UVIVU

بسم الله الرحمن الرحیم

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu.

Imamu Baqir (a.s) amesema:

«الکسل یضر بالدین والدنیا».

"Uvivu unadhuru dini na Dunia”. (mizaanul hikma, kipengele cha uvivu).

Moja ya mada iliyotajwa katika hadithi na kusisitizwa zaidi ni ulazima wa kuwa na uchangamfu na kuepuka uvivu na kukosa hamu katika kazi. Ukosefu wa hamu na uchache wa subira humzuia mtu kufikia mafanikio. Kigezo hiki humfanya mwanadamu kutodumu katika kazi ambayo ni mwenye uwezo nayo, maandalizi nayo na kadhalika, na hatima yake kuziacha kazi zikiwa nusu na kutafuta tawi lingine la kazi.

Kwa kawaida, wavivu, wenye kuchoka na wasio na subira ni kwa sababu hawana uvumilivu wa kufanya kazi na ilihali wakati huo wanataka kupata matokeo mengi ya mapema, kamwe hakuna chochote kizuri watakachokifanya ikiwa kazi zenyewe huishia njiani, wameghafilika na nukta hii kwamba ikiwa watavumilia kazi zao hata kiasi kidogo, na kujiepusha na uvivu hakika watakipata kile wakikusudiacho.

Imepokelewa Dua hii kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ikisema: "Mola wangu hakika mimi ninajilinda kwako uniepushe na uvivu”.

AINA ZA UVIVU:

Uvivu wa ibada: Ni katika aina mbaya za uvivu katika suala zima la kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, kwani amesema katika kitabu chake:

«وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيعْبُدُونِ».

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi”.

Uvivu wa kutafuta elimu: Ni mojawapo ya kuiteketeza jamii kusoka vijana ambao watakuwa ni rasilimali ya jamii kwa ajili ya kuikomboa jamii husika.

Uvivu katika suala la kimaadili: Ni pale ambapo mtu amekwisha kata tamaa ya kubadilisha mwenendo wake mbaya.

Uvivu wa masuala ya kijamii: Ni mtu kuzembea na kupuuzia nyadhifa za kijamii kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wanajamii kwa ujumla.

Uvivu wa kiuchumi: Ni pale ambapo vijana wanapotafuta kazi nyepesi na zenye mafanikio ya haraka bila usumbufu.

SABABU/ VYANZO VYA UVIVU:

1. Kukosa usingizi wa kutosha na hitajika wakati wa usiku.

2. Kukosa muda wa mazoezi na michezo.

3. Wasiwasi na huzuni za hapa na pale.

4. Kukosa muda kwa ajili ya chakula kamili cha asubuhi.

Amesema Imamu Baqir (a.s):

«إیّاکَ و الکَسَلَ و الضَّجَرَ فإنّهُمَا مِفتَاحُ کلِّ شَرٍّ، مَن کَسِلَ لَم یُؤَدِ حقّاً».

"Jiepushe mbali na uvivu na hasira kwani (viwili hivyo) ni ufunguo wa kila shari, yeyote awaye mvivu hazitekelezi haki za kijamii ipasavyo”. (Rejea: Tuhaf al- U’quul, uk 656).