Surat Ikhlas na siri ya Kumpwekesha Mungu -3

Hizi ni maana nne ambazo zote ukitaka kuziashiria unatumia neno "Mmojaā€¯, lakini tunapokuja kwa Mwenyezi Mungu ni lazima tuelewe ni Mmoja gani ambayo tunaikusudia?, isije kuwa tunakusudia kumpwekesha kumbe wakati huohuo tunaangukia katika kumshirikisha.

Tuanze na maana ya nne, ambapo unaelezea umoja wa kitu ambacho kinashirikiana na vingine katika sifa fulani, lakini unakitenga na kusema kwamba hicho ni kimoja. Maana hii haiwezekani ikaambatana na Mwenyezi Mungu hata mara moja, kwa maana kitendo cha vitu kufanana sifa katika kila nyanja, kisha ukaja kusema kwamba hiki kipo peke yake ni kutenga kitu bila ya kuwa na dalili, jambo ambalo kiakili si sahihi.

Tuje katika maana ya tatu, ambayo ni kusema jambo fulani ni moja kwa maana ya umoja wa kiidadi. Hapa itabidi ukumbuke kwamba kila chemye moja kiidadi kina mbili na tatu na kuendelea kiidadi kadhalika, hivyo unaposema Mungu ni mmoja na ukawa na maana ya kwamba yaani sio wawili bado utakuwa katika mushkeli wa Tawhid. Ndiyo, kwa sababu wewe utakuwa katika fikra zako kuna Miungu zaidi ya mmoja, lakini ukaamua kuambatana na mmoja na kumpa sifa ya umoja, yaani yule wa pili na wa tatu hawana haki ya kuwa Mungu. Hivyo maana hii pia haiwezi kuwa sahihi kwa Mwenyezi Mungu.

Tuje katika maana ya pili ambapo unakusudia Umoja wa kitu bila ya kuwa na Mwenza. Naam, hii ni maana sahihi kabisa kwa Mwenyezi Mungu, bali hata katika Sura hii pia tutakuja kuona kwamba imeashiriwa pale aliposema kwamba hakuna yeyote mfano wake.

Kama ambavyo pia tukija katika maana ya kwanza ambayo imesimamia katika Umoja wa yule ambaye hakuna jambo lolote lenye kuhusika na kumfanya awe, tunaona wazi kabisa namna ambavyo inaendana na Mwenyezi Mungu, ambaye si mwenye kuumbika kutokana na vipengele kadhaa ili useme kwamba kuna vipengele vyenye kumuunda yeye.

Hapa ndipo tunatambua kwanini Sura hii imekuwa maarufu kwa swala la Tawhid.

Hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo yanapatikana katika aya ya kwanza ya Surat Ikhlas au Tawhid.