Itikadi sahihi ndio msingi wa mafanikio


Bismillah Rahman Rahim

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote, kisha sala na salamu zote ziende kwa Mtukufu Mtume Muhammad (saww) pamoja na watu wa nyumba yake iliyo tukufu.

Bila shaka kila mwanadamu baada ya kukamilika uwepo wake hapa duniani, huwa kuna lengo ambalo Mwenyezi Mungu amemuwekea na inatakiwa afikie, kama ambavyo mwanadamu mwenyewe pia huwa anajua katika nafsi yake kwamba kuna lengo ambalo anatakiwa afikie. Tunaweza kutofautiana katika kuanisha lengo hilo kwa mfano, lakini tunaweza pia kuungana pamoja katika kujua kwamba lengo hilo si kufeli bali ni kufanikiwa, kwa maana vyovyote itakavyokuwa basi kila mmoja huwa anapanga kufanikiwa.

Hii inaashiria kwamba wanadamu wote huwa wana lengo la kufanikiwa katika maisha yao ima yawe ya sasa tu, au ya sasa na ya baadaye (kiyama), na hapa ndipo ambapo tunaanzia mazungumzo yetu na kusema kwamba hayo mafanikio ambayo tunayafikiria hayawezi kuja bila kuwa na mtazamo sahihi, lakini je ni upi huo mtazamo, au tunakusudia nini katika mtazamo?, tuwe pamoja.

1. Maajabu ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake

Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu amepambika nayo ni namna ambavyo amepangilia mambo yake katika hali ambayo mwanadamu wa kawaida hawezi hata kufikiria mbali na kutenda.

Angalia namna ambavyo ameumba wanadamu katika hali zao na namna ambavyo wanaingiliana katika mifumo ya maisha yao, kwamba kila mwanadamu huwa ni mwenye kumtegemea mwanadamu mwingine. Angalia namna ambavyo ameumba viumbe vingine ambavyo vipo kwa ajili ya kumtumikia mwanadamu, Wanyama, Ndege na wengineo, wote hawa wapo katika hali ya kumtumikia mwanadamu.

Lakini pia angalia namna ambavyo Mwenyezi Mungu ameweka aina ya uongofu kwa hawa wanyama na kuwafanya kwamba waelekee mahitaji yao ya muhimu bila hata ya kufundishwa wala kuambiwa kuhusu hilo, angalia mnyama ambavyo anapata mahitaji yake ya chakula, kuendeleza kizazi chake na mengineyo, yote ni maajabu matupu.

Pia kuna siri kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka kwa hawa wanyama, siri ambayo inaweza kuwa ni tofauti kubwa baina ya uongofu uliopo kwao na hali ambayo tutakuja kuiona ipo kwa mwanadamu, nikiwa na maana kwamba Mwenyezi Mungu ameweka uongofu kwa mnyama kwa kadri ya mahitajio yake, yaani mnyama anapokuwa anaongozwa na matamanio yake kwa ajili ya chakula, basi huwezi kuta anakula zaidi ya haja yake, na hapa ndipo utakuta kwamba baadhi ya wataalamu wanasema kuwa miongoni mwa siri ambazo zinafanya mnyama asiumwe kwa kula wala kunywa ni kwamba huwa anakula na kunywa kwa kadri ya mahitaji yake. (mazingatio).

Mwenyezi Mungu kuhusiana na uongofu ambao kauweka kwa wanyama anasema :

﴿قَالَ فَمَنْ رَبُّكُمَا يَا مُوسَى * قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَى كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَى﴾

"(Firauni) akasema: Ewe Musa Basi Mola wenu Mlezi ni nani?... Mussa akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoza....”[1]

Huu ndio uongofu ambao Mwenyezi Mungu kauweka kwa wanyama, japokuwa baadhi ya wataalamu pia wameupa jina la matamanio, ila lengo ni kutaka kubainisha kwamba wanyama huwa wanafikia malengo yao na haja zao kwa njia ambayo haihitajii mwalimu.

Baadhi ya mifano yenye kuashiria kwamba matamanio ya mnyama hayazidi mahitaji yake.

1. Siku moja bwana mmoja alialikwa katika baadhi ya hafla za chakula na vinywaji, kutokana na utamu wa vyakula vile yule bwana alijikuta amekula mpaka imemuwia vigumu hali yake. Wakati akipanda farasi wake na kujiandaa kuondoka, wenyeji wa hafla ile wakamwambia kwamba mbona bado hajala kama walivyotaka?, hivyo wakamuomba aweze kula kidogo kwa heshima na taadhima ya wenyeji.

Bwana yule akachukua tena chakula na kushuka chini na kuanza kula huku tumbo likiwa limejaa. Baada ya chakula kile bwana yule akapanda farasi wake kwa shida na kuanza safari. Wakiwa njiani akaamua ampitishe farasi wake sehemu kwa ajili ya kumywesha maji, walipofika sehemu ile yule farasi akanywa maji na kutosheka, lakini yule bwana akaona bado farasi mbona hajanywa kitu kutokana na umbali wa safari, hivyo akaamua kumsemesha na kumwambia "Kwa ajili ya heshima yangu naomba unywe tena maji”, lakini yule farasi bado hakurejea tena kunywa maji yale.

Yule bwana baada ya tukio lile akawa akijisemea moyoni na kusema "Kwa hiyo ni kwamba huyu farasi ana akili kuliko mimi!?”. Akiwa na maana kwamba yeye hakuweza kukataa nyongeza ya chakula hata baada ya kujaa kwa tumbo lake, jambo ambalo farasi ameweza kulifanya na kuchunga mipaka ya tumbo lake.

2. Paka na dawa ya ugonjwa wake

Imenukuliwa katika vitabu kwamba kuna jamaa mmoja alikuwa akifuga paka, kwa muda kadhaa akawa anamuona paka yule kwa hayupo sawa kiafya, kwa maana ya kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa fulani.

Siku moja yule jamaa akamuona paka wake akiondoka na kuelekea kando ya mto, hivyo akaona ni jambo jema kama atamfuatilia na kujua hatma yake, basi akamfuatilia mpaka paka yule alipofika na kusogelea baadhi ya majani yaliyo pembezoni mwa mto ule na kuanza kuyatafuna, jambo ambalo baada ya muda lilimpa nafuu na kupona.

Baada ya pale yule jamaa akawa akimuona paka wake yupo na hali kama ile alikuwa akienda na kuchuma majani yale na kumletea kama dawa.

Hawa ndio wanyama ambao Mwenyezi Mungu kawaumba kwa matamanio au uongofu wa namna kama hii, lakini mbali yote haya bado Mwenyezi Mungu kawaweka wanyama hawa chini ya himaya ya mwanadamu, ni ipi siri katika hilo?.

Itaendelea........[1] Surat Twaha aya 49-50