Umakini wa Quran katika kutumia maneno - sehemu ya mwisho

Mwenza: huyu ni mwanamke ambaye hana mahusiano ya kimwili, mapenzi wala kimawazo na mwanaume, na hapa tunaweza kutumia maana hii hata pale yanapokosekana mahusiano baina ya mtu na mtu mwingine, kwa maana ya kwamba wapo pamoja kwa kuwaangalia, ila hakuna mahusiano ya aina yeyote baina yao. Lakini tubakie katika mfumo wetu wa wanandoa au wapendanao.

Quran inasemaje?

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ

وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ

وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ

"....Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, Na mamaye na babaye, Na mwenza wake na wanawe….”

Mwenza anayekusudiwa hapa ni huyu ambaye mimi namzungumzia katika makala hii, mwanamke ambaye unaishi naye pamoja leo hapa duniani, lakini kutokana na uzito wa siku ya kiama hatokuwa na nasaba yeyote kwake, si kimwili wala kimawazo. Yaani anakuwa ni kama ajnabi kwako kutokana na uzito wa siku hiyo.

Muhimu hapa ni kutaka kuashiria kwamba neno mwenza limetumika na Quran kuonyesha kwamba baina ya mwanaume huyu na mwanamke yule hakuna aina yeyote ya mahusiano na ndio maana neno mwenza likatumika.

Angalia pia neno mwenza limetumikaje na Quran katika kadhia nzima ya kukanusha kwamba Mwenyezi Mungu ana mtoto. Anasema :

أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ وَلَدٌ وَلَمْ تَكُنْ لَهُ صَاحِبَةٌ

"….Vipi atakuwa na mwana hali ya kuwa hana mwenza!?.....”[1]

Kwa maana ya kwamba achilia mbali swala la kwamba Mwenyezi Mungu ana ambaye wanaweza kuendana kimawazo na kimapenzi na mwingine ili awe mke wake, yaani hakuna hata ambaye anaweza kuendana naye kwa namna yeyote ile, si kimwili kwa maana Mungu hana mwili wala kiana yeyote ambayo unaweza kuidhania. Hivyo utumiaji neno mwenza hapa umekanusha kila aina ya mahusiano ambayo unaweza kuyafikiria katika swala la kumnasibisha Mungu na mwana.

Ametakasika Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma na miujiza.

Namalizia makala yangu kwa kuuliza swali kwa kina baba wote, hiyo ndio Quran katika utumiaji wa maneno hayo matatu kunako jinsia au upande wa pili, je wewe kama wewe unatumia neno gani kwa huyo uliye naye ndani?.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal (AbuuAsghar).[1] Suat an am aya 101