Umakini wa Quran katika kutumia maneno - 2

Mke : Ni yule ambaye anakuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume, na pia kunakuwa na hali ya mwendano wa kifikra na mapenzi baina yao. Ikikosekana nguzo moja basi ujue maana halisi inapotea.

Quran inasemaje?

وَقُلْنَا يَا آدَمُ اسْكُنْ أَنْتَ وَزَوْجُكَ الْجَنَّةَ وَكُلَا مِنْهَا رَغَدًا حَيْثُ شِئْتُمَا وَلَا تَقْرَبَا هَٰذِهِ الشَّجَرَةَ فَتَكُونَا مِنَ الظَّالِمِينَ

"....Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu...”[1]

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَنْ يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا

Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu….”[2]

Naam, hapa Mwenyezi Mungu ametumia neno mke kwa wake wa Mtume Muhammad na Mke wa Nabii Adam kutokana na muowano wa kimwili, kimawazo na hata imani pia.

Unaweza kujiuliza.....

Ikiwa neno Mke hutumika kwa mwanamke mwenye mahusiano thabiti na mwanaume kuanzia kimwili mpaka kimawazo na imani, basi vipi katika dua ya Nabii Zakaria tunakuta ametumia neno mwanamke hali ya kuwa hakuwa ni mwenye kutofautiana naye kiimani wala kimwili?. Angalia Nabii Zakaria anasemaje:

قَالَ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا وَقَدْ بَلَغْتُ مِنَ الْكِبَرِ عِتِيًّا

"....Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nitakuwa na mwana hali ya kuwa mwanamke wangu hazai, na mimi nimeshafikia ukongwe katika uzee?..”.[3]

Pamoja na usahihi wa swali au mawazo haya, bado haiwezi kuwa kasoro katika umakini wa Quran katika kutumia maneno katika maana yake sahihi. Ukirejea historia ya Nabii Zakaria bila shaka utakuta ni namna gani swala la kukosa mtoto kwa miaka mingi lilikuwa ni changamoto ya maisha yake yeye na mke wake, na hii ipo wazi hata katika maisha ya kila siku ya wanandoa pale ambapo mwenyezi Mungu anawapa mtihani wa kutopata mtoto basi inawezekana mmoja wao akaghafilika kunako mtihani ule na kujikuta akitofautiana na mwenzake kimawazo. Wakati mwingine kuanza kumwangalia kama vile yeye ndio mkosaji na msababishaji wa yote, ili mradi tu kunakuwa na tofauti baina yao. Na hilo ndilo ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa analikusudia hapa katika maneno ya Nabii Zakaria, kwamba pamoja na mahusiano mazito yaliyopo baina ya Nabii na Mke wake, linapokuja swala la watoto basi kulikuwa hakuna maelewano mazuri baina yao. Ndio likatumika neno Mwanamke na si Mke, yaani katika kadhia ile mahususi.

Na hili pia unaweza kuliona baada ya kuruzukiwa mtoto, halikutumika tena neno mwanamke bali lilitumika neno mke. Mwenyezi Mungu anasema:

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ

"…. Nasi tukamjibu dua yake na kumruzuku Yahya na kumfanya mwema mke wake….”

Sio kwamba mke wake hakuwa mwema, hapana, bali katika swala zima la kupata mtoto ndio kulikuwa na hali ya kutoelewana, lakini baada ya kupatikana kwa mtoto mambo yakawa safi na Mwenyezi Mungu akatumia tena neno Mke.

Ungana nami katika sehemu ya mwisho.
Sh Abdul Razaq Bilal (AbuuAsghar).

[1] Surat Albaqara aya 35

[2] Surat Ahzab aya 59

[3] Surat Maryam aya 8