bayyinaat

Published time: 09 ,May ,2017      12:23:15
Moja: Mtume alikuwa akimwambia Hamza mambo ambayo kila mwanadamu anatakiwa ayaamini ili tu atakapokutana na mola wake siku ya mwisho akutane naye hali ya kuwa ni mwanadamu aliyekamilika kuanzia kimwenendo mpaka kiitikadi. Na hii ni kutokana na msingi ambao Mwenyezi Mungu ameuweka pale aliposema.....
News ID: 85

UMUHIMU WA MASWALA YA ITIKADI KATIKA MANENO YA MTUME (SAWW) NA MAIMAMU

Kutokana na umuhimu wa swala zima la itikadi ya mwanadamu katika maisha yake ya hapa duniani mpaka kesho siku ya mwisho, nimeona ni vyema kujadili jambo hili kwa kupitia maneno ya Mtume (saww) pamoja na maimamu, ili tuweze kuona je, wao pia walitilia umuhimu swala hili au la?. Na hapa tutajaribu kuja na riwaya ambazo zimepokewa kutoka kwao na kisha kuchambua nukta muhimu katika maneno hayo.

SEHEMU YA KWANZA

MANENO YA MTUKUFU MTUME (SAWW)

Ni jambo lililo wazi kabisa kwamba mtukufu mtume (saww) alikuwa mstari wa mbele kabisa katika kuhakikisha kwamba jambo la itikadi linathibiti kwa ukamilifu katika vifua vya Waislamu kwa ujumla, na ili kubainisha hili tunaleta riwaya ambayo imepokelewa katika kubainisha baadhi ya mambo ya muhimu katika itikadi. Inapokelewa kwamba baada ya kujeruhiwa vibaya Hamza katika vita ya Uhud, na akawa yupo katika nyakati za mwisho za kuaga dunia alijiwa na bwana mtume na kuanza kuthibitishwa katika mambo muhimu ya itikadi, na riwaya yenyewe ni kama ifuatavyo:

Kutoka kwa Mussa bin Jaafar, kutoka kwa baba yake ambaye amepokea kutoka kwa babu yake ambaye amesema "...Ulipofika usiku ambao Hamza alikuwa anafariki, alijiwa na bwana Mtume na kuambiwa : ewe Hamza na mjomba wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hakika naona upo katika kuelekea safari yako ambao hatutakuona tena, je, utajibu nini endapo utakutana na mola wako na akakuuliza juu ya maswala ya kisheria na misingi ya dini yako?. Hamza alilia sana kisha akasema "niambie na nielekeze ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu”. Mtume saww akasema: kwanza kabisa unatakiwa utoe shahada ya kwamba hakuna mola isipokuwa mmoja tu na hali ya kuwa ukiwa na imani juu ya hilo, na pia ukubali kwamba mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu na nimetumwa kwa haki”. Hamza ra akajibu "hakika nashuhudia hayo”, kisha mtume akasema "na pia ushuhudie kwamba moto na pepo ni haki ya kweli, na kwamba siku ya mwisho ipo, na kwamba kuna kuvuka katika "sirat”, na kwamba kuna mizani ambayo itapima jambo liwe dogo au kubwa na kisha kuonyeshwa kwa mtendaji, na kwamba kuna ambao wataingia motoni na kuna ambao wataingia peponi, na kwamba Ally as ni kiongozi wa waumini, na maimamu watokanao na kizazi chake ni maimamu wa kweli. Hamza akajibu kwa kusema "nimeshuhudia”. Kisha Mtume akasema: na pia ushuhudie kwamba Fatima ni kiongozi wa wanawake wote wa ulimwenguni, na kwamba Hamza ni kiongozi wa mashahidi wote, na ni simba wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na pia ni mjomba wa Mtume pia”. Hamza akajibu huku akilia "naam nashuhudia hayo pia”. Kisha mtume akasema: na pia ushuhudie kwamba ndugu yako Jafar yupo peponi pamoja na malaika, na kwamba Muhammad saww ndiye mbora wa viumbe wote, na kisha uamini kunako siri zao na ya dhahiri yao, na ufe ukiwa na imani hiyohiyo. Hamza akajibu "nashuhudia hayo pia”. Kisha mtume saww akasema "Mwenyezi Mungu akuafikishe na akutie nguvu”.[1]

Mafunzo kutoka katika riwaya hii

Hakika kwa kila mwenye kusoma riwaya hii na kuiangalia kwa jicho la tatu basi ataweza kugundua mambo muhimu ambayo ni:

Moja: Mtume alikuwa akimwambia Hamza mambo ambayo kila mwanadamu anatakiwa ayaamini ili tu atakapokutana na mola wake siku ya mwisho akutane naye hali ya kuwa ni mwanadamu aliyekamilika kuanzia kimwenendo mpaka kiitikadi. Na hii ni kutokana na msingi ambao Mwenyezi Mungu ameuweka pale aliposema:

و ان ليس للانسان الا ما سعي

" Na kwamba mwanadamu hatapata ila yale aliyoyatendea kazi”[2]

Ikiwa na maana kwamba kila ambacho mwanadamu atakipata siku ya kiyama basi msingi wake ni juhudi zake hapa duniani, na juhudi hizi haziangalii nyanja fulani bila ya nyingine, na bila shaka nyanja ya itikadi ni miongoni mwa nyanja muhimu sana katika kuhakikisha kwamba mwanadamu huyu anafaulu siku ya kiyama. Na miongoni mwa itikadi muhimu mno kwa mwanadamu ni itikadi yake juu ya Mwenyezi Mungu ambapo inatakiwa aamini kwamba yupo peke yake na kisha kufanya matendo yote hali ya kuwa unamtegemea yeye, iwe ni katika mambo ya itikadi yenyewe au hata utendaji kwa ujumla. Na hapa ndipo tunaweza kufahamu maana ya maneno ya Imamu Ally as pale aliposema:

اول الدين معرفته.......

"Jambo la kwanza katika dini ni kuijua dini yenyewe”

Na vipi utaweza kuijua dini ikiwa haumjui mwenye dini?. Hivyo kuna umuhimu wa kumjua muumba na kumtukuza kwa kila namna ikiwa tunataka kukutana naye hali ya kuwa ni wenye kufaulu.

Kisha Mtume akaashiria swala la itikadi muhimu ya utume wake, kisha akaashiria swala la uimamu wa Imamu Ally as.

Bila kusahau pia alikuja kubainisha nafasi mbalimbali za watu muhimu katika Uislamu na kwamba kuamini nafasi zao hizo pia kuna nafasi kubwa mno katika ufaulu wa mwanadamu siku ya kiyama. Hivyo ni wajibu wa kila Mwislamu kuweza kukipa nafasi yake kila ambacho kimepewa nafasi katika dini ili tu aweze kufikia katika ufaulu mkubwa siku ya mwisho.[1] Biharul anwar juz 22 uk 298 hadithi ya 32

[2] Surat Najm aya 39

LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: