Surat Ikhlas na siri ya Kumpwekesha Mungu -1

Hakuna shaka kwamba Quran ni kitabu ambacho kimekuja kukusanya nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu, na ndio maana tunaweza kusema kwamba kitabu hiki ni kitabu chenye kukusanya kila jambo ambalo mwanadamu analihitajia kwa anuani ya mwongozo wa maisha yake ya hapa duniani na hata baadaye akhera.

Lakini ili kuweza kufaidika na mwongozo uliopo ndani ya kitabu hiki inahitajia kwanza moyo uliokunjuka, kwa maana moyo ambao upo tayari kupokea hayo yanayoashiriwa na Quran, kwani kama mtu atakuwa hayupo tayari kuongoka hata kama atajaziwa kila lililomo katika Quran hatoweza kuongoka.

Pili inahitajika watu ambao wao ndio watakaohusika na kuelekeza yale mambo ambayo huenda wanadamu wakasema wameelewa, lakini kumbe ikiwa wameelewa kwa maana tofauti, au hata kama watakuwa wamepatia basi watakuwa wamepatia kwa asilimia chache sana ukilinganisha na zile ambazo Mwenyezi Mungu anataka tuzielewe na kuzitumia.

Hapo ndipo unakuta kwamba Mwenyezi Mungu akatupatia Mtume Muhammad (saww) kwa anuani ya mwalimu wa hii silabasi ya Quran, mwalimu ambaye pia baada ya uhai wake wa duniani kumalizika akatuachia kizazi chake kama warithi wa kazi yake ya kufasiri na kuelekeza yale ambayo yamo katika Quran tukufu.

Hivyo kwa minajili hii basi, ni kwamba ili kuweza kunufaika na Quran kwa maana ya kunufaika, kuna haja yetu sisi kama sisi kuchukua maana za Quran kutoka kwa walimu wake, na ili kuweza kubainisha hili tumeamua kuja na makala ambazo zitakuwa zinalenga kuonyesha ni namna gani Quran ina maarifa mengi mno ambayo yamefundishwa na hao walimu, maarifa ambayo laiti kama wasingalikuwa wao basi sidhani kama kuna mtu angeweza kuyafikia.

Na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutakuwa tunachukua baadhi ya sura tukufu kutoka katika Quran, kisha kuashiria mambo ya muhimu au elimu zinazopatikana katika sura hizo.

1. Surat Al Ikhlas

Kama ambavyo anuani inasema, ni kwamba tunataka kuielezea Sura hii maarufu ili tu kuweza kuona kile ambacho walimu wa Quran (Watu wa nyumba ya Mtume) wamekibainisha.

Ni Sura maarufu, yenye fadhila nyingi sana kwa mwenye kuisoma, inatosha tu kuelewa kwamba Sura hii inachukua nafasi ya Theluthi ya Quran kutokana na daraja na cheo chake kama ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) aliposema:

"أيعجز أحدكم أن يقرأ ثلث القرآن في ليلة"؟ قيل: يا رسول اللّه ومن يطيق ذلك؟

قال: "اقرأوا قل هو اللّه أحد"

"......Je inakuwa ngumu kwenu kusoma Theluthi ya Quran katika usiku mmoja?, Wakamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni nani mwenye kuweza hivyo?, Mtume akasema "Someni Surat Ikhlas (Qul Huwa Llahu Ahad)...”

Au kama ilivyopokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) aliposema:

من مضى به يوم واحد فصلى فيه الخمس صلوات ولم يقرأ فيها بقل هو اللّه أحد، قيل له: يا عبد اللّه لست من المصلين

"....Mwenye kupitwa siku moja ambayo ameswali swala zake tano bila ya kusoma Suratul Ikhlas, huambiwa "..Ewe Mja wa Mwenyezi Mungu, hujaswali kitu”.

Haina maana kwamba mwenye kuswali bila ya kusoma Sura hii basi swala yake inakuwa ni batili, la hasha, bali Imamu alitaka kubainisha tofauti iliyopo baina ya mwenye kuswali na kusoma Sura hii na yule mwenye kuswali bila ya kusoma Sura hii kwa upande wa fadhila na daraja na malipo kwa ujumla.

Kwa hiyo ni Sura ambayo ina fadhila kubwa sana, lakini tukiachana na upande huo wa fadhila zake, ambao sitaki kuuzungumzia sana katika sehemu hii, kuna upande mwingine ambao mimi napenda kuuita upande wa kimaarifa zaidi, nikiwa na maana upande wa elimu na yale ambayo tunaweza kuyapata katika sura hii kwa mujibu wa mafundisho ya walimu wa Quran.

Sura hii imezoeleka kwa jina lingine maarufu la Surat Tawhid, kwamba ni sura yenye kuzungumzia maswala ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu (swt), lakini je Kumpwekesha huko kumewekwa katika misingi gani na mana gani?, hili ndilo ambalo ningependa walimu wetu waweze kutubainishia katika Sura hii ili nasi tuweze kunufaika.

Hebu tusome kwa pamoja Sura hii na kuona walimu wetu ni mambo gani ambayo wameyanyambua kutoka ndani yake.

﴿قُلْ هُوَ اللّهُ أَحَدٌ * اللَّهُ الصَّمَدٌ * لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ * وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُواً أَحَدٌ﴾

Sura imeanza kwa kusema:

قُلْ هُوَ اللّهُ أَحَدٌ

".....Sema kwamba yeye ni Mungu mmoja”

Ni jibu ambalo linakwenda moja kwa moja kwa wale wote wenye kuwa na maswali tofauti juu ya huyu Mwenyezi Mungu, kwani tunaambiwa makafiri wa zama za Mtume walikuwa wakimuuliza sana Mtume kunako huyo Mungu anayemlingania, mbona si kama miungu yao waliyoizoea?, mbona si mwenye kuonekana kama ambavyo yao inaonekana?.

Imamu Muhammad Al Baqir katika kuelezea aya hiyo hasa neno " قُلْ "Sema” ambalo lilikuwa likimwelekea Bwana Mtume (saww) anasema:

".....Makafiri walikuwa wamezoea kuashiria Miungu yao kwa viashiria vya karibu na kusema hii ndiyo Miungu yetu, tunaweza kuihisi na kuiona kwa macho, basi nawe Muhammad tuashirie huyo Mungu wako unayetulingania kwake ili tuweze kumuona kwa macho na kumuhisi, ndipo Mwenyezi Mungu aliposhusha aya hii na kumwambia Mtume wake kwamba "Sema kwamba yeye ni Mungu mmoja”.