Njama za madola ya Magharibi za kuvuruga umoja wa Waislamu


Madola ya Magharibi na maadui wa Uislamu wakiwa na shabaha ya kufikia lengo lao hilo wamekuwa wakitumia nyenzo na suhula mbalimbali kama vile filamu, vitabu, magazeti na intaneti na hivyo kutaka kuonyesha taswira kwamba, Uislamu ni dini hatari na tishio. Kisha hutaka kuwaonyesha kwamba, hatari hiyo yaani Uislamu imo katika hali ya kuenea kwa kasi na muda si mrefu itaingia Ulaya na Marekani.

Maadui wa Uislamu wamekuwa wakiutuhumu Uislamu kwamba, ni dini ya kutumia mabavu na kwamba, inapinga haki za binaadamu na kwa msingi huo kufanya njama za kuwaogopesha na Uislamu wananchi walioko katika ulimwengu wa Magharibi. Hata hivyo kinyume kabisa na hima na juhudi zao hizo, ukweli wa mambo ni kuwa, hivi sasa kuna watu wengi katika ulimwengu wa Magharibi ambao wamesilimu na kuingia katika Uislamu na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi mno. Uchunguzi unaonyesha kwamba licha ya njama za maadui dhidi ya Uislamu, lakini wimbi la muelekeo wa kupenda Uislamu na mafundisho yake linavuma kwa kasi mno. Wanaoingia katika Uislamu huko katika ulimwengu wa Magharibi wanasema kuwa, sababu ya wao kuikubali dini ya Kiislamu ni kwamba, dini hii inaheshimu thamani za mwanaadamu na ina mafundisho ambayo yana hoja za kimantiki na ambazo zinaingia akilini.

Juhudi za Imam Khomeini katika kuleta umoja miongoni mwa Waislamu

Kutokana na uongozi shupavu na wa busara wa Imam Khomeini (MA), Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameweza kudhihirisha muujiza wa umoja katika karne hii. Kwa kufuata kikamilifu miongozo ya Qur'ani Tukufu ambayo inawataka Waislamu kuwa na umoja na pia kuungana na wafuasi wa dini nyinginezo zinazompwekesha Mwenyezi Mungu, Imam Khomeini (MA) alitoa wito wa kuwepo umoja miongoni mwa madhehebu zote za Kiislamu na hata wafuasi wa dini nyingine, kushirikiana kwa pamoja chini ya kivuli cha Mapinduzi ya Kiislamu. Ni wazi kuwa umoja hapa hauna maana ya wafuasi wa madhehebu na dini tofauti kuacha imani zao na kufuata itikadi moja lakini una maana ya kwamba licha ya kuwepo tofauti za kiimani na kiitikadi lakini wote wanapasa kuimarisha umoja na kushirikiana kwa msingi wa kuheshimiana na kuzingatia udugu baina yao. Tofauti zilizopo zinapaswa kuchunguzwa na kujadiliwa si kwa njia za kawaida na za kijuu juu tu bali kwa mbinu za kielimu, kitaalamu na katika mazingira yaliyo mbali na dharau, matusi na kukufurishana ili ukweli wa mambo upate kufahamika.
Kwa kuwa na mtazamo wa kina na mwamko wa kupigiwa mfano na katika hali ambayo ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa umedhoofishwa pakubwa na hitilafu za kikabila na kimadhehebu, Imam Khomeini (MA) alifanikiwa kulifahamisha taifa la Iran udharura wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu na hivyo kuzuia kutokea mgawanyiko katika jamii hii ya kimapinduzi, kupitia hotuba zake za hamasa na mwamko. Alisema: 'Leo ni siku ambayo makundi yote ya Kiislamu yamesimama mkabala na nguvu za kishetani ambazo zinataka kufuta msingi wa Uislamu, nguvu ambazo zimetambua kwamba kitu ambacho ni hatari kwao ni Uislamu na umoja wa mataifa ya Kiislamu. Leo ni siku ambayo Waislamu wa nchi zote za dunia wanapasa kushikamana.' Imam Khomeini (MA) alikuwa akisema: 'Katika Uislamu, lugha, kabila na sehemu havitambuliki (havipewi umuhimu). Waislamu wote, wawe ni Masuni au Mashia, ni ndugu na wote ni sawa, na wote wananufaika na fursa na haki za Kiislamu. Usuni na Ushia haujadiliwi kwenye Uislamu wala Mkurdi na Mfursi, wote ni ndugu." Si taifa la Iran tu, bali Imam Khomeini aliwataka Waislamu wa mataifa yote bali wanyonge wote wa ulimwengu bila kujali dini zao kuwa na umoja mbele ya uistikbari wa dunia. Hata hivyo alitilia mkazo sana umoja baina ya Shia na Suni katika nchi za Kiislamu. Aliamini kuwa jambo lililowadhoofisha Waislamu wengi na kuwafanya wadhalilishwe duniani ni mfarakano ulio baina yao. Alikuwa akisema: 'Hitilafu zinazoletwa nchini Iraq, Iran na nchi nyigine za Kiislamu zinapasa kutiliwa maanani na viongozi wa serikali za Kiislamu na kutambua kwamba hitilafu hizo zitafuta nguzo yao. Wanapasa kutambua kwa kutumia akili na busara kwamba wanataka kuufuta Uislamu kwa kisingizio cha madhehebu na Uislamu. Mikono miovu ambayo inazua hitilafu miongoni mwa Mashia na Masuni katika nchi hizi sio Mashia wala Masuni halisi. Hii ni mikono ya wakoloni ambayo inataka kudhibiti nchi za Kiislamu kupora utajiri wao na kuanzisha masoko ya magendo katika nchi zinazotajwa kuwa zimeendelea.'

Nafasi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kuleta umoja katika umma wa Kiislamu

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya tarehe 11 Februari 1979 ulikuwa ni mwanzo wa kutokea mabadiliko makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla, kutokana na athari kubwa ya mapinduzi hayo kimataifa. Hayo ni mapinduzi matukufu ambayo yalifanyika kwa kutegemea imani na itikadi za dini tukufu ya Kiislamu chini ya kaulimbiu ya "si Mashariki na si Magharibi" na kufanikiwa kuunda Jamhuri ya Kiislamu katika nchi hii baada ya kuuangusha utawala wa kiimla wa Shah. Mapinduzi ya Kiislamu ni moja ya matukio muhimu na makubwa sana katika karne ya hivi sasa na imekuwa na matunda mazuri mno ndani ya Iran na nje ya Iran.

Roger Garaudy, msomi Muislamu wa nchini Ufaransa aliandika makala kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran akisema: Kwa kweli Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini (MA) hayafanani hata kidogo na mapinduzi yoyote mengine yaliyotokea huko nyuma. Katika kipindi chote cha historia, yamekuwepo mapinduzi ya kila namna yaliyofanyika kwa lengo la kubadilisha mfumo wa kisiasa katika nchi mbalimbali, lakini mapinduzi yote hayo hayafanani hata chembe na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kumetokea pia mapinduzi ya kijamii duniani ya kuonesha hasira za watu masikini dhidi ya matajiri. Kumetokea pia mapinduzi ya kitaifa, ya wananchi ili kuonesha hasira zao dhidi ya wakoloni na watu waliopora ardhi zao. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran nayo yalikuwa na misukumo yote hiyo. Hata hivyo mapinduzi hayo, mbali na masuala tuliyoyataja, yamekuja na maana mpya na si kwamba yamepindua utawala wa kisiasa, kijamii na kikoloni tu, bali muhimu zaidi ni kuwa, yameupindua utamaduni na mtazamo maalumu uliokuwepo duniani kuhusiana na dini.

Miongoni mwa taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kutia nguvu udugu wa Kiislamu na kuleta na kuimarisha mshikamano kati ya Waislamu. Mapinduzi hayo yalifufua hima ya kuzingatia mafundisho ya Qur'ani Tukufu na sira tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kuweka msingi wa umoja wa Kiislamu na kuleta kigezo cha mshikamano na utangamano kati ya Waislamu.
Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, tangu awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa mwito kwa Waislamu wote duniani kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kukabiliana na watawala madikteta na maadui wa Uislamu. Alisisitiza mara nyingi kuwa siri ya kuweza mataifa ya Waislamu kurejesha heshima yao ni kufungamana na kuwa na kauli moja.
Katika moja ya matamshi yake, Imam Khomeini alisikika akisema: Enyi Waislamu duniani ambao mnauamini kikweli Uislamu! Simameni na muungane pamoja chini ya bendera ya tauhidi na chini ya kivuli cha mafundisho ya Uislamu ili kukata mikono ya madola ya kibeberu yanayopora utajiri wa nchi zenu na rejesheni heshima ya Uislamu kwa kujiweka mbali na mizozo na matamanio ya nafsi. Tambueni Waislamu kuwa nyinyi mna kila kitu.