Uhakika wa Imani

Wasomaji wapenzi ni matumaini yangu kuwa mnafahamu vyema kuwa neno 'imani' lina maana ya kukubali na kuwa na yakini juu ya kitu au jambo fulani. Imani ni hali fulani ya nguvu inayotokana na hisia ambayo humpelekea mtu kujiamini. Imani ambayo hutoa mwelekeo maalumu kwa maisha ya mwanadamu na kuyaathiri kwa kiwango kikubwa. Mtu anayekuwa na imani ya aina hiyo moyoni mwake ndiye huitwa muumini. Katika makala yetu ya leo, sambamba na kulifafanua neno imani, tunakusudia pia kutaja baadhi ya sifa za muumini kwa mujibu wa nadharia ya kidini, ili kwa njia hiyo tuweze kufahamu iwapo nasi tupo katika kundi la watu wa aina hiyo au la?

Kwa mujibu wa nadharia ya kidini, neno 'imani' ni mwelekeo wa kimoyo wenye mafungamano ya kifikra, kiitikadi na kiroho juu ya Mwenyezi Mungu Muumba wa dunia, kuamini wokovu kwa watu watendao mema, kuwepo maisha ya milele baada ya kuondoka duniani (yaani kuamini Kiyama), kuamini vitabu vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu na hali kadhalika kuwaamini Mitume ambao ni wajumbe wa Allah kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu. Hayo na mengineyo, ni miongoni mwa mambo yaliyo na ulazima wa kuyaamini na kisha kuyafanyia kazi. Kuhusiana na suala hilo Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema: "Imani ni kukiri kwa ulimi, kutambua na kukubali kwa moyo na kisha kwenda sambamba na utekelezaji wa viungo." katika Qur'ani Tukufu, imani imetajwa kwa maana mbili, "kukiri kwa moyo" na "utekelezaji kivitendo." tunaposoma Qur'ani Tukufu daima tunakutana na ibara inayosema: "Watakaoamini na wakafanya matendo mema," ikimaanisha kwamba, imani inafungamana na matendo mema. Ikiwa tutafahamu kuwa imani ni mfano wa mti, basi matendo yatakuwa ni matunda ya mti huo. Hivi inawezekanaje mtu kumuamini Mwenyezi Mungu, Kiyama, Pepo, Jahanamu, Wahyi, Mitume na vitabu vya mbinguni, lakini matendo yake yakafanana na watu wasiomwamini Mungu wala siku ya Kiyama? akafanya dhambi na matendo yanayopingana na dini? Imani lazima ianzie moyoni kuelekea kwenye viungo na kutoka ndani kwenda nje na kutoka katika kukubali kwa ndani kuelekea kwenye utendaji wa nje ya dhamira ya mwanadamu. Tunaweza kusema kuwa, imani ambayo haina athari yoyote moyoni na katika matendo, kwa hakika sio imani.

Ukweli wa mambo ni kwamba, imani ya baadhi ya watu ni ya juu juu tu ambayo hutokana na kufuata au kuiga kibubusa, na kufuata matamanio ya nafsi zao, huku ya wengine ikiwa inatokana na uelewa na mazingatio ya kina. Kwa hivyo, imani inayotokana na uelewa, utafiti na kuzingatia, ndiyo imani ya kweli na ambayo huwa imara. Imani ya kufuata kibubusa tu na isiyotegemea mantiki wala dalili yoyote ya msingi huweza kusambaratika kwa kukumbwa na mtingiziko wowote na huwa haina athari katika maisha ya mwanadamu. Lakini kwa upande wa pili, imani inayotokana na mtazamo wa kina na wa kweli, inashabihiana na mti wenye umri wa miaka mingi na wenye mizizi imara na ambao hauyumbishwi na upepo wala mafuriko. Imani ya aina hiyo ndiyo siku zote huambatana na vitendo. Kwa ajili hiyo, imani inayoambatana na matendo, huwa na natija njema na ikiwa mtu atafanya dhambi bila kuzingatia imani yake, basi hawezi kuingia peponi. na hapa tunapenda kuashiria kwamba sio kila imani ni sahihi, kiasi kwamba chochote utakacho kiamini, na matendo yako yakaambatana nacho, itakuwa sababu ya kuingia peponi, bali tunakusudia imani sahihi yenye dalili na kukubalika kiakili. Na hapa tutasema tena, sio sahihi kusema kwamba, imani humpeleka na kumuokoa moja kwa moja mwanadamu na kwamba, muumini anayefariki dunia hasailiwi. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat Zilzaal aya ya 7-8 kama ifuatavyo: "Basi anayefanya wema sawa na chembe atauona. Na anayefanya uovu sawa na chembe atauona." Hata hivyo kwa mujibu wa aya kadhaa za Qur'ani Tukufu, ikiwa muumini atafanya hata dhambi kubwa, basi Mwenyezi Mungu humpa muda ili aweze kutubu na anaposhindwa kutubu, basi Mwenyezi Mungu humwadhibu katika ulimwengu wa Barzakh (yaani kaburini) kwa kiwango kile kile cha dhambi ile aliyoifanya, na ikiwa ataendelea kuhifadhi imani yake basi hatimaye atapata kuokoka siku ya Kiyama. Je, inawezekana muumini kuaga dunia na kisha kukabiliwa na adhabu mbalimbali kutokana na dhambi nyingi alizotenda akiwa hai? Kumepokelewa riwaya nyingi kutoka kwa Maimamu watwaharifu (a.s) zinazoelezea kuwa, wakati muumini anapofariki dunia, na akawa hajatubia dhambi zake na kusamehewa, kuna uwezekano wa yeye kupata rehema na msamaha wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kulingana na hadhi na matendo yake mema aliyoyatenda duniani, katika moja ya hatua zake za kutolewa roho, au katika usiku wa kwanza wa kulazwa kaburini, au katika ulimwengu wa Barzakh na hatimaye siku ya Kiyama.

Baada ya hayo sasa ni wakati wa kutaja baadhi ya alama za imani na muumini kwa msingi wa aya za Qur’ani Tukufu. Kwa mujibu wa aya ya pili ya Suratul-Anfal inayosema: "Hakika wenye kuamini ni wale tu ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu, nyoyo zao hujaa khofu na wanaposomewa Aya zake huwazidishia imani, na wakamtegemea Mola wao tu,” Muumini ni yule ambaye wakati Mwenyezi Mungu anapotajwa au pale anapomkumbuka Mola wake basi haraka moyo wake hupatwa na khofu. Mtu anayemtambua Mwenyezi Mungu kuwa ndiye chanzo cha nguvu kubwa na rehema, wakati anapomkumbuka Mwenyezi Mungu basi hukumbwa na hali ya mabadiliko. Hii ni kusema kuwa, athari ya kwanza ya imani kwa muumini ni kwamba, mara tu anapomkubuka Mola wake, hupatwa ghafla na hali ya mabadiliko ya ndani. Alama ya pili ni kwamba, mtu huyo (muumini) huwa ni mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila jambo. Wakati imani ya mtu inapoongezeka na kumfanya kuzidi kumtambua Mwenyezi Mungu kuwa chimbuko na ufunguo wa kila jambo na kila kazi na kwamba yeye ndiye anayedhibiti kila kitu, basi wakati huo, hawamtegemei yeyote tofauti na Mwenyezi Mungu. Ikiwa mwanadamu atamtambua kwamba Mola wake ndiye anayedhibiti harakati zake zote na kwamba utulivu wa ulimwengu unatokana na idhini yake, basi atamtegemea yeye tu na kamwe hatatishwa na matatizo ya kidhahiri yanayomkumba duniani. Mtu muumini aliyepata izza ya nafsi yake kutokana na Mwenyezi Mungu pekee, hawezi kumtumainia mwingine yeyote yule asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Aidha mwishoni mwa aya ya pili ya Suratul-Anfal inasema "Na (Waumini) wakamtegemea Mola wao tu.” Dalili iliyo wazi ya kumjua mtu muumini ni kutumaini na kutarajia kwake kwa Mola wake pekee. Alama ya tatu ya kumjua muumini wa kweli ni kwa mujibu wa hadithi ya Imam Swadiq (a.s) inayosema: "Waumini ni wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu.” Katika kila kazi mtu muumini anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye msimamizi wa matendo yake yote huku akijawa na khofu moyoni mwake. Muumini huyo huchelea asije akachanganya matendo yake na dhambi na hivyo kujiweka mbali na rehema za Mola wake. Kwa kawaida hofu ya mwanadamu kwa Mola wake, hutokana na matendo yake mabaya, ambayo husababisha adhabu na kuporomoka kwake. Hata hivyo hofu ya waumini wa kweli, hutokana na ukubwa na utukufu wa Mwenyezi Mungu. Ni kwa ajili hiyo ndipo huwa waumini wa kweli, huku wakiwa wamejawa na hofu wakamuomba dua Mola wao kwa kusema: "Mola wetu! Usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema itokayo kwako, hakika wewe ndiye Mpaji mkuu.” (Surat Al-Imran). Yaani, Ewe Mola wetu! tuchunge ili imani yetu isije ikapotoka kutokana na kughafilika na matendo yetu mabaya. Suala ambalo kwa hakika ndiyo sababu kuu ya waumini kukariri maneno haya matakatifu yasemayo, "Tuongoze njia iliyonyoka,” Katika swala zao. Yaani Mola wetu! Kwa hakika sisi tunahitaji msaada na uongofu utokao kwako.

Na: Alhaj Sheikh Kadhim Abbas