na miongoni mwa alama zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kisha kuzitofautisha ndimi na hata rangi zenu, na hakika katika hayo kuna mazingatio kwa walimwengu..”1

Kwamba asili na maumbile ya wanadamu ni kutofautiana katika nyanja mbalimbali, lakini kukiwa na lengo la wao kuweza kufikia katika jambo fulani.

Kwa hiyo mpaka hapa tunakuwa tumeweza kubainisha na kuelezea uhalisia wa sababu zinazopelekea kudhihiri au kupatikana kwa tamaduni.[1] Suratul rum aya 22

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: