Je Quran Inazungumziaje Uumbaji Wa Dunia?

Kila siku Mwanadamu ajitahidi kuvumbua na kugundua vitu tofauti ili kujua sababu ya kuwepo vitu hivyo au kutokuwepo, upeo huo wa Mwanadamu humpelekea kujiuliza maswali mengi kunako Ulimwengu huu na kutaka kujua ni siri gani iliyojificha ndani mwake, na kujiuliza ulimwengu uliumbwa vipi?! Na ulichukua muda gani wa kuumbwa kwake?! na...

Kutokana na maswali hayo hadi sasa Wanazuoni wa elimu ya Cosmology walitoa nadharia tofauti kunako kuumbwa Dunia, na nadharia zote hizo hakuna hata moja ilionekana kuwa imeafikiwa na wote, nadharia hizo tutaziashiria baadaye baada ya kuona mtazamo wa Quran kunako kuumbwa Dunia.

Bila shaka Quran ni Kitabu cha uongofu, na ili kufikia katika malengo hayo ilitumia njia tofauti ili kumfahamisha Mwanadamu kuwa Mwenyezi Mungu ni Mweza  wa kila kitu, na moja miongoni mwa njia hizo ni kutumia elimu ya Cosmology ili kumuongoza Mwanadamu.

Quran haijazungumzia moja kwa moja jinsi ya kuumbwa Dunia ila imeashiria tu mwanzo wa Dunia jinsi ulivyo kuwa, na Aya mbili  ndizo zimeashiria suala hili na kutafsiriwa tofauti ila madhumuni yao ni mamoja, na Aya hizo ni:

1-    ثُمَّ اسْتَوَى إِلَى السَّمَاءِ وَهِيَ دُخَانٌ...

"Kisha aliumba mbingu, na ilhali zilikuwa moshi...” Quran 41/11.

Na Neno(دُخَانٌ) katika Aya hii linamaanisha  Moshi au Gesi na kuwa sambamba na maana Kilugha, ama Neno(السَّمَاء) linamaanisha anga au kila kilichokua juu, na Neno(اسْتَوَى)linamaanisha mapumziko, kuwa sawa vitu viwili na kumiliki kitu.

 

 

2-    أَوَلَمْ يَرَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ كَانَتَا رَتْقًا فَفَتَقْنَاهُمَا وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ.

"Je! walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukaziachanisha? Na tukaumba kwa maji kila kiumbe kilicho hai? Basi je, hawaamini? ”Quran 21/30.

Na Neno(رَتْقًا) lina maana ya kuambatana na kuambatanisha, na Neno(فتَقاً) maana yake ni kuachana na kuachanisha.

Dhahiri ya Aya mbili hizi yaonyesha kuwa kabla ya kuumbwa Dunia kulikuwepo Gesi, na Gesi hiyo ilisababisha Mbingu na Ardhi kuambatana ila Mwenyezi Mungu aliziachanisha.

Ayatullah Makarim Shirazi: katika kufafanua sentensi hii kasema "Kisha aliumba mbingu, na ilhali zilikuwa moshi...” ni ishara  ya kuwa mwanzo wa Dunia ilikuwa ni mkusanyiko wa Gesi, na maneno haya ni sambamba na uhakiki uliofanywa hivi karibuni kunako chanzo cha kuwepo Dunia, kuthibiti hilo ni kutokea Sayari nyingi kupitia mkusanyiko wa Gesi.

Kauli tatu za Wafasiri wa Quran kunako Aya hii:

1-Kushikana Mbingu na Ardhi ni ishara ya kuanza kuumbwa Dunia, kulingana na nadharia za Wanazuoni ni kuwa Dunia ni mkusanyiko wa Gesi na Mvuke uliokusanyika baada ya miripuko ya anga, na kulingana na miripuko hiyo ikakusanyika Gesi sehemu mbalimbali na kusababisha kutokea Sayari tofauti Sayari ya Dunia na nyinginezo.

2-Kushikana Mbingu na Ardhi maana yake ni kuwa sawa Mbingu na Ardhi, ama baada ya kupita muda kadhaa ikaachana Mbingu na Ardhi na kuanza kuota mimea na kuwepo viumbe tofauti katika Mbingu na Ardhi.

3-Kushikana Mbingu na Ardhi inamaanisha kutonyesha mvua, na Kushikana Ardhi na Mbingu ni kutokuwa mimea katika Ardhi katika muda ule, ama Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake alishusha mvua na akaotesha mimea katika Ardhi.

Pia Wanazuoni na Maulama waitakidi kuwa Gesi au moshi ilikua hatua ya kwanza ya kuumbwa Dunia kwani hapo kabla Mbingu na Ardhi zilikuwa zikishikana na baadaye  zikaachana.

Baadhi ya Nadharia za Wanazuoni wa elimu ya Cosmology:

1-Dunia ni athari ya mlipuko mkubwa uliotokea kabla ya miaka milioni 20 iliopita, baada ya mlipuko huo Gesi na Moshi ulijikusanya sehemu moja na kuanza kuweka kitu kama nukta ndogo na baada ya muda ikawa nukta ile ikikua miaka hadi miaka na hatimaye kutokea Sayari ya Dunia hii tuliyomo, nadharia hii ni ya mwaka 1900.

2-Dunia ni athari ya miripuko midogo iliokuwa ikitokea na kukusanyika sehemu moja, baada ya miaka kadhaa kuwa Sayari ya Dunia. Pia kuna nadharia nyingi kunako kuumbwa Dunia ila tu muda hutoshelezi kutaja zote.

Kwa mantiki hii kama tulivyo tangulia kusema hapo kabla, Quran haijazungumzia moja kwa moja jinsi ya kuumbwa Dunia, ila tu iliashiria mwanzo wa Dunia ulivyo kuwa, kulinga na ishara hizo za Quran kukatolewa tija kutokana na nadharia za Wanazuoni, na nadharia iliokuwa karibu na ishara ya Quran ni ile nadharia ya Wanazuoni inayosema kuwa; Dunia ni athari ya mripuko mkubwa uliotokea kabla ya miaka milioni 20 iliopita. Kwa upande mwingine kulingana na  wingi wa nadharia kunako kuumbwa Dunia kwa Wanazuoni wa elimu ya Cosmology nadharia zilizokuwa kinyume na ishara ya Quran haziwezi kutabikishwa na kuthibitisha kuumbwa Dunia kwa kuwa kwake kinyume na ishara hizo.

Hii ndio Quran mbayo ni muujiza wa milele isio na kasoro ndani yake, Quran imezungumzia mambo mengi ambapo hapo kabla Wanazuoni walikua hawaelewi Quran inamaanisha nini, baada ya kupita miaka ndio Wanazuoni na Wagunduzi walielewa Quran inamaanisha nini.

 

Na Sh Khamis Sadiki