Antony Flew na uwepo wa Mungu

Tunapozungumzia jambo la kuamini kwamba kuna Mungu basi lazima tutambue ya kwamba si kila mmoja wetu anakubaliana nalo, kwa maana kuna ambao mpaka leo hii bado wameshikamana ni misimamo yao ya kwamba jambo la kwamba kuna Mungu si jambo la hakika bali ni mitazamo tu ambayo watu wanaamua kuijenga.

Na ili kuthibitisha jambo hili inatutosha tu kurejea katika jamii zetu na kuona kwamba kuna wangapi ambao hawakubaliani na uhakika wa kwamba kuna Mungu?, natumia neno Uhakika wa uwepo wa Mungu nikiwa na maana ya kwamba hao wanaoamini kinyume na haya basi ni kwa ndimi zao tu, lakini kama utarejea ndani ya nafsi zao basi utakuta wanakubaliana na Uhakika huu, kama ambavyo tukipata nafasi tutakuja kuzungumzia uwanja huu wa kwamba Mungu anaweza kuthibitishwa uwepo wake kwa kutumia nafsi zetu tu bila hata ya jambo la ziada.

Kwa sasa acha tukubaliane na vigawanyo hivi ya kwamba kuna ambao wana amini uwepo wa Mungu na kuna ambao hawaamini uwepo wake, kisha tuingie katika kiini cha ninachotaka kuzungumzia hapa.

Cha msingi ni kwamba pamoja na uwepo wa watu ambao hawana imani ya uwepo wa Mungu, haina maana kwamba basi maisha yao yote ndio wanalazimika kuwa hivyo, kama ambavyo pia hata hao wanaoamini uwepo wa Mungu haina maana kwamba wanabakia hivyo miaka yote, nikiwa na maana kwamba kuna wakati mwanadamu anaamua kuachana na imani yake ya kwamba hakuna Mungu na kushikamana na imani ya uwepo wa Mungu, au wakati mwingine pia ikawa ni kinyume na hivyo.

Jambo hili pia lipo wazi kutokana na historia ambazo zimeandikwa katika ulimwengu huu, kwamba wapo ambao wameachana na Imani moja na kushikamana na imani nyingine. Ila katika nafasi hii ningependa kuzungumzia moja ya watu ambao wamekuwa ni moja ya mifano hai katika jambo hili, hapa namzungumzia Antony Flew, moja ya wana falsafa maarufu sana wa Kiingereza katika karne ya 21.

Mwanafalsafa aliyeamua kuachana na imani yake ya kutokuwepo na Mungu, mpaka kujiunga na Uislamu ikiwa kama moja ya dini ambazo zinaamini kwamba kuna Mungu, na hakuishia hapo bali mpaka akaamua kutunga kitabu alichokipa jina la "There is a God” akiwa na maana ya kwamba "Kuna Mungu”.

Jambo la muhimu na ambalo pia nataka kuzungumzia hapa si kwamba eti Antony ameamua kutamka hadharani kwamba kuna Mungu, au ameamua kutunga kitabu katika kuthibitisha hilo, la hasha!, bali hapa nataka kuashiria kunako mambo muhimu yaliyopelekea mpaka wakaamua kufanya mambo hayo au kuchukua hatua hiyo. Hivyo yafuatayo ni mambo ambayo yamempelekea Antony kuchukua maamuzi hayo kwa mujibu wa maneno yake mwenyewe ambayo yanapatikana katika kitabu chake hicho.

Nasi kwa uwezo wa Mungu tutajaribu kuchambua na kuelezea kwa upana hayo mambo ambayo ni kama dalili alizotumia katika kuthibitisha uwepo wa Mungu, kama ambavyo pia tutajaribu kuangalia misingi ya mambo hayo.

Antony anaanza kwa kusema ".........Nimefikia katika natija ya kwamba ulimwengu umepatikana kutokana na muumba ambaye yu hai, na pia kila nidhamu na mpangilio uliopo katika ulimwengu huu vinaashiria uwepo wa huyu ambaye tunaweza kumwita Mungu....”

Ufafanuzi:

Maana ya kauli yake hii ni kwamba anataka kutuambia ya kwamba, ulimwengu kama ulimwengu kuna wakati ulikuwa haupo kisha ukaja ukapatikana, lakini sasa katika upatikanaji wa ulimwengu huu ambao tunashuhudia kila aina ya nidhamu na mipangilio ya hali ya juu, je kuna ambaye amehusika na hili au la?, hapo mwanzoni alikuwa hana imani kwamba kuna ambaye amehusika na hili, lakini sasa hivi ana imani kwamba yupo, tena si yoyote anaweza kuhusika na jambo hili, bali ni lazima awe ni mwenye upeo wa hali ya juu mno katika mambo ya upangiliaji na nidhamu.

Sasa jaribu kumchukua mwanadamu ambaye unaamini kwamba ana upeo wa hali ya juu sana katika upangiliaji, kisha uone je, ana uwezo wa kuweka mpangilio thabiti kama ambao unapatikana katika ulimwengu huu?, bila shaka hapana, kutokana na kwamba tumeona katika ulimwengu watu ambao walijidai wana upeo mkubwa katika kupangilia mambo, lakini zama zikaja zikawaonyesha kwamba hawapo sahihi bali ni wenye kukosea. Na ndio maana Bw Antony akafikia katika natija ya kwamba ambaye anaweza kuhusika na upangaji huu kamili ni ambaye yupo juu ya upeo wa mwanadamu, naye si mwingine bali ni Mungu peke yake.

Anaendelea kusema "......Kwanini nimefikia katika natija hii?, baada ya kuwa ni mpingaji wa jambo hili kwa miaka mingi mno?, ni kwamba nimegundua kwamba:

1. Ulimwengu una mwanzo, kwa maana ya kwamba haukuwepo kisha ukawepo.

2. Ni kwamba maisha ya kitabia kwa ujumla yapo katika mfumo wenye mafungamano

3. Akili sahihi......”.

Ufafanuzi:

Hakuna mwenye kubisha kwamba katika ulimwengu huu kuna mpangilio wa hali ya juu sana, n akama atapatikana basi itakuwa hajaelewa ni mpangilio upi upo katika hicho atakachobishia nacho. Pia hakuna atakayebisha kwamba ulimwengu na hii mipangilio yote ni kwamba hapo mwanzoni haikuwepo, bali ilikuja kipindi ikaanza. Sasa hapa ndipo ambapo tunaanzia na kusema, ni nani huyo ambaye ameanzisha? Kwa sababu kila ambacho kimeanzishwa basi ni lazima kiwe na mwanzilishi wake, na hii i kanuni ya kiakili kabisa ambayo hatuwezi kupingana nayo, sasa ni nani ambaye ameanzisha uwepo wa ulimwengu?.

Bw Antony alikuwa anajua kwamba kuna ambao wanaamini kwamba asili ya kimaumbile au wanavyoita wenyewe "Nature”, ndio msingi wa upatikanaji wa ulimwengu, lakini kutokana na kwamba hakuna tafsiri ya kutosheleza katika jambo hilo ndipo ambapo akaamua kuipa akili nafasi yake na kufikia katika natija ya kwamba Mungu pekee ndiye ambaye anahusika na jambo hilo. Kama anavyosema ".....Ikawa hakuna kimbilio zaidi ya kuamini kwamba kuna nguvu ya ulimwengu usio wa kimaada, na mimi nikashikamana na msingi usemao kwamba shikamana na dalili popote itakapokupeleka, basi nami ikanipeleka katika imani hii....”

There is a God.