Itikadi sahihi ndio msingi wa mafanikio - 2

Mwanadamu amekirimiwa kwa akili na matakwa

Mwanadamu ni kiumbe kingine ambacho Mwenyezi Mungu pia amekipa nguvu za kutamani na kuelekea mwelekeo ambao haja zake zinaweza kutimia, kwa maana ya kwamba anaposikia njaa basi anajikuta anahangaika kusaka chakula, kama ambavyo pia anahangaika kuhakikisha kwamba anatimiza haja zake za kijinsia na kuamua kushiriki tendo la ndoa na kujenga familia na vizazi. Lakini tofauti kubwa iliyopo baina ya haya yaliyowekwa kwa mwanadamu na yale ambayo tumeyaona kwa wanyama ni kwamba kiwango cha kutimiza haja zake hakijawekewa kiwango maalumu au mipaka kama ambavyo ipo hivyo kwa wanyama. Kwa maana ya kwamba mwanadamu ana uwezo wa kuendelea kula na kunywa hata kama tumbo lake limeshajaa. lakini pembeni mwa hayo yote mwanadamu huyu pia amepewa nguvu ya akili yenye kupambanua kwamba hapa nimefikia mwisho wa haja yangu hivyo inatakiwa niache kuongezaHii ni neema kubwa mno ambayo mwanadamu amepewa na Mola wake, neema ambayo kwayo anaweza kujua kwamba ni wakati gani sahihi kwake kutimiza haja zake na kwa kiwango gani, bila kusahau kwamba kutokana na neema hii ya kuwa na akili, uwezo wa kuchagua na kufikiri na kutaka au kutotaka, Mwenyezi Mungu amemuweka mwanadamu katika uwanja wa hukumu zitakazotokana na namna ambavyo ametumia neema hiyo. Kwa maana nyingine huyu mwanadamu sasa anakuwa ni "Mukallaf” ana hesabiwa na mola wake. "mazingatio”.

1. Namna ambavyo uwezo wa kufikiri unakuwa kwa mwanadamu

Ni jambo lililo wazi kwamba mwanadamu hubadilika uwezo wake w kufikiri kadri ambavyo anabadilika kimaumbile, mtoto mdogo katika umri wake wa kwanza kabisa anakuwa anaongozwa na matamanio bila ya akili kwa kiasi ambacho anashindwa kubainisha baina ya baba au mama yake na mwanaume au mwanamke mwingine yule, lakini baada ya muda kupita mtoto huyuhuyu anapanda daraja na kuanza kuingiwa na akili pembuzi kiasi kwamba anaanza kupambanua baina yao.

Hii ni hatua ya kwanza kwa binadamu katika harakati za kukua kwa uwezo wake wa kupambanua na kutofautisha mambo, nacho ndio kipindi ambacho wataalamu wanakiita ni kipindi cha mtoto kuhama kutoka katika ngazi ya hisia na kuhamia katika ngazi ya kupambanua mambo.

Baada ya ngazi hiyo sasa tunakuta mwanadamu huyu anapanda ngazi na kufikia katika ngazi ya kumiliki mafuhumu mbalimbali za vitu, kwa maana hata kama kitu fulani hakitakuwepo mbele ya macho yake bado atakuwa na uwezo wa kujua kitu kile kwamba kipo na kina athari fulani. Mfano mzuri ni pale ambapo mtu anajua kwamba uliopo mbele yake ni moto na una unguza, na ikitokea kwamba moto ule haupo mbele yake siku moja, kiasi cha kuweza kuukumbuka tu basi anajua moja kwa moja kwamba huu hapa katika mawazo yangu ni moto na unaunguza. Hii sasa ni ngazi ya kuweza kuweka vitu katika kumbukumbu na fikra zake, kwamba anakuwa na nguvu ya kuhifadhi athari za vitu hata kama havitakuwepo mbele yake.

Hii nguvu sasa ambayo inamfanya mwanadamu aweze kuhifadhi mambo pamoja na athari zake ndiyo ambayo huitwa akili, akili ambayo inamwambia mwanadamu kwamba huo ni moto na hii ni sumu hivyo kuwa mbali navyo, na hiki ni kizuri hivyo shikamana nacho na kisha kuacha maamuzi kwa mwanadamu mwenyewe.

Mfano hai:

Chukulia kwamba una mtoto mdogo nyumbani, mtoto ambaye hajawahi na wala hajui kitu kinaitwa nyoka, mara siku moja akiwa anacheza anakatiza nyoka mbele yake, utakuta mtoyo yule moja kwa moja pamoja na kuona nyoka yule na kuingia katika ubongo wake, bado hutakuta ni mwenye kumkimbia bali atamkimbilia na kutaka kumshika. Lakini baada ya kuongeza umri kidogo na akaenda shule na kujifunza kwamba nyoka ni katika wanyama hatari na wenye sumu kali na wanaweza kuua, ikatokea siku ameenda mbuga za wanyama na kuona nyoka bila shaka picha ya maelezo yote kuhusu nyoka itamjia na kumfanya awe mbali na mnyama huyo. Na siri katika hilo ni kwamba tayari maana ya nyoka imeshakaa katika ubongo wa mtoto huyu. Na hivi ndivyo ilivyo kwa kila mwanadamu.

Tofauti ya Muumini wa kweli na asiyekuwa yeye ni umiliki wa Itikadi sahihi inayotokana na mafuhumu (mtazamo) sahihi

Baada ya kuelezea kwa muda juu ya makuzi ya mwanadamu tangu utotoni mpaka anakuwa, na namna ambavyo mtazamo wa mwanadamu huyu unapatikana katika akili yake, sasa umefika wakati wa kuweza kuambatanisha hayo na maisha halisi ya muumini wa kweli na asiyekuwa wa kweli.

Tulisema kwamba mwanadamu yeyote yule baada ya kuwa na mafuhumu kunako hatari za nyoka basi hukimbia pindi amuonapo, hii maana yake ni kwamba mwanadamu huyu ana maarifa kamili juu ya jambo lile, na kama isingekuwa maarifa kamili basi asingalikimbia.

Hivyo tunafikia katika nukta na kusema kwamba, ili mwanadamu aweze kubakia salama siku zote, na aweze kufikia katika malengo ni lazima awe na imani iliyojengeka katika msingi sahihi na wa kweli.

Muumini wa kweli, tangu utotoni mwake anaanza kujifunza mitazamo sahihi, mfano anatambua ya kwamba kusalimiana, kusaidiana, kwenda msikitini, kuswali swala za jamaa, kuheshimu wazazi wawili na mengineyo ni katika mambo mema, hivyo muda wote unamkuta mja huyu anashikamana nayo.

Ndugu msomaji... hii ambayo imejengeka katika moyo wako ndiyo ambayo tunaiita Itikadi, itikadi ambayo kama itajengeka katika misingi sahihi basi ule ufaulu ambao tunautizama utaufikia, na kama itakuwa Itikadi yako imejengeka katika misingi ambayo si sahihi basi kamwe hutoweza timiza malengo hata kama utaona umetimiza kwa mtazamo wa kidunia.

Mwanadamu ambaye unamkuta kwamba ni tapeli mkubwa, anakula riba, anaghushi katika miamala yake, ni mwanadamu ambaye itikadi yake imejengeka katika msingi wa kwamba hakuna maisha bila ya mambo haya, na kwamba mbona watu wote hufanya hivyo, mtazamo ambao si sahihi kabisa. Bali inabidi ajengeke katika mtazamo wa kwamba kuna Mungu ambaye anaona kila kitu, na kwamba yeye ndiye mruzuku wa wote na kwa njia ambazo amezitaka kwa waja wake.

Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe ni wenye kujengeka kwa misingi ya Itikadi zilizo sahihi.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.