Kumjua Mwenyezi Mungu Na Kutanua Maarifa

Kutaka Kumjua Mwenyezi Mungu ni sababu ya kuendelea kimaarifa

Jaribu kuwaza kwamba kuna rafiki yako ambaye ametoka safari na amekuletea kitabu kama zawadi, na akajaribu kukusifia kwa kukwambia kwamba kitabu hiki ni kizuri mno kwa sababu tu mtunzi wake ni katika watunzi mashuhuri na makini mno. Je ni hali gani ambayo utakuwa unayo wakati unasoma kitabu kile? Bila shaka licha ya kuwa na shauku kubwa juu ya kukisoma kwa haraka, pia utakuwa ni mwenye kuwa na umakini mkubwa mno katika usomaji wako ili tu kusije kukawa na nukta ya muhimu ndani yake na wewe ukaiacha.

Sasa jaribu pia kufikiria kwamba umeletewa kitabu ambacho unaambiwa kabisa kwamba kitabu hiki ni kizuri tu kwa nje, lakini mtunzi wake sio katika watu mahiri wala wenye elimu kubwa ya utunzi, bila shaka utajikuta kwamba ni mwenye kusoma kitabu kile kwa juujuu pia, na hata kama itatokea kuna nukta ambayo hujaelewa basi mapungufu yote yatarejea kwa mtunzi na utaona kwamba yeye ndiye aliyekosea katika kubainisha nukta ile.

Sasa hali hizo mbili ndizo hali ambazo tunazikuta pale ambapo tunarejea na kuutazama ulimwengu huu, kwani watu wote wanapouangalia jinsi ulivyoumbwa, viumbe vya aina mbalimbali, mipangilio iliyopo baina yake, wanafikia katika natija ya kwamba ulimwengu ni sawa na kitabu kimoja kikubwa sana ambacho kimetungwa na mtunzi mahiri mno. Japokuwa watu hutofautiana kunako huyu mtunzi wa kitabu hiki kikubwa, kuna ambao husema kwamba ni Mwenyezi Mungu, na hawa ni wale ambao wana amini ya kwamba haiwezekani mambo kama haya yakaja yenyewe bila ya kuwa na mwenye kuyapangilia. Na kuna ambao husema kwamba ni Tabia ya kimaumbile (yaani vyenyewe vimejipanga).

Lakini jambo la muhimu ambalo nataka kuliashiria hapa ni kwamba, pamoja na kwamba watu hawa wametofautiana katika natija ya kwamba ni nani ndie mtunzi wa kitabu hiki (ulimwengu), tunakuta kwamba wote kabla ya kufikia natija hiyo walikuwa na kitu ambacho kimewasukuma mpaka wakaitafuta natija hii, na kitu hicho ni pale walipouangalia ulimwengu na kutaka kujua kilichouweka ulimwengu huu, na kutokana na msukumo huu wa kutaka kujua kilichoweka ulimwengu huu, wakaweza kuongeza maarifa yao kwani walijikuta wakisoma kwa umakini kila nukta na kila jambo kunako ulimwengu huu.

Na ndio maana tunasema kwamba, kumtafuta muumba huongeza maarifa ya mwanadamu, hivyo mbali na kwamba tunafikia katika kumjua mola wetu pia tunakuwa ni wenye kuongeza maarifa yetu na kupanua upeo wetu.