Shahada ya Imamu Zainul Abidin (as)

Ni imamu wa nne kati ya maimamu 12 ambao wametajwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saww) kwa anuani ya viongozi waongofu baada yake, ni Imamu ambaye amepitia kipindi kigumu tangu uhai wake mpaka Mwenyezi Mungu anamchukua na kukutana naye, si mwingine bali ni Ally bin Hussein bin Ally bin Abi Talib (as).

Zainul Abidin kwa maana ya kipambo cha wachamungu ni moja ya sifa zake kutokana na wingi wake wa kumuabudu Mwenyezi Mungu (swt).

Inaelezwa kwamba baada ya tukio la Karbala ambalo lilimkuta akiwa ni mgonjwa, Yazid alikuwa akitafuta sana mbinu za kuhakikisha kwamba anammaliza kwa njia yeyote ile, kwani miongoni mwa malengo yake makubwa ni kuhakikisha kuwa anamaliza kabisa kizazi cha Mtume katika uso wa ardhi. Kutokana na hilo mara kwa mara Yazid alikuwa akikutana na Imamu kwa ajili ya kuongea naye huenda angekutana na majibu ambayo yangekuwa ni sababu za kutekeleza azma yake. Siku moja Yazid akaamrisha Imamu aletwe mbele yake, mara baada ya kuletwa akaanza kumuuliza maswali huku Imamu akiwa anajishughulisha na kuvuta uradi na kumsabihi Mwenyezi Mungu, jambo ambalo lilimkera sana Yazid na kusema "...Unapata wapi ujasiri wa kuvuta uradi hali ya kuwa mimi nakuuliza?..”. Imamu akamjibu kwa kusema ".....Baba yangu alininukulia kutoka kwa babu yangu kwamba alisema endapo mja ataamka asubuhi akaswali kisha kabla ya kuzungumza na yeyote yule akachukua uradi wake na kusema

"...اللهم انی اصبحت و اسبحّک و امجدک و احمدک و اُهللک بعدد ما ادیر به سبحتی

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika nimeamka hali ya kuwa nakusabihi, nakusifu, nakutukuza, na nakupwekesha kwa idadi ya mzunguko wa Tasbihi yangu hii...” basi mpaka atakapokuwa anataka kupanda tena kitandani kwa ajili ya kulala (usiku), kwa kila atakachoongea atakuwa anahesabiwa malipo ya mwenye kumtaja Mwenyezi Mungu....”

Kutokana na tukio hili Yazid akasema "....Hakuna wakati ambao nimezungumza na mmoja wenu ila atanijibu jibu zuri..” Kisha akampa Imamu zawadi na kuamrisha aachiwe huru.

Kwa mujibu wa pokezi nyingine katika kuashiria namna ambavyo Imamu aliachiwa huru na Yazid ni kwamba baada ya tukio la Bibi Zainab (as) kutoa hotuba nzito kiasi kwamba Yazid alijikuta anapiga mayowe, aliwauliza watu wa Sham kama kuwataka ushauri juu ya nini akifanye kwa mateka wa Karbala?, kuna ambao walitoa rai kwamba nao wauliwe, lakini bwana mmoja kwa jina la Luqman bin Bashir akasema "...Hebu jaribu kufikiria, laiti kama Bwana Mtume angelikuwepo basi angalifanya nini kwa mateka hawa?, na wewe fanya mfano wake...”.

Kisha Imamu Baqir ambaye pia alikuwa moja ya mateka, akaongea maneno ambayo ni hoja tosha juu ya kutokuwepo haki ya kuuliwa kwao, jambo ambalo lilimfanya Yazid asibakie na njia zaidi ya kwaachia huru, hivyo akainama nchini na kutoa hukumu kwamba waachiwe huru.

Kwa namna yeyote ile ni kwamba Yazid alikuwa akitafuta sana njia za kumteketeza mtukufu huyu, lakini kila mara alikutana na hoja nyingi zenye kumzuia kufanya hivyo. Imamu mwenyewe anasema "....Hakuna muda ambao Yazid alikuwa akituita tukawa hatuna shaka ya kuuliwa” Kwa maana walikuwa wanajua kuwa kizazi hichi kubakia kwake ni sawa na bure kazi yao ya Karbala.

Imamu Zainul Abidiz alifariki lini?

Kama ambavyo wanahistoria wametofautiana katika siku ya kuzaliwa kwake, vile vile katika siku, tarehe na hata mwaka wa kufariki kwake pia kuna tofauti baina ya wanahistoria. Lakini kwa kila aina ya tofauti hakuna aliyetoka kati ya mwaka 92 mpaka 100 hijiria, pamoja na kwamba kati ya hiyo miaka ya 94 na 95 ndio miaka ambayo imekuwa mashuhuri sana.

Kwa mujibu wa Hussein bin Ally, mtoto wa Imamu Zainul Abidin ni kwamba baba yake alifariki mnamo mwaka 94, na ndio maana maulama wakubwa kama vile Sheikh Mufid, Sheikh Tusiy na wengineo wanaamini kwamba ndio mwaka aliofariki Imamu.

Ama kwa mujibu wa riwaya ambayo imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq kupitia Abu Basir ni kwamba Imamu Zainul Abidin alifariki akiwa na miaka 57 ambayo ilikuwa ni mwaka 95 Hijiria.

Usiku wa Mwisho wa maisha yake:

Imamu Sadiq anasema "...Usiku wa mwisho wa maisha yake, Imamu alimuita mwanawe (Imamu Baqir) na kumwambia amletee maji kwa ajili ya kuchukua udhu, Imamu Baqir akainuka na kuleta maji ambayo baba yake akasema ".Ewe mwanangu, haya maji hayafai kuchukulia udhu, kwani ndani yake kuna panya amefia”. Imamu Baqir akainuka na kwenda kuchukua taa na kukagua na kukuta ni kweli kulikuwa na panya amefia humo, hivyo akainuka na kwenda kuchuka maji mengine na kumletea baba yake.

Aliporudi na wakati baba yake akiwa anachukua udhu, Imamu Zainul Abidina akaanza kumwambia mwanawe "....Ewe mwanangu, huu ndio usiku ambao umetengwa kwa ajili ya kutimia ahadi yangu”. Kisha akampa usia wa kumlinda vizuri ngamia wake ambaye inasemekana ndiye aliyekuwa akimtumia katika safari zake zote za Hijja.

Kufariki kwake:

Ukiachana na wanahistoria kutofautiana kunako mwaka wa kufariki kwake, pia siku hasa ya kufariki kwake wametofautiana. Kuna ambao wanasema ni tarehe 18, wengine 22, ila yenye nguvu sana ni tarehe 25 ya mwezi wa Muharram.

Na hii ni kwa mahesabu ya kwamba Imamu Zainul Abidin aliishi utawala wa Imamu Ally kwa miaka miwili, kisha akaishi katika utawala wa Imamu Hassan kwa muda wa miaka 10, kisha akaishi katika utawala wa baba yake kwa muda wa miaka 10, kisha utawala na Uimamu wake pia ulidumu kwa miaka 35.

Alipozikwa:

Baada ya kufariki kwake, watu wa Madina waliambatana katika kumsindikiza na kwenda kumlaza katika sehemu tukufu ya Baqee, sehemu ambayo watu watukufu wakiwemo baadhi ya maimamu, mke wa Mtume, mama wa Imamu Ally na baadhi ya masahaba watukufu wamezikwa hapo.

Pembeni kabisa ya kaburi la baba yake mkubwa Imamu Hassan Al Mujtaba ndipo alipozikwa Imamu huyu.

Ni nani alimuua Imamu Zainul Abidina?

Kuna tofauti kunako muuwaji mkuu wa Imamu Zainul Abidina, kuna ambao wanasema ni Walid, kama ambavyo pia wanasema kuwa ni Hisham bin Abdul Malik. Lakini kauli yenye nguvu ni kwamba Walid ndio alihusika katika kumuwekea sumu Imamu na hivyo hata kama Hisham atakuwa anatajwa basi ni kwa amri ya Walid.

Watu wa Madina na kuomboleza kwao:

Said bin Musayad ananukuu "....Baada ya kufariki Imamu watu wote wa Madina walijiwa na habari, na wote wakaungama katika kumuombea na kumuomboleza kifo chake, hakuna hata mmoja ambaye alibakia msikitini bila ya kumuomboleza....”

Inapokelewa kuwa Imamu alikuwa na ngamia wake ambaye alikuwa akimtumia katika safari zake za Hijja, ngamia ambaye alimpenda sana kiasi kwamba hakuna hata siku moja ambayo aliinua mkono wake na kumpiga. Baada ya kufariki Imamu ngamia yule kila siku alikuwa akienda katika kaburi la Imamu na kuanza kujigaragaza huku machozi yakimtoka kwa huzuni. Habari ya tukio hili zikamfikia Imamu Baqir ambaye alienda na kuongea na yule ngamia kwamba ainuke na awe mpore kwani Mungu atambariki kwa hilo.

Ngamia yule aliinuka na kukaa kwa muda na kisha kurudi tena juu ya kaburi lile na kufanya kama alivyokuwa akifanya.

Kitendo hicho kilijirudia mpaka maa ya tatu Imamu Baqir aliposema kuwa wamuache ngamia yule, kwani anajua kuwa karibuni ataungana na mmiliki wake. Baada ya tukio hilo hazikupita siku tatu mpaka kufariki kwa ngamia yule.

Hii ni ishara kwamba Imamu Zainul Abidin hakuliliwa tu na binadamu, bali hata wanyama pia walimlilia. Na hii ni kutokana na wema wake kwa viumbe vyote bila kubagua.

Mwenyezi Mungu atujaalie tuweze kuchukua kiigizo chema kutoka kwa Imamu huyu.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.