Sababu za Kuwepo na Kuanguka kwa Tamaduni Kwa Mtazamo wa Quran -3

SEHEMU YA PILI

SABABU ZINAZOPELEKEA KUZALIKA KWA TAMADUNI

Baada ya kuelezea na kubainisha rai mbalimbali juu ya maana halisi ya neno "tamaduni” sasa tujaribu kwa pamoja kuweza kudodosa na kuchunguza sababu zinaopelekea kuzalika kwa tamaduni hiyo. Na hapa pia tutakuja na baadhi ya rai na mitazamo ya wataalamu katika kubainisha sababu hizo.

"LUGHA”

Baadhi ya wataalamu wa maswala ya tamaduni, wanajaribu kutueleza kwamba sababu ya msingi katika kapatikana kwa tamaduni yoyote ile ni "lugha”, yaani namna ambavyo idadi ile maalumu ya watu wanaoishi katika mazingira fulani, wanaweza kufahamiana na kufikishiana yale wanayokuwa nayo kwa njia maalumu ambayo inakuwa inajulikana na kila mmoja katika idadi ile.

Na hii ni kwa sababu endapo itakuwa katika watu maalumu hakuna njia ya wao kuweza kuwasilishiana wanayokuwa nayo, basi itakuwa vigumu kwao wao kuweza kuzalisha hata kitu kidogo baina yao, sasa watawezaje kuzalisha jambo kubwa ambalo ndilo litakalowatambulisha kwamba wao wanaishi katika mfumo maalumu. Kwa hiyo kwa maana na mtazamo wa wataalamu hawa ni kwamba lugha ina nafasi kubwa sana katika kuzalisha tamaduni yoyote ile.

Angalizo

Kwa mtazamo wa haraka tu katika maneno na rai ya wataalamu hawa tunaweza kufikia katika natija ya kwamba, wanataka kutuambia kwamba lugha ndio sababu ya kuzalika kwa tamaduni, naam, hakuna ambaye atakataa swala hili, lakini inawezekana tusiafikiane kwa anuani ya kwamba lugha ndio sababu pekee ya kuzalika kwa tamaduni. Na hii ni kwa sababu ifuatayo:

Kama utakuwa ni mwenye kupambanua mambo kutoka katika asili yake, bila shaka utafikia katika natija ya kwamba kabla ya mwanadamu huyu kuamua kutumia lugha ili kufikisha anayowaza, bila shaka anakuwa na kitu ambacho anakiwaza kwanza, kisha ndio anataka kukifikisha. Sasa tujiulize ni kwa sababu gani mwanadamu huyu anakuwa na hamu ya kufikisha mambo anayowaza? Na je kama asingalikuwa na mambo haya bado lugha ingekuwa na nafasi katika kuendeleza tamaduni?. Haya maswali endapo tutayajibu ndio tutaweza kujua kwamba ni kitu gani ambacho ndio asili hasa ya kuzalika kwa tamaduni. Na majibu kamili ya maswali haya yatakuja katika kubainisha rai sahihi ya sababu ya kupatikana kwa tamaduni hivi karibuni.

"BIASHARA NA VIWANDA”

Huu ni mtazamo wa wataalamu wengi sana wa Magharibi, ambao nao katika kubainisha sababu ya msingi ya kupatikana na kuzalika kwa tamaduni basi viwanda na biashara ndio sababu ya hayo. Kwa maana ya kwamba katika swala zima la biashara, basi kwa upande ambao unahusika na kutoa bidhaa bila shaka utakuwa ni upande ambao unafahamu angalau kwa watu maalumu namna ya kutengeneza malighafi husika, na bila shaka kabla ya kutengeneza malighafi ile basi watakuwa ni watu ambao wanaendana kimtazamo na hata kinamna ambavyo wanaishi katika mazingira mazima ya kuandaa malighafi ile, sasa hapa katika kuendana ndipo ambapo inazalika tamaduni. Na kama ambavyo pia upande wa pili ambao unahusika na swala zima la ununuzi nao utaweza kutambua aina ya maisha ambayo wanaishi wale ambao wanawaletea malighafi zile, na kwa njia hii basi utamaduni unazalika na unapatikana.

"KILIMO”

Hii pia ni rai nyingine katika kuelezea sababu ya kupatikana kwa tamaduni, ambao wao huona kwamba swala zima la kilimo ndio linachukua nafasi hiyo kutokana na mchango wake. Na hii ni kwa sababu ya kwamba, kutoka na mfumo wa kilimo ulivyo ni vigumu sana kukuta kwamba ni mtu mmoja ndio anahusika na jambo hilo katika mkusanyiko wa watu zaidi ya mmoja, sasa jinsi wanavyotumia njia zao katika kufanikisha kilimo chao, au katika kukabiliana na changamoto za kilimo, ndipo ambapo kuna sura mpya inapatikana, nayo ni sura ya kwamba watu hawa wanafanya jambo hili linapotokea jambo hili, na hapo tamaduni inakuwa inazaliwa.

Angalizo

Baada ya kusoma na kuzichunguza rai mbili za mwisho tunakuta kwamba ndani yake kuna tatizo lilelile ambalo tulikutana nalo wakati tunaiangalia rai ya kwanza, nalo ni tatizo la kwamba kitu ambacho sio sababu ya msingi ndio tunakifanya kuwa ni sababu ya msingi katika jambo fulani, na haya ni makosa. Hebu angalia kwa makini, unaanzaje kusema kwamba kilimo au biashara ndio sababu ya kupatikana kwa tamaduni? Kama itakuwa kwa namna hii basi kila kitu kinaweza kuwa ni sababu ya kupatikana kwa tamaduni, na mwisho wa siku kila mmoja akawa na haki ya kusema kwamba hiki ndio sababu ya kuzalika kwa tamaduni maana kina mchango katika hilo. Ni lazima tuweze kutambua kwamba sisi hapa hatupo katika maudhui ya kubainisha kwamba kitu hiki kina mchango katika kupatikana kwa tamaduni au la, bali tupo katika hali ya kubainisha kwamba ni ipi sababu ya asili na msingi ya kupatikana kwa tamaduni, kwa hiyo inakuwa haina maana kuleta na kuorodhesha kila kitu ambacho kinakuwa na mchango katika hilo.

Hebu angalia mambo kama kilimo na biashara, ni mambo ambayo yanakuja katika akili ya mwanadamu baada ya kuwa kuna jambo ambalo limetangulia katika akili yake au nafsi na mawazo yake, na laiti kama asingalikuwa na mambo hayo basi mwanadamu huyu usingalimuona anahangaika kulima wala kufanya biashara. Sasa je ni mambo gani hayo? Hili ndilo swali la msingi ambalo endapo tutapata jibu lake basi tutakuwa tumefahamu ni ipi sababu ya msingi ya kupatikana kwa tamaduni. Na mwisho wa siku tutakuwa tumejua kwamba mambo mengine yote ni mambo ambayo yanakuja baada ya kupatikana kwa jambo hili.

Itaendelea....

Sh Abdul Razak Bilal.