Utumiaji mabavu dhidi ya wanawake wanaovaa hijabu; silaha ya Wamagharibi ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia)
Na Salum Bendera
Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika nchi za Magharibi zikiwemo Ujerumani na Uhispania zimeongezeka mno katika miaka ya hivi karibuni, hususan wimbi la vitendo vya utumiaji mabavu na kuvunjiwa heshima wanawake wanaovaa vazi na hijabu. Takwimu rasmi zilizotolewa nchini Ujerumani na Uhispania zinaonyesha juu ya kukithiri hujuma dhidi ya Waislamu katika nchi mbili hizo za bara Ulaya. Makundi yenye misimamo mikali na chuki dhidi ya Waislamu yanatajwa kuwa ndiyo yanayoendesha kampeni hiyo chafu dhidi ya Waislamu. Takwimu rasmi za serikali ya Ujerumani zinaonyesha kwamba, katika mwaka uliopita wa 2017 pekee, jumla ya matukio 950 ya mashambulio na hujuma dhidi ya Waislamu na Misikiti yaliripotiwa kutokea katika nchi hiyo. Aidha nchini Uhispania, nchi nyingine ya bara Ulaya, mwaka uliopita wa 2017, ulishuhudia vitendo 500 vya matukio ya chuki dhidi ya Uislamu yakitokea nchini humo. Baadhi ya matukio hayo ni kushambuliwa na kuvunjiwa heshima wanawake waliokuwa wamevaa hijabu na vijana waliokuwa wakielekea au kutoka msikitini. Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, katika mwezi wa Januari mwaka huu kulianza kuchukuliwa hatua za kufuatilia mashtaka ya Waislamu kutendewa vitendo visivyostahiki ambapo chimbuko lake ni chuki za kidini.
Makundi yenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani, Uhispania na barani Ulaya kwa ujumla yamekuwa yakiwashambulia mara kwa mara wanawake wanaovaa vazi la hijabu au kuchoma moto misikiti na hata kuandika maandishi ya kibaguzi katika kuta za misikiti.
Baada ya shambulio la kigaidi lililotokea Septemba 11, 2011 huko nchini Marekani, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) viliongezeka sana barani Ulaya na katika ulimwengu wa Magharibi kwa ujumla. Kuvunjiwa heshima Qur’ani, Mtume SAWW na matukufu mengine ya Kiislamu kama Kaaba na kadhalika, yaliwekwa katika ajenda za chuki dhidi ya Uislamu za tawala na vyombo vya habari vya Magharibi. Wahusika wakiwa na lengo la kuhalalisha matukio hayo ya kuutusi na kuuvunjia heshima Uislamu walifanya hima ya kuuonyesha kwamba, Uislamu ni dini ya misimamo mikali na ambayo inaeneza vitendo vya utumiaji mabavu na mauaji hususan dhidi ya wanawake. Tawala za magharibi zikishirikiana na vyombo vyao vya habari zilifanya kila hali kuonyesha matendo yanayofanywa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda, Taliban, Daesh, Boko Haram, al-Shabab na mengineyo ambayo yanadai kuwa yanatetea Uislamu kuwa, mfano wa wazi wa utumiaji mabavu na mauaji yanayofanywa na Uislamu.
Hii ni katika hali ambayo, makundi hayo yamepotea na kukengeuka njia sahihi ya Uislamu na kimsingi hayawakilishi fikra sahihi ya Uislamu na mafundisho yake sahihi. Uislamu ni dini ya amani na upendo na inayopinga kuuawa watu wasio na hatia yoyote, kuporwa mali zao au kudhulumiwa mtu. Kwa hakika Uislamu unajibari (unajitenga) na makundi hayo na katu hautetei wala kuunga mkono vitendo vinavyofanywa na makundi hayo ya kigaidi. 
Weledi wengi wa mambo wanaamini kwamba, lengo hasa la madola ya Magharibi kutumia nguvu zao zote kupambana na Uislamu ni hofu kubwa walionayo kutokana na dini hiyo kuzidi kupata wafuasi katika nchi zao. Hujuma hizo hazijasaidia chochote kwani watu wanaosilimu na kuingia katika Uislamu katika ulimwengu wa Magharibi wamekuwa wakiongezeka kila leo. Hii ni kutokana na kuwa, mafundisho ya Uislamu yamejengeka juu ya akili, mantiki, fitra (maumbile) na hali ya kati na kati.
Matamshi yanayotolewa na raia wa Ulaya wanaosilimu yanaonyesha kwamba, Uislamu ndio kimbilio lao pekee kutokana na dini hii kukidhi mahitaji yao na kukata kiu yao ya kupata kitu ambacho kitakuwa na mwongozo wa kweli katika maisha yao ya kila siku.