Maulid na Usahihi wake -3 Je, Maulid ina msingi katika dini au la?

Katika kujibu swala hili ndugu yangu moja kwa moja nitakupeleka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt), ili tuone kwanza je kuna msingi kama huo ambao unakuwa ni wenye kukusanya jambo la Maulid au la?.

Bila shaka hakuna hata Mwislamu mmoja ambaye atapinga kwamba katika Quran kuna aya ambazo ni zenye kuhimiza Waislamu kunako swala la kumkirimu, kumtukuza, awe hai au hata baada ya uhai wake pia. Ila sasa ni namna gani ambavyo tunatakiwa kumkirimu na kumtukuza hilo ni jambo ambalo wameachiwa Waislamu waweze kulifanyia kazi, cha muhimu ni kwamba kulindwe misingi na mipaka ya kisheria.

Mwenyezi Mungu anasema "

....... فالذين آمنوا به وعزّروه ونصروه واتّبعوا النّور الذي اُنزل معه اُولئك هم المفلحون

.............Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa......”[1]

Ambapo wafasiri wamejaribu kutuambia kwamba neno (Taazir) halina maana sawa na neno (Nusra), kwa dalili ya kwamba kama ingalikuwa yana maana moja basi Mungu asingeyarudia mahala hapo, na ndio maana wakafasiri neno hilo kwa maana ya Heshima n a kutukuza. Hivyo basi kuna umuhimu wa kumtukuza bila ya kikomo, kwa sababu kauli hiyo imekuja bila kikomo, kwa maana ya kwamba kusema kwamba asifiwe wakati wa uhai wake tu, ama baada ya uhai wake watu wakatishe, la hasha.

Aya nyingine ni pale Mungu aliposema:

إن الله وملائكته يصلّون على النبي يا أيها الذين آمنوا صلّوا عليه وسلّموا تسليماً

"......Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu….”.

Ambapo Mungu anawaamrisha Waislamu kwamba wawe ni wenye kumswalia n a kumkumbuka Mtume wao kwa sala na salamu, kwa sababu tu jambo hili lina daraja kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani hata yeye Mwenyezi mwenyewe pamoja na malaika wake wanafanya jambo hili. Cha muhimu hapa pia ni kwamba amri hii imekuja bila ya kikomo, hivyo swala hili litaendelea kuwepo bila ya kikomo.

Hizi ni baadhi tu ya aya ambazo ni zenye kulenga umuhimu wa kumtukuta na kumkumbuka Mtume, ngoja tuangalie riwaya moja pia kisha tutoe natija katika jambo hili.

Imepokelewa kwamba siku moja Omar bin Khatwab alimwambia Mtume (saww) "....Ewe Mtume, kwa hakika wewe nakupenda kuliko jambo lolote isipokuwa nafsi yangu”, Mtume akasema "....Naapa kwa ambaye nafsi yangu ipo mikononi mwake, sitokuwa mpenzi wa mtu mpaka pale ambapo atanipenda zaidi ya nafsi yake”, Omar akasema "....Oooh, basi kuanzia sasa nakupenda hata kuliko nafsi yangu”, kisha Mtume akasema "...Sasa hivi ewe Omar?!”.[2]

Hivyo basi kwa aya na hadithi hizo, tunafikia katika natija zifuatazo, kwanza ni kwamba swala la kumsifu na kumtukuza Mtume ni swala ambalo lipo na lina misingi katika dini yetu, pili ni kwamba mbali na kuw ania misingi pia ni jambo ambalo imekokotezwa sana na Mtume mwenyewe na hata Mwenyezi Mungu pia. N akisha ndipo linakuja swala la namna gani watu wamsifu n a kumtukuza Mtume huyo, ambapo pia tumeeleza kwamba kipimo cha jambo hilo ni kwamba watu wasitoke katika misingi sahihi ya dini, kama vile kufanya maasi, kutochunga misingi ya Hijabu kwa kina mama, na mengineyo mengi ambayo yanaweza kuchafua sura ya Kiislamu katika kuadhimisha mambo haya.

Pia niashirie nukta ya muhimu ambayo ni, kuna baadhi ya watu wanaweza kusema kwamba sawa jambo hili lina msingi katika dini, lakini kutokana na kwamba kwa namna ambayo watu wanalifanya na kuliadhimisha ndio maana sisi tunalikataza na kulikemea.

Nasema: namna ya watu wanavyofanya na kuadhimisha jambo hili haina mshikamano wala mafungamano na uhalali au uharamu wa jambo hili, ni sawa n a uje usema kwamba kuanzia leo swala unaikataza kwa kuwa tu kuna watu ambao wanaswali kwa mchezo katika swala zao, haiingii akilini hata kidogo, bali badala yake inatakiwa njia sahihi za kuelimisha watu kunako jambo husika zifuatwe na sio kukataza kabisa jambo hilo.

Tukutane tena katika mwendelezo wa mada hii yenye lengo la kuelezea dalili za kutetea uadhimishwaji wa mazazi ya Mtume (saww).[1] Al Aaraf 157

[2] Siirat bilighatil Hub bwa Shiir 15