Sababu za Kuwepo na Kuanguka kwa Tamaduni Kwa Mtazamo wa Quran -2

 

SEHEMU YA KWANZA

Nini maana ya tamaduni, na je neno (tamaduni) hutumika mahala gani?

Katika kuelezea maana halisi ya neno "tamaduni” kumekuwa na kauli na rai mbalimbali ambazo zote zina lengo moja la kuweza kubainisha na kuweka sawa maana halisi ya neno hili. Na hapa tutajaribu kuleta baadhi ya kauli na rai hizo, kisha tuone ni kitu gani ambacho kinalengwa na kauli na rai hizo kwa pamoja.

MAANA YA KWANZA

 Baadhi ya wataalamu wa masuala yanayohusiana na tamaduni, wamejaribu kuelezea maana ya neno "tamaduni” kuwa ni : namna na jinsi ambavyo mwanadamu anakabiliana na maisha katika mazingira yake.

Kwa maana ya kwamba kunakuwa na mambo matatu muhimu katika maana hii, kwanza na mwanadamu na kisha ni mazingira na mwisho kabisa ni maisha anayoishi na namna ambavyo anakabiliana na kila jambo linalojitokeza katika maisha hayo. Sasa njia na namna ambazo anazitumia kukabiliana na changamoto au maisha yake kwa ujumla ndio huitwa tamaduni. Na kitu cha muhimu katika maana hii ni namna ambayo hutumika katika kukabiliana na maisha husika.

 

 

MAANA YA PILI

Wataalamu wengine wa maswala ya kijamii na tamaduni husika kwa ujumla, wanajaribu kuelezea maana ya tamaduni kwa kusema: ni mkusanyiko wa watu maalumu na ambao huishi katika mazingira maalumu huku wakiwa ni wenye kuendelea katika sekta ya uandishi. Kwa maana ya kwamba ili kuwe na tamaduni basi ni lazima kwanza kupatikane watu maalumu, na watu hawa wawe ni wenye kuishi katika mfumo maalumu, na kisha ni lazima watu hawa wawe ni wenye kuendelea katika sekta ya uandishi, kwa maana ya kwamba bila ya kuwa na mwendelezo katika nyanja ya uandishi basi hakuwezi kuwa na tamaduni.

 

MAANA YA TATU

Wataalamu waliokuja na maana hii, hawakuwa mbali sana na wale waliokuja na maana ya tatu kwamba, ni lazima kuwe na watu maalumu ambao wanaishi katika mazingira maalumu, na wawe ni wenye kuendelea katika sekta ya uandishi, ila tu wataalamu hawa wamekuja na kitu cha ziada ambacho ni: ili iwe ni tamaduni, basi ni lazima watu hawa maalumu wawe ni wenye elimu au ujuzi kuhusiana na watu waliopita pamja na historia zao.

Kwa maana ya kwamba sawa wanatakiwa wawe ni wajuzi katika sekta ya uandishi, lakini ujuzi huu wanautumia wapi? Moja ya sehemu husika au moja ya sehemu zinazotumia ujuzi huo ni kuweza kunakili na kudhibiti taarifa muhimu za watu waliopita pamoja na jinsi walivyokuwa wakiishi au kukabiliana na maisha katika sehemu yao.

Kwa maana hii basi, kitu cha muhimu zaidi ni kwamba watu hawa ni lazima wawe na ujuzi na elimu ya kuhusiana na watu waliokuwa kabla yao, wao na jinsi walivyokuwa wakiishi.

MAANA YA NNE

Hii ni maana ambayo imekuja kuletwa na wataalamu wa maswala ya lugha na kisha kuweza kuitumia kama maana sahihi ya neno "tamaduni”.

Ambapo wataalamu hawa wanatuambia kuwa tamaduni ni neno lenye asili ya Kiarabu ambalo ni "مدن” "madana” likiwa na maana ya "aliishi sehemu fulani”, kwa hiyo neno "tamaduni” linakuwa na maana ya "kuishi katika sehemu fulani” bila ya kuwa na sharti wala kitu cha ziada ili kuweza kuleta maana ya neno hili kama ambavyo wataalamu waliokuja na maana za juu wameashiria.  na kutokana na maana hii ndipo wakaja na maana ya neno "tamaduni” kuwa ni kitendo cha mwanadamu kuwa ni mwenye kuishi katika mazingira fulani.

Sasa hizi zote ni maana ambazo wataalamu wa maswala ya tamaduni na lugha kwa ujumla wanajaribu kutueleza ili tufahamu maana ya neno  "tamaduni”. Lakini kama tutakuwa tumezingatia maana zote hizo ambazo tumezileta hapo juu, bila shaka tutakuwa tumegundua kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo tunaweza kuyakusanya pamoja, na hii ni kutokana kwamba mambo hayo yote japokuwa yameletwa na wataalamu mbalimbali, lakini kwa pamoja yanalenga maana moja. Kwa mfano tumeweza kushuhudia katika maana zote kwamba:

Moja: tamaduni ni lazima wawe watu ndio wanahusika na sio viumbe wengine.

Mbili: watu hawa ni lazima wawe wanaishi katika mazingira maalumu yanayofanana.

Tatu: watu hawa ni lazima wawe na uelewa, na uelewa huu haijalishi na kuhusiana na nini, inaweza kuwa jinsi wao wenyewe wanavyoishi, au inaweza kuwa ni uelewa juu ya watu waliokuwa kabla yao, Cha muhimu ni kwamba watu hawa wana uelewa.

Na hapa ndipo tunafikia katika hatua ya kusema kwamba neno "tamaduni” maana yake ni: mkusanyiko wa watu fulani wanaoishi katika mazingira fulani wakiwa na uelewa wa kila jambo wanalolisimamia. Na kwa maana hii tunakuwa tumefikia hatua fulani katika kuelezea maana ya tamaduni na pia kuweza kutambua kwamba neno hili hutumika mahala gani.

Itaendelea.....