UISLAMU NA TABIA

TABIA MBAYA

Tabia mbaya inakuwa ni: Hali ambayo inayoiamrisha nafsi kuelekea kwenye mambo ambayo yako kinyume na maadili mema, pia ina sababisha mwanadamu kuwa kinyume na maumbile ya ubinadamu, na miongoni mwa mambo yaliyokuwa wazi ni kwamba tabia hiyo ina athari mbaya katika maisha ya mwanadamu huyo, na ina sababisha kuchukiwa na kutengwa na watu, na kwamba hatima yake huwa ni mbaya.

Mtume mtukufu (s.a.w.w) anatueleza mwisho ya tabia mbaya ni wapi, na hatima ya tabia njema ni wapi kwa kusema:

"عليکم بحسن الخلق، فإنّ حسن الخلق فی الجنة لا محالة، وإياکم وسوءالخلق، فإنّ سوءالخلق فی النّار لا محالة"

"Jihimizeni kwa tabia njema na jipambeni nayo, kwani tabia njema mafikio yake ni peponi haina pingamizi, na jiepusheni na tabia mbaya kwani tabia mbaya mafikio yake ni motoni haina pingamizi”.

Pia Imam Jafar Sadiq (a.s) anatueleza umuhimu wa kuwa na tabia njema, na kujiepusha na tabia mbaya:

"إنّ شئت أن تکرم فلن، وإن شئت أن تهان فاخشن"

"Ikiwa unapenda kukirimiwa basi kuwa mpole, na ikiwa unapenda kudhalilishwa basi kuwa mkaidi”.

MAMBO YANAYO IBDILISHA TABIA YA MWANADAMU

Kama vile mwili unavyopata ugonjwa wa aina yoyote na kupeleka kudhoofika kwa afya yake, basi ndivyo ambavyo na tabia inavyopatwa na ugonjwa pia hudhoofika. Na laiti kama ingekuwa hakuna uwezekano wa kuitibu tabia hiyo na kuiweka katika mstari ulionyooka, basi mitume wa Mwenyezi Mungu wangefeli katika kuwarekebisha watu kitabia. Na kuwaelekeza katika yale yaliyo ya kheri. Na binadamu angetoka katika hali ya ubinadamu na kuwa katika hali ya uhayawani (Unyama).

Hivyo basi kuna mambo ambayo yanaipata tabia ya mwanadamu na kuibadilisha kuwa tabia mbaya, nayo ni moja katika mambo yafuatayo:

1. Kujiona dhalili na dhaifu katika jamii na ukosefu wa afya mwilini.

2. Huzuni nyingi: Pia inaondosha akili ya mwanadamu na inabadilisha tabia yake.

3. Ufakiri: Ni moja ya vitu vinavyosababisha kubadilisha tabia ya mwanadamu kwa machungu ya ukosefu wa neema. Au kuhuzunika sana kwa kuondokewa na neema iliyopita. Au kupoteza utajiri aliokuwa nao.

4. Utajiri: mara nyingi kitu kinacho mfanya mwanadamu kuwa na kiburi na kujiona ni kwa sababu ya uwezo aliokuwa nao.

5. Cheo: kina sababisha kuwa na utovu wa adabu.

6. Kujitenga na kujiona kuwa mimi ndio mimi au kutengwa na watu ni tatizo kubwa linalompelekea mtu kuwa na mabadiliko ya kimaadili.

TIBA YAKE

Kulingana na utovu wa adabu kuwa ni sifa mbaya, mwanadamu anayependa kujirekebisha na kurekebisha mwenendo wa tabia yake anapaswa kufuata nasaha hizi zifuatazo:

Kwanza: Akumbuke kuwa madhara ya tabia hiyo, inapelekea Mwenyezi Mungu kuchukia, pili: Kutengwa na watu na kumlaani.

Pia azingatie ubora wa tabia njema na athari zake nzuri, kulingana na hadithi za bwana mtume (s.a.w.w) na maimamu (a.s).