FUNGAMANO LA ELIMU NA DINI


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Utangulizi

Kwa jina la Mola Muumba mwelevu msamehevu mwenye huruma, katika mtiririko wa makala hizi kwa uwezo wa mwenyezi Mungu tutazungumzia suala muhimu sana liliopo katika jamii ya wenye ilimu waliokuwa na ufahamu wa mitazamo mbalimbali na fikira ziliopo ulimwenguni, kwa maana kuna changamoto mbalimbali wanazokutana nazo watafiti waliokuwa wanafuata mafunzo ya dini au wanaoamini usahihi wa dini! Changamoto hii inashadidi zaidi baada ya kukutana na watu wasiokuwa na imani kuhusu uwepo wa Mungu na suala zima la uwepo wa kitu kinachoitwa dini na mambo ya mitafizikia au kusoma nadharia za watu wenye mitazamo kama hiyo.

Kwa ufupi ukiangalia historia ya fungamano la Elimu ya Sayansi na Dini, utaona kwamba kulitokea mvutano mkubwa baina ya wafuasi na wasimamizi wa Dini na wataalamu wa tafiti za Kisayansi, hususan katika Karne za kati katika bara la Ulaya kati ya viongozi wa Kanisa na watafiti kama vile Galileo mnamo karne ya kumi na sita na wengineo wengi waliokuja baada yake, ambapo Kanisa na viongozi wake walisimama kidete kupinga kwa nguvu zote tija ya tafiti ziliofanywa na watafiti wa elimu ya Sayansi, kwa sababu kwamba tija ya tafiti zao zinakinzana na maandiko matakatifu ya Biblia, hivyo kwakuwa Kanisa ndio lilikuwa na nguvu na ndio lilikuwa msingi wa kila kitu, lilikataa katukatu kuamini tija ziliofikiwa na watafiti hao ambapo historia inatueleza kuwa Kanisa lilitoa hukumu ya kunyongwa kila aliyefanya utafiti ambapo ukatoa tija inayokinzana na mafundisho na maandiko ya kitabu kitukufu cha Biblia, hivyo basi katika kipindi hicho ndipo watu na wataalamu wakataka kujua na kufahamu fungamano liliopo baina ya mafunzo ya Dini na Elimu ya Sayansi, hatimaye watafiti wengi walikana kuwepo fungamano lolote kati ya Dini na Elimu, isipokuwa pale ambapo mafunzo ya Dini kama hayatakinzana na tija ya tafiti za Elimu ya Sayansi.

Hapo ndipo zikatokea nadharia ya kupinga uwepo na ukweli wa Dini kwakuwa tu mafunzo ya Dini haziendani na tija za tafiti ambazo hutoa majibu ya uhakika, na kutoka na kauli mbiu hii kuwa Dini haina ukweli kwa sababu semi na mafunzo yake hatuwezi tukayafanyia uchunguzi na kufikia tija, kwa maana asilimia kubwa ya semi na mafunzo ya Dini yamesimamia mambo na masuala ya Mitafizikia, hata kufikia mbali zaidi ya hapo kwa kusema kuwa dini ni katika masuala ya ngano alioyatengeza mwanadamu hasa pale aliposhindwa mwanadamu huyo kuyapatia uvumbuzi baadhi ya mambo yaliokuwa yanampata katika maisha yake, kama vile ukame, mafuriko, matetemeko ya Ardhi, maradhi yaliomkuta nk, ambapo baada ya kushindwa kuyapatia uvumbuzi mambo hayo, ndipo akatengeza kitu na kudai ni Mungu ambaye husababisha kupatikana kwa majanga hayo.

Hivyo basi suala la Dini halina nafasi katika ulimwengu wa sasa hususan baada ya mwanadamu kufikia kiwango kikubwa cha Tekinolojia inayomuwezesha kufahamu sababu za mambo hayo na kupatia utatuzi wake! Lakini baadhi ya watafiti wakataka kufanya marekebisho kunako tafsiri ya mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Biblia hata kiwe chenye kuendana na tija ya tafiti zitakazokuwa zinafanywa.

Mvutano wa fungamano la Elimu na Dini liliendelea hata kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya Kikristo mpaka hapa tulipo, lakini kwa upande mwingine anaweza akatokea mtu akasema kuwa suala hili halina nafasi kufanyiwa uchunguzi kwa sasa katika Dini ya Uislamu kwakuwa chanzo cha malumbano ilikuwa katika viongozi wa Kanisa na watafiti wa masuala ya kisayansi hata kufikia kuitenga Dini na masuala ya kielimu. Jambo ambalo halipo katika dini ya Uislamu, kwa maana mafunzo ya Uislamu hayakinzani na tafiti za kisayansi, ama kimsingi hatuwezi kujipaka mafuta kwa mgongo wa chupa na kuona kuwa hilo ndio jibu, katika hali ambo sababu zilezile zinaweza zikashamili dini zote katika kipindi hichi, hivyo kwa upande wangu tutakuwa tunalizungumzia suala hili yaani fungamano la elimu na Dini, ambapo dini tunayokusudia ni Dini ya Kiislamu, pamoja yakuwa baadhi ya nyakati tutazungumzia mitazamo ya dini nyingine zisiokuwa za Kiislamu, hivyo basi tumuombe mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kuimudu mada hii na kukidhi mahitaji ya wale waliokuwa na kiu ya kutaka kufahamu suala hili.

Itaendelea....