Umuhimu wa salamu katika Uislamu-3

Salamu ni aina ya maamkizi ya Kiislamu na asili ya neno "Tahiyyat” yaani Maamkizi" linatokana na neno "Hayy” yaani hai" ikimaanisha kumtakia uhai na maisha yule anayesalimiwa. Qur'ani Tukufu inasema hivi katika aya ya 61 ya sura ya an-Nur: 

"….Na mnapoingia katika majumba basi mtoleane salamu, ni maamkio yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu yenye baraka njema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni Aya ili mpate kufahamu."
Aya hii inataja salamu kuwa, maamkizi ya Mwenyezi Mungu ambayo mbali na kuwa ni maamkizi, lakini pia ni yenye baraka nzuri. Aidha kwa mujibu wa aya hii itafahamika hapa kuwa maana halisi ya neno, "Salamu Alaykum” yaani amani iwe juu yenu" inatokana na asili ya neno "Salamullahi Alaykum" ikimaanisha, "amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu, Mwenyezi Mungu anakutoleeni salamu na dumuni katika amani." Kwa ajili hiyo kusalimiana ni moja ya njia za kutangaza urafiki na udugu. Amri hii ya Kiislamu imejengeka juu ya msingi mkuu wa kuimarisha uhusiano wa kijamii kati ya watu wote.

Aina za Salamu

Kila jamii ina desturi na misingi yake maalumu ya kusalimiana, ambapo katika baadhi ya jamii watu husalimiana kwa kuinama mbele ya wenzao, wengine husalimiana kwa kutikisa vichwa, kuinua mikono na wengine husalimiana kwa kuvua kofia vichwani kwao. Amma katika Uislamu mbali na kusalimiana pia kuna kupeana mikono. Mtukufu Mtume (SAW) anasema: "Wakati wowote mnapokutana, salimianeni kwa kupeana mikono." Aidha mtukufu Mtume alikuwa akisalimiana huku akitabasamu na alipokuwa akipeana mkono na mtu yeyote alikuwa akichukua kitambo kuuachilia, hadi mtu wa upande wa pili ndiye aanze kulegeza na kuurudisha nyuma mkono wake. Hakuna shaka kwamba, mtukufu huyo alikuwa akifanya kitendo hicho katika hali ya kudhihirisha mapenzi yake ya moyoni kwa mtu yule. Hii ni kwa sababu uhusiano wa thamani uliofichika ndani ya nafsi lazima ufichuliwe ili uweze kupata baraka. Thamani hiyo huweza kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili. Ni kwa ajili hiyo, ndio maana Waislamu wanapokutana wanatakiwa kudhihirisha tabasamu, uso mkunjufu na bashasha kati yao.


Kasoro za baadhi ya watu katika salamu
Licha ya kuwa salamu ni moja ya vyanzo vya kuimarisha mahusiano ya kijamii, lakini hutokea baadhi ya upungufu na uzembe kuhusu jambo hilo, kama vile baadhi ya watu kusubiri salamu na heshima kutoka kwa mtu mwengine, kuchelewa kusalimiana, kutotoa majibu kwa salamu na kadhalika, mambo ambayo yanaweza kuharibu na kuzusha vinyongo na uadui kati ya watu. Kwa ajili hiyo dini tukufu ya Kiislamu imewausia sana wafuasi wake daima watoe salamu na majibu kwa sauti za juu ili yapate kusikika na upande wa pili. Imam Swadiq (as) anasema: "Wakati wowote mmoja wenu anapotoa salamu, basi dhihirisheni majibu yake." Aidha suala lingine muhimu ni hili kwamba, pamoja na kwamba salamu ni sunna, lakini kujibu salamu hiyo ni wajibu (lazima), hivyo jibu linapaswa kusikika na liwe ni lenye mapenzi ndani yake, kwa kuwa salamu ni maamkizi na zawadi kutoka kwa Mwislamu. Udhihirishaji huo wa mahaba unatokana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu inayotuamrisha kufanya hivyo kwa kusema, "Na mnaposalimiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au mrejeshe hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhesabu kila jambo."