Umuhimu wa salamu katika Uislamu - 2

Salaam (salamu) ni moja ya majina ya Mwenyezi Mungu

Tukirejea katika Qur’ani Tukufu tunaona kwamba, salamu imetajwa kuwa moja ya majina yake Mwenyezi Mungu. Allah anasema:

هُوَ اللَّهُ الَّذِي لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ

Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha nayo. (Hashr - 23)

Kwa ajili hiyo kila mwanzo wa salamu, usafi na uzima ni vyake yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu Muumba wa kila kitu ambaye ni mpole, huwasalimu waja wake kwa salamu ambazo zimejaa baraka na amani. Ayatullah Jawadi Amoli mmoja wa maulamaa wakubwa wa kidini, mwanafalsafa na mfasiri mkubwa wa Qur'ani Tukufu wa mjini Qum Iran anasema hivi kuhusiana na suala la salamu:

"Maamkizi bora ya Mwenyezi Mungu kwa Mitume na waja wake wema ni salamu. Wakati mwingine salamu hii hushuka moja kwa moja bila ya kuwepo mtu wa kati, kama vile salamu ya Mwenyezi Mungu kwa Nabii Nuhu na Ibrahim (as). Na wakati mwingine salamu hiyo hutoka kwa mmoja wa mawalii wa Mwenyezi Mungu, kama vile salamu ya Nabii Musa (as) kwenda kwa waja wake wema. Kadhalika salamu iliyotajwa katika sura ya Taha aya ya 47 isemayo:

وَالسَّلامُ عَلَى مَنِ اتَّبَعَ الْهُدَى

"…. Na amani itakuwa juu ya aliyefuata uwongofu.

Bila shaka salamu haihusu duniani peke yake, bali pia wakati wa kufarijika na rehema za Mwenyezi Mungu katika Siku ya Kiyama pia kutatolewa salamu ambayo ndiyo zawadi na maamkizi maalumu kwa ajili ya waja wake wema. Malaika nao pia watawakaribisha watu wa peponi kwa salamu kwenye meza pana ya neema za Mwenyezi Mungu, kama wanavyowatolea salamu na maamkizi ya Mwenyezi Mungu wakati wa kutolewa roho zao.

Faida za kutoleana salamu

Kusalimiana au kutoleana salamu kama tulivyoeleza awali kuna faida nyingi lakini miongoni mwa faida za kimsingi kabisa mbali na kuleta hali ya huba na mapenzi ni kughufiriwa na kusamehewa madhambi. Mtume Muhammad saw amesema:

إنَّ مِن مُوجِباتِ المَغفِرَةِ بَذلَ السلامِ و حُسنَ الكلامِ

Miongoni mwa mambo yanayopelekea maghfira ni kusalimia na kusema maneno mazuri (kuzungumza kwa wema).

Faida nyingine ni mtu kuondolewa katika kundi la mabakhili. Kwani mtu asiyesalimia ndiye anayehesabiwa kuwa bakhili zaidi miongoni mwa watu katika jamii.

Mtume saw amenukuliwa katika hadithi mashuhuri akisema kwamba:

إنَّ أبخَلَ الناسِ مَن بَخِلَ بِالسلامِ

Hakika bakhili zaidi miongoni mwa watu ni yule anayefanya ubakhili wa salamu (asiyesalimia).

Sambamba na salamu kuleta mapenzi na ukunjufu wa nyoyo kati ya watu, pia huleta hali ya unyenyekevu na kuepukana na jeuri. Hivyo basi faida nyingine ya salamu ni mtu kuwa mnyenyekevu na kuepukana na kiburi na ujeuri au hata hali ya kujiona na kujikweza. Watu wanyenyekevu si tu kwamba huwa hawapati hasara na madhara, bali pia hupata izza na mapenzi kutoka kwa wenzao. Kuhusiana na suala hilo, Imam Ja’afar Swadiq (as) anasema: "Miongoni mwa alama za unyeyekevu ni kumsalimia kila mtu unayekutana naye." Aidha imamu huyo anasema:

"Enezeni salamu kati yenu mtapendana."

Mtume (saw) daima aliwatangulia watu kutoa salamu

Na  Salum Bendera