Matendo ya Mwezi wa Rajab


قال رسول الله صل الله علیه و اله و سلم:
ألاَ إنّ رجب شهر الله الأصمّ، وهو شهر عظيم؛ وإنّما سُمّي الأصمَّ لأنّه لا يقارنه شهر من الشهور حرمةً وفضلاً عند الله تبارك وتعالى. وكان أهلُ الجاهليّة يعظّمونه في جاهليّتها، فلمّا جاء الإسلام لم يَزدَد إلاّ تعظيماً وفضلاً

Amesema mtukufu Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yak epamoja na kizazi chake kitoharifu:

"....Kwa hakika mwezi wa Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu wenye sifa ya (Al Asammu) (Tutaeleza maana ya jina hili), nao ni mwezi mtukufu, na umepewa jina la Al Asammu kutokana na kwamba hakuna mwezi wowote wenye kuufikia kwa utukufu na fadhila mbele ya Mwenyezi Mungu (swt). Majahili katika zama zao walikuwa wakiutukuza mwezi huu, na ulipokuja Uislamu haukufanya zaidi ya kuuongezea utukufu....”

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Ally (as) kwamba amesema:

رجب شهر عظيم يضاعف الله فيه الحسنات ويمحوَالسيئات

"….Rajab ni mwezi mtukufu, kwani ndani yake Mwenyezi Mungu huongezea mema maradufu na hufuta maovu….”

Kutokana na madhumuni ya riwaya hizo mbili ambazo ni baadhi tu ya riwaya nyingi mno ambazo zimekuja katika kuelezea fadhila zinazopatikana ndani ya mwezi wa Rajab, tuna kila haja kama Waislamu kukumbushana na kuambiana kheri gani hizo ambzo zinapatikan andani ya mwezi huu kiasi kwamba kuna lundo la hadithi ambazo zimekuja kuelezea utukufu wake.

Ni jambo lililo wazi kwa waja wote, kwamba hakuna heri yeyote ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka kwetu kisha ikawa ni heri tu bila ya sisi ama sisi kusimama kwa namna moja au nyingine.

Hivyo basi pamoja na kwamba kuna fadhila nyingi sana katika mwezi huu, haina maana kwamba fadhila hizo zitaambatana na kila mmoja hata kwa yule ambaye atakaa bila ya kujishughulisha na lolote.

Na haya sio kwamba ni maneno ambayo nayasema bila ya kuwa na mashiko katika hayo, bali ni maneno ambayo tunayatoa katika mafundisho sahihi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad (saww), hebu angalia riwaya hii inavyosema.

Amesema Mtume Muhammad (saww):

إن الله تعالى نصب في السماء السابعة ملَكاً يقال له الداعي، فإذا دخل شهر رجب نادى ذلك الملك كل ليلة منه الى الصباح يقول: "طوبى للذاكرين، طوبى للطائعين"، (يعني هنيئاً) ويقول الله تعالى:"أنا جليس من جالسني ومطيع من أطاعني وغافر من استغفرني. الشهر شهري والعبد عبدي..والرحمة رحمتي، فمن دعاني في هذا الشهر، أجبته وجعلت هذا الشهر حبلاً بيني وبين عبادي، فمن إعتصم به وصل إلي

"….Hakika Mwenyezi Mungu ana malaika wake katika mbingu ya saba kwa jina la "Mlinganiaji”, pindi tu unapoingia mwezi wa Rajab hunadi kuanzia usiku mpaka asubuhi na kusema "…Heri wenye kumtaja Mwenyezi Mungu, Heri yao wenye kumtii Mwenyezi Mungu”. Na pia Mwenyezi Mungu mwenyewe husema "…..Mimi huwa karibu na mwenye kuwa karibu nami, humsikia mwenye kunitii, husamehe mwenye kuniomba msamaha, mwezi huu ni mwezi wangu na mja ni mja wangu kama ambavyo rehema ni rehema zangu, hivyo mwenye kuniomba katika mwezi huu humjibu, na mwezi huu nimeufanya kuwa ni kamba baina yangu na waja wangu, hivyo mwenye kushikamana nayo atanifikia….”

Tunachopata katika riwaya hii ni kwamba pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu ametangaza ofa kibao kwa waja wake, bado kuna jambo la muhimu nalo ni kwamba mja anatakiwa naye ajishughulishe kuhakikisha kwamba anakaribia hizo ofa.

Hivyo basi swala la kuoga rehema za mwezi mtukufu wa Rajab ni lazima pia mja awe na maandalizi ya kuweza kufanikiwa katika hilo. Na kwa minajili hiyo basi katika sehemu hii ya leo tuaweza kukumbushana baadhi ya mambo muhimu ambayo yanatakiwa kufanywa katika mwezi huu wa Rajab ili tu tuweze kuzivuna hizo ofa za Mwenyezi Mungu katika mwezi huu wa Rajab.