Faida za kisomo cha Surat Alfatiha

Imepokelewa kutoka kwa Amirul muumin Ali bin Abitalib (a.s) kuwa amesema: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) kuwa amesema Mwenyezi Mungu mtukufu: Nimeapa kwa kupitia suratul Fatihah baina yangu na Mja wangu, hivyo nusu (Sura hiyo) ni yangu na nusu nyingine ya Mja wangu, na nusu nyingine kwa lile aliombalo.

1. Atakaposema Mja wangu: (بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ) (Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema mwenye kurehemu), Mungu atasema: Mja wangu ameanza kwa jina langu, na ni haki yangu kutimiza mambo yake na kuibariki hali yake.

2. Na atakaposema: (الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ) (Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu Bwana wa Ulimweng) atasema Allah mtukufu: Mja wangu amenihimidi Mimi, na akatambua kuwa Neema alizonazo ni kutoka kwangu, hakika nitamuepushia Balaa, na ninakuhakikishieni nitamzidishia neema za Dunia na neema za Akhera, nitamuondolea Balaa ya Siku ya Akhera kama ninavyomundolea za Duniani.

3. Na atakaposema sema: (الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ) (Mwingi wa rehema mwenye kurehemu) atasema tena Allah: Ameshuhudia kuwa Mimi ni Mwingi wa rehema mwenye kurehemu, ninakuhakikishieni tena kuwa nitamjazia Rehema zangu tele na kumjazia bahati njema za Maisha yake, na nitamlipa mengi katika yale niyatoayo kwa waja wangu.

4. Na akisema: (مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ) (Mfalme wa siku ya mwisho) Allah atasema tena: Ninakuhakikishieni kama alivyokiri Ufalme wangu wa siku ya mwisho, nitamsahilishia hesabu ya malipo yake, na nitakubali mema yake, na nitamsamehe makosa yake.

5. Na akisema: (إِيَّاكَ نَعْبُدُ ...) (Wewe pekee ndiye twakuabudu…), Allah atasema: Amesema kweli Mja wangu Mimi pekee ndiye mwabudiwa, na ninakuhakikishieni tena nitamlipa thawabu Mja wangu kwa Ibada zake ambazo zitamfunika kila atakayelingana naye katika kuniabudu Mimi.

6. Na akisema tena: (... وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ) (Wewe pekee tunakuhitajia), atasema Allah: Hakika amenitegemea Mimi na kuelekeza matatizo yake kwangu, ninakuhakikishieni nitamsaidia katika mambo yake yote, na nitamsaidia katika Dhiki na nitamshika Mkono katika matatizo yake.

7. Na akisema: (اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ) (Tuongoze njia iliyonyooka) hadi mwisho wa Sura, Allah atasema: Hii kwa ajili ya Mja wangu, na kwa ajili ya lile aliloniomba, nimekwisha mjibu Mja wangu na nimempa alilotarajia kutoka kwangu, na nimempa salama kwa aliloliendea.

FAIDA ZA SURATUL FATIHAH TUKUFU

1. Imepokelewa ya kuwa Suratul Fatihah ni ponyo/ shifaa ya kila huzuni, na kuwa sura hiyo ni ponyo ya kila maumivu na magonjwa na yeyote atakayeiandika sura hiyo katika chombo kisafi, na akakiosha kwa maji ya mvua hakika maji hayo yatakuwa ni ponyo ya kila maradhi kwa atakaye kunywa au kuoga.

2. Soma suratul hamd mara 40 juu ya chombo cha maji, kisha mmwagie mgonjwa na utoe sadaka kwa niaba ya mgonjwa, kisha muombe fukara kumuombea mgonjwa Mungu amuafu mgonjwa.

3. Yeyote atakayesoma sura hiyo mara 41 kila siku kwa muda wa siku arobaini kuanzia siku ya Ijumaa, na akasoma baada yake dua hii mara 13: (یا مفتح فتح، یا مفرج فرج، یا مسبب سبب، یا میسر یسر، یا مسهل سهل، یا متمم تمم، وحسبنا الله ونعم الکیل) na utakapo sahau siku hiyo anza siku nyingine, na atakaye fanya hivyo kwa nia safi na uchamungu na kuihudhurisha nafsi atafikia nafasi ya juu bila pingamizi.

4. Soma suratul hamd mara 1011 bila kuchelewa wala kulala, kisha omba haja yako.

5. Kutoka kwa Salama bin Muhammad amesema: Nilimsikia Imam Sadiq (a.s) anasema: Asiyeponywa na Al-hamd hakuna kingine kitakachomponya.

6. Na yeyote atakayeisoma mara arobaini mwisho wa usiku atapata riziki bila taabu na mashaka ya usumbufu.