MAISHA YA IMAM HASANI AL ASKARI (A.S)
MAISHA YA IMAM HASANI AL ASKARI (A.S)

JINA LA UKOO

Jina lake ni Hasan. 'Kunyat' (Jina la heshima) ni Abu Muhammad.

Na kwa kuwa aliishi katika sehemu ya jiji la Samarrah iliyoitwa Askari, jina lake lililojulikana zaidi ni lile la Askari.

BABA YAKE NA MAMA YAKE

Baba yake alikuwa Imamu Ali Naqi(a.s). Na mama yake ni Bibi Salil Khatun ambaye alikuwa mfano wa utawa wa hali ya juu, Uchamungu, Utakatifu na Ukarimu.

KUZALIWA KWAKE

Alizaliwa tarehe 10 ya Rabi-ul-Thani (Mfunguo Saba) mnamo mwaka 232 Hijiriya huko Madina.

KULELEWA KWAKE

Alikaa na baba yake kwa muda usio pungua miaka kumi na moja katika sehemu ya kwao. Muda huu unaweza kuitwa muda wa amani. Baada ya hapo ilimbidi Ali Naqi(a.s)aende Iraq na Imamu Hasan Askari(a.s)alifika Samarrah na baba yake baada ya taabu zote za safari ndefu. Huko aliishi na baba yake jela chini ya uchunguzi na wakati mwingine aliishi katika uhuru kidogo. Lakini kila wakati aliishi na baba yake akijifunza kwa makini tabia yake katika hali za kila aina ambayo, pamoja na Mwanga alioupewa na Mwenyezi Mungu, alikuwa kamili kabisa kwa kazi ambazo alitazamiwa kuzishika.

UIMAMU WAKE

Mnamo mwaka wa 254 Hijiriya, Imamu Ali Naqi(a.s)alifariki wakati Imamu Hasan(a.s)akiwa na umri wa miaka 22. Miezi minne kabla hajafa, Imamu Ali Naqi(a.s)aliutangaza Uimamu wa mwanawe na aliwaita wafuasi wake waje kushuhudia.

WAFALME NA VIONGOZI WA ZAMA ZAKE

Mu'tazz Billah Abbasi alikuwa Mfalme wakati Imamu Hasan Askari(a.s)alipopata Uimamu. Baada ya Mu'tazz kupinduliwa, Muhtadi alitawala kwa muda wa miezi kumi na moja na siku chache naye alirithiwa na Mu'tamad. Hakuna hata mmoja wa hao Wafalme aliyemwacha Imamu(a.s)akae kwa amani. lngawaje Serikali ya ukoo wa Bani Abbas ilikuwa katika machafuko, licha ya matatizo hayo yote wote waliona afadhali kumwacha Imamu(a.s)abaki humo jela. Sababu muhimu ilikuwa ni ile hadithi ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w)ibashiriyo kuwa atafuatiwa na Maimamu kumi na wawili, wa mwisho wao akiwa ni Mahdi Akhirul Zaman (Imamu wa Zama hizi) na Qaimu Ali Muhammad (endelezo la Ukoo wa Mtukufu Mtumes.a.w.w). Hadithi hii ilienea kote katika ulimwengu wa Kiislamu.

Watawala wa ukoo wa Bani Abbas walijua sana kuwa hao ndiyo makhalifa halali wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w)na katika hao Imamu Hasan Askari(a.s)alikuwa wa kumi na moja, kwa hiyo mwanawe atakuwa ni kutimia kwa ubashiri wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w). Kwa hiyo kila wakati walikuwa wakizuia kuwepo kwa Khalifa wake. Ndiyo maana hawakuacha kumchunguza Imamu Hasan Askari(a.s)kama ilivyokuwa kwa baba yake, hivyo waliona kuwa ni lazima kumfungia katika jela ya peke yake. Lilikuwa jambo tofauti kabisa wakati mapinduzi ya kisiasa yameacha pengo katika nyakati za ufungwa wake, Iakini kila Mtawala aliyetawala alifuata shauri la watawala wa kabla yake la kumfunga Imamu tena. Hivyo karibuni muda wake mfupi wote wa Uimamu aliumalizia jela. Kuchungwa kwake kulifikia kilele wakati wa utawala wa Mu'tamad, ingawaje naye, kama wale wengine wa nyuma wote, alikijua vizuri cheo cha Imamu(a.s). Kwani, wakati mmoja njaa iliingia nchini na mtawa mmoja wa Kikristo alidai kuwa anaweza kufanya mvua inyeshe na alifaulu kufanya hivyo. Hivyo kulikuwepo mlegolego katika imani ya Waislamu. Mu'tamad alihofia kuwa serikali yake itaangushwa hivyo aIimwita Imamu Hasan Askari(a.s)kutoka jela. Imamu(a.s)alimwomba mfalme amruhusu mtawa huyo kuja hadharani na kufanya muujiza wake mbele ya Imamu mwenyewe na alimtuma mtu fulani amwendee haraka yule mtawa wakati alipoinua mikono yake kuomba mvua na kuchukua cho chote kile alichokuwa nacho mikononi mwake. Wakati mambo haya yanafanika yule mtawa alionekana akionyesha mfupa kwenye jua na mvua zilianza kunyesha. Imamu alimwambia kuwa mfupa ule ulitoka katika mwili wa Mtume fulani na kwamba ilikuwa ni tabia ya mifupa va Mitume kuwa kama inaonyeshwa kwenye jua, mawingu yatatanda. Kisha Imamu aliufunika ule mfupa na yeye mwenyewe aliomba mvua inyeshe na ikanyesha kwa wingi sana.

KUTEULIWA KWA WAJUMBE

Maimamu wa Ukoo wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w)wakati wote walifanya kazi zao wakiwa Maimamu katika hali zote. Imamu Hasan Askari(a.s)alikuwa akiishi katika vizuizi vya namna nyingi sana kwamba ilikuwa vigumu kwa wenye kupenda kujifunza kutoka kwa Imamu kuweza kuonana naye. Hivyo Imamu aliwateua watu wenye kuaminika kutokana na uaminifu wao kuelewa kwao na elimu yao. Wajumbe hawa waliwaongoza watu kwa kadiri ya uwezo wao na kama palitokea tatizo lililokuwa zaidi ya uwezo wao basi walingojea mpaka wapate nafasi ya kumuona Imamu ili awape majibu na wao wawape watu. Mpango huu haukukataliwa sana na serikali kwa sababu ulihitaji mtu mmoja mmoja kwenda kumwona.

Wajumbe hawa walifanya kazi nyingine zaidi. Khums (moja ifananayo na Zaka) ilikuwa inatolewa na wale waliokiri kuwa Imamu alikuwa mwakilishi wa serikali ya Mwenyezi Mungu na kupewa hao wajumbe ambao waliitumia kama alivyoagiza Imamu. Watu hawa walipata jaribio gumu kweli, kwani wapelelezi wa serikali ya ukoo wa Bani Abbas walikuwa wakipeleleza shughuli zao. Hivyo Bwana Uthman bin Sa'id na mwanawe Abu Ja'afar Muhammad bin Uthman ambao walikuwa wajumbe mashuhuri wa Imamu walifungua duka kubwa la mafuta na manukato mjini Baghdad walikokuwa wakikaa ili kuepukana na kutiliwa wasiwasi na watu waliokwenda kumwona Imamu(a.s). Kwa hiyo licha ya shari ya serikali, kazi ya Uislamu ilikuwa inaendelea.

MAADILI YAKE

Maisha yake yalikuwa ni yale ya wenzake wa Ukoo wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w). Alikuwa wa pekee katika upole ustahimilivu, ukarimu, uvumilivu, huruma na Kumuabudu Mungu kwake kulifanyika kiasi ambacho, hata wakati alipokuwa kafungwa katika kizuizi kikali sana kila Mu'tamad alipoulizia habari zake, aliambiwa kuwa Imamu alikuwa aki funga mchana na usiku kucha akisali na alikuwa hasemi neno ila maneno ya ibada tu.

Ingawaje Imamu(a.s)alikuwa na uhuru mdogo sana hata hivyo ilipowezekana watu walikwenda kumwona na kutoa hamu yao ya kujifunza na walirudi wakiwa wametosheka kabisa.

Maadili yake na tabia zake viliwavutia watu wote. Bwana Ahmad bin Khazan aliyekuwa mwangalizi mkuu wa zaka, khums, sadaka, n.k., katika Mji wa Qum (nchini Iran), kila walipotajwa mbele yake Masayyid wa Alawi (wa ukoo wa Alia.s), alisema kuwa alikuwa hajapata kuona mtu mwingine mwenye tabia nzuri kama za Imamu Hasan Askari(a.s)au Mchamungu na mwenye kumwabudu Mungu, mpole, anayeheshimiwa,mwenye kustahili heshima au anayefikiriwa kuwa yu astahili kuheshimiwa sana.

Alipofariki Imamu Ali Naqi na watu wote walipokuwa wakishughulika na mipango ya maziko yake, baadhi ya watumishi wa nyumbani waliiba vitu kadhaa. Walikuwa hawakufikiria kuwa labda Imamu angejua yote hayo.Shughuli za maziko zilipomalizika aliwaita wote wale waliohusika na kuwaambia kuwa kama wakimwambia ukweli atawasamehe kwa yale yote waliyoyatenda, la sivyo watavirudisha vile vitu walivyoviiba na atawaadhibu. Kisha akavitaja vile vitu vyote kila mmoja wao alivyoiba na walipokubali aliwasamehe.

UMAARUFU WAKE WA KIELIMU

Ingawa aliishi miaka ishirini na nane tu, aliiua kiu ya kisomo ya wanachuoni wengi wa wakati ule na pia aliweza kupambana vya kutosha na mafalsafa wa wakati huo ambao walikuwa wakieneza mambo yaliyokuwa kinyume cha mafundisho ya dini.

Mtu mmoja aliyeitwa Ishaq Kindi alikuwa akiandika kitabu juu ya migongano ya aya za Qur'ani. Habari hizi zilipomfikia Imamu(a.s)alianza kutafuta nafasi. Siku moja wanafunzi kadhaa wa Ishaq aliwauliza, "Hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye akili za kutosha kumshauri mwalimu aache upuuzi aufanyao juu ya Qur'ani? Walisema, "Tutafanya nini na sisi ni wafunzi wake tu"? "Imamu alisema, "Vizuri, je, mnaweza angalau kumwambia yale ninayowaambieni? Wakasema, "ndiyo tunaweza kufanya".

Ndipo Imamu alipowaonyesha baadhi ya zile aya za Qur'ani zinazozungumziwa na akawaambia waende wamuulize mwalimu wao kama maneno ambayo alikuwa anayatumia katika hoja zake yana maana hizo tu alizoyachukulia tu au kama kwa kutazama matumizi ya maneno ya Waarabu, maana nyingine za maneno hayo zilipatikana, ambazo kama yakifikiriwa maneno hayo kwa maana hizo yanaondoa suala lolote lile Ia kupingana kwa aya hizi. Kama zipo maana nyingine, basi alikuwa na haki gani ya kung'ang'ania kuyachukua maneno hayo kwa maana hizo alizozichukulia yeye? Kisha Imamu(a.s)aliwaeleza wale wanafunzi maana halisi yaa aya hizo. Nao wakaenda na wakafanya kama walivyoagizwa. Ishaq alipozisikia zile hoja walizozitoa aliwauliza wamweleze walipojifunza yote hayo. Kwanza, walitaka kuficha lakini aliposisitiza kuwa hayo siyo mawazo yao, walikubali kuwa walijifunza kutoka kwa Abu Muhammad, yaani Imamu(a.s). Ishaq alisema "Hakuna mwingine ambaye angelifanya hivyo, isipokuwa mtu wa ukoo wa Mtume". Kisha akachoma yale yote aliyokwisha kuandika.

Huu ni mfano mmoja tu wa yale aliyokuwa akiyafanya Imamu kila siku, akielewa kuwa hiyo ni kazi yake akiwa mrithi wa kweli wa Mtukufu Mtume. Na serikali ikidai kuwa ni ya Kiislamu, ilikuwa inafanya mambo ya zinaa na ulevi, na wakati watawala rahisi waliposhika madaraka ilikuwa ni kuongeza vizuizi tu kwa lmamu. Lakini alikuwa mfano halisi wa subira na uvumilivu na hivyo aliendelea katika njia yake ya kazi hii tukufu.

Katika kukusanya Hadithi za Mtukufu Mtume(s.a.w.w)"wakusanya hadithi" wamechukua hadithi toka kwake. Moja ya hadithi muhimu sana ni ile isemayo, "Mlevi ni sawa na mwenye kuabudu sanamu". Hadithi hii imekaririwa na Bwana Ibn Al-Jauzi katika kitabu chake kiitwacho 'Tabrim-ul-Khamr' (Uharamu wa Kulewa Mvinyo). Na Bwana Abu Na'im Fazl bin Wakin alisema kuwa hadithi hii ni ya kuaminika sana na imechukuliwa kutoka kwenye ukoo wa Mtukufu Mtume na pia imepokewa na kundi Ia masahaba wa Mtukufu Mtume.

Bwana Sam'ani katika kitabu chake kiitwacho 'Kitab-Al-Ansab' ameandika, "Abu Muhammad Ahmad bin Ibrahim bin Hashim Tusi Baladhuri Hafiz Wa'iz alisikia hadithi ya Mtukufu Mtume huko Maka kutoka kwa Imamu atokanaye na dhuria wa Mtume, Hasan bin Ali bin Muhammad bin Ali bin Musa Al-Ridha na akazikusanya".

Zaidi ya bwana huyu, majina ya wanafunzi wengine mashuhuri wa Imamu yanaorodheshwa hapa chini:

1. Bwana Abu Hashim Dawud bin Qasim Ja'fari aliyekuwa Mwanachuoni mzee ambaye aliwaona Maimamu wanne kutoka lmamu Ali Ridha(a.s)hadi Imamu Hasan Askari(a.s)na alisoma kwao wote. Vile vile alikuwa mjumbe wa Imamu Hasan Askari(a.s).

2. Bwana Dawud bin Abi-Zaid Nishapuri aliwaona Imamu Hasan Askari(a.s)na baba yake lmamu Ali Naqi(a.s).

3. Bwana Abu Tahir Muhammad bin Ali bin Hilal.

4. Bwana Abul Abbas Abdullah bin Ja'far Himyari Qummi alikuwa mwanachuoni mashuhuri sana na mwandishi wa vitabu vingi ambavyo miongoni mwao Qurb-al-Asnad bado kipo mpaka leo na ndiyo chanzo cha kitabu kiitwacho Kafi na vitabu vingine.

5. Bwana Muhammad bin Ahmad bin Ja'far Qummi alikuwa mmoja wa wajumbe mashuhuri wa Imamu.

6. Bwana Ja'far bin Suhail Saiqal pia alikuwa mjumbe mashuhuri wa Imamu.

7. Bwana Muhammad bin Hasan Jaffar Qummi alikuwa mwanachuoni mashuhuri na mwandishi wa vitabu kadhaa kati ya hivyo, Basa'irul Darajat kinajulikana. Pia alihifadhi barua walizokuwa wakiandikiana na Imamu Hasan Askari kuhusu sheria za kidini.

8. Bwana Abu Ja'far Humani Barmaki aliandika kitabu cha majibu ya Imamu kuhusu maswali ya sheria za kidini ambayo mwandishi aliandika kumwuliza Imamu(a.s).

9. Bwana lbrahimu bin Abi Hafs Abu Ashaq Katib, Bwana huyu alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Imamu na aliandika kitabu.

10. Bwana Ibrahim bin Mehryar, alikuwa mwandishi wa kitabu kiitwacho 'Kitabul Basharat'.

11. Bwana Ahmad bin Ibrahim bin Isma'il bin Dawud Hamdan Al-Katib Al-Nadim, alikuwa na elimu kubwa ya uandishi wa vitabu na lugha. Aliandika vitabu vingi na alijiambatanisha sana na Imamu.

12. Bwana Ahmad bin Ashaq Al-Ashari Abu Ali Al-Qummi, alikuwa mwanachuoni mwenye elimu ya kutosha. Aliandika vitabu vichache miongoni mwao kikiwemo kitabu kiitwacho "Ilal-Al-Saum", (Falsafa ya Funga).

Haya ni majina machache tu. Patahitajika kitabu kizima kuweza kuyataja majina yote.

Bwana Abu Ali Hasan Khalidi bin Muhammad bin Ali Barqi aliandika Tafsir (kitabu juu ya ufafanuzi wa Qur'ani Tukufu) kwa njia ya imla aliyosomewa na Imamu. Wanachuoni wa kidini wanasema kuwa kitabu hiki kiligawanywa katika juzuu 120.

Kwa bahati mbaya maandishi haya muhimu sana hayapatikani siku hizi. Hata hivyo katika Tafsiri kadhaa kuna kumbukumbu za Imamu ambazo zinaweza zikawa zinatokana na kitabu hiki. Kitabu kingine juu ya somo hilo kilichopo na kinachosemekana kuwa kimetokana na Imamu hakiaminiki. Waraka mrefu wa Imamu, aliomwandikia Bwana Ishaq bin Isma'il Ash'ari na mkusanyo mkubwa wa hadithi za kuaminika, mafundisho na hotuba vimehifadhiwa katika kitabu Kiitwacho 'Tuhaful-Uqul'.

Yote hii ni kazi ya maisha ya muda wa miaka 28, muda ambao miaka sita tu ndiyo aliyokuwa Imamu baada ya kifo cha baba yake Imamu Ali Naqi(a.s)na hiyo pia aliitumia katika hali ya majaribio magumu kama ilivyokwisha elezwa awali.

KUFARIKI KWAKE

Baada ya maisha yenye shughuli namna hiyo kuna uwezekano wa kupatikana wakati wo wote ule kwa ajili ya fitina za kisiasa au lo lote lile lifananalo na hilo? Lakini kuongezeka kwa mvuto wake kwa watu katika mambo ya Kiroho na kuwa kwake chanzo cha Elimu ya Kidini vilikua ndiyo sababu kubwa ya watawala kutaka kuyaondoa maisha yake. Kwa maana dola ya Bani Abbas ingeliweza kusimama iwapo tu, Uislamu wa kweli usingelifahamika; au kwa ujumla hakukuwepo nafasi kwa wafalme wa ukoo huo, na matendo yao yote hayawezi kupata kibali cho chote kile cha raia isipokuwa tu, kama raia hao wakiwekwa gizani kuhusu kuwepo kwa Falsafia yo yote ile ya maisha yaliyo mazuri kuliko yale yanayofuatwa na serikali. Maimamu wa ukoo wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w)walikuwa ni mifano halisi ya mafundisho ya Mtume(s.a.w.w)ambayo yalipinga kabisa desturi za Waarabu, zilizothibitika au yo yote kati ya madhehebu zilizoamini aina yo yote ile ubora wa taifa au yo yote kati ya zana nyingi za kimataifa ambazo hubadilika kila siku kulingana na matakwa ya watawala.

Hivyo, kutaka kuyaondoa maisha ya Imamu lilikuwa jambo muhimu sana kwa kuendeleza maisha ya serikali kama ilivyokuwa kabla hivyo mwishowe walifikiria hivyo.

Imamu alifariki (kwa kupewa sumu na Mu'tamad) mnamo tarehe 8 Rabi-ul-Awwal (Mfunguo Sita) mwaka 260 Hijiriya. Alizikwa huko Samarrah (Iraq) karibu na kaburi la baba yake, ambako, licha ya hali mbaya msikiti wa kaburi hilo bado umesimame, ambao ni moja ya sehemu kadhaa zilizo takatifu kwa watu wote.

NYONGEZA

Mifano ya Maandishi na Hadithi za Imamu(a.s)

1. Jiepushe na kuwa pamoja na mjinga hata kama yu akutakiaye kila Ia kheri na usijiepushe na mtu mwenye hekima hata kama ni adui yako. Kwani mjinga atakuumiza uhitajipo msaada ambapo utu wa mtu mwenye hekima utamzuia kufanya jambo lililo chanzo cha uadui.

2. Waraka wake kwa watu wa Qum, Iran: Mwenyezi Mungu aliudhihirisha wema wake kwa viumbe wake kwa kumleta Mtume wake Muhammad(s.a.w.w)na ahadi zake na maonyo yake na kakubarikini kwa Rehema zake kwa kukuwezesheni mkubali dini yake ya kweli na kukutukuzeni kwa kukuangazeni na akapanda mbegu ya imani katika mioyo ya wahenga wenu na kuwabariki wale watu miongoni mwenu ambao wanaishi maisha marefu na kawabariki kwa kuwepo kwa Dhuria wa Mtume wake(a.s)kuwa ndiyo viongozi wao.

Hivyo, wale waifuatao njia ya Haki watafaulu na kufaidi yale matunda waliyochuma kabla.Tunastarehe kwa sababu ya maarifa yenu mazuri na uhusiano wetu ni wa kuaminika. Shikaneni na amri zile ambazo wahenga wetu waliwapa vijana wenu na muwe na uhakika na zile ambazo vijana wetu waliwaahidi baba zenu. Mwenyezi Mungu awabarikini nyote.

3. Barua yake kwa Bwana Ibn Babawaihi Qummi: Ewe Hasan bin Ali bin Husain bin Babawaihi Al-Qummi, kuwa mvumilivu ili kungojea nyakati nzuri. Marafiki zetu wataendelea kuwepo kila wakati katika hali hii ya hatari mpaka aje mwanangu ambaye Mtukufu Mtume wa Mungu(s.a.w.w)alimbashiri kuwa ataijaza dunia kwa haki na usawa kama vile ambavyo ingelijaa mateso na dhuluma.

Hivyo, Ewe Sheikh, muwe wavumilivu wewe mwenyewe na wale marafiki zetu wote. Mwenyezi Mungu humpa hii dunia yake ye yote yule amuonaye kuwa anafaa katika viumbe wake. Na hakika mwishilizo mwema utakuwa na wale wamchao Mwenyezi Mungu. Amani ya Mwenyezi Mungu na Baraka zake na ziwe juu yako na juu ya marafiki zetu. Neema Zake na ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad(s.a.w.w)na Dhuria wake(a.s).