Sababu za Kuwepo na Kuanguka kwa Tamaduni Kwa Mtazamo wa Quran -6

(1)KUKUFURU NEEMA ZA MWENYEZI MUNGU (SWT)

Kwa sababu hapo mwanzoni tulijaribu kuelezea kwamba mwanadamu kama mwanadamu ana maumbile ya kwamba siku zote anataka kuwa katika hali ya mkusanyiko ambao utafikia katika ukamilifu, na kuashiria kwamba sababu ya kudhihiri tamaduni ipo ndani ya mwanadamu basi na hapa ni lazima tuweze kutambua kwamba sababu ya kuanguka tamaduni ile pia ipo ndani ya mwanadamu mwenyewe. Na moja ya nyakati ambazo mwanadamu anaangukia katika shimo la kupoteza tamaduni zake ni pale ambapo atakuwa ni mwenye kukufuru na kutoshukuru neema za Mwenyezi Mungu (swt). Moja ya mifano ambayo ni dhahiri katika jambo hili, ni kadhia nzima ya wana wa Israel pale ambapo Mwenyezi Mungu alikuwa amewaneemesha neema mbalimbali, na kutokana na neema hizo tunaambiwa kwamba walikuwa ni kama watoto waliokusanywa katika hema moja, jinsi walivyokuwa wakiishi kwa umoja na kuelewana, lakini walipoanza tu kukufuru neema walizopewa basi ndipo walipoanza kupoteza tamaduni zao na hatimaye kuweza kutawaliwa na watawala wa kibabe mfano wa Firauni. Na hakukuwa na kosa kubwa ambalo walifanya wana wa Israel tofauti na kwamba kwanza walitoka katika msingi wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa kuanza kuabudu masanamu na mengineyo.

Miongoni mwa tamaduni nyengine ambazo Quran inaziashiria kwamba nayo ilianguka ni ile tamaduni na "saba” ambayo pia ilikuwa ni matokeo ya kukufuru na kutoshukuru neema za muumba wao.

(2)DHULMA, KIBURI, NA KUPINGA DALILI ZA MWENYEZI MUNGU

Quran katika kuelezea pia sababu za kuanguka kwa tamaduni inatuambia kwamba, dhulma, kiburi na hata kuwafanyia mzaha wale ambao ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu pia ni sababu katika kuanguka tamaduni.

Na mfano wa dhahiri ambao inatuletea ni kisa kizima cha nabii Nuhu (as) na watu wake, jinsi gani walivyokuwa wakimdharau na kumfanyia mzaha, lakini mwisho wa siku wao ndio ambao walipoteza mwelekeo wa maisha yao na tamaduni yao kwa ujumla.

(3)KUFUATA BILA YA KUWA NA UELEWA

Hii ni miongoni mwa sababu nyengine ambayo pia hupelekea kuanguka kwa tamaduni, ni pale ambapo mwanadamu anakuwa katika hali ya kufuata kila ambacho anakiona bila ya kuwa na uelewa katika hilo, mwisho wa siku anajikuta ameangamia bila ya kujua sababu yake ni nini, maana huwezi kuiga kitu ambacho hujui uhalisia wake ni upi.

Quran inasema kuhusiana na hili :

وقالوا ربنا إنا أطعنا سادتنا وكبراءنا فأضلونا السبيل

"... na watasema ewe mola wetu, hakika sisi tuliwatii wakubwa wetu na kuwafuata na wao sasa wametupoteza...”[1]

Miongoni mwa mambo ambayo Quran na dini ya Kiislamu kwa ujumla vimejaribu kupiga vita sana na hali ya kufuata katika kila jambo bila ya kuwa na uelewa ndani yake, bila kujali ni nani ambaye anakuambia wewe ufanye jambo lile. Kwani mwisho wa siku kila mtu ataulizwa kutokana na uelewa wake kuhusu jambo lile, sasa cha ajabu leo hii unakuta mtu mpaka katika maswala yanayoambata na misingi muhimu katika dini yake bado anataka aambiwe na mkuu wake kwamba fanya hivi au la, haya ni makosa makubwa mno kwani pia hupelekea katika kupoteza tamaduni kama ambavyo Quran inatuzindua.

(4)KHIYANA NA UDANGANYIFU

Moja ya sababu ambazo Quran inatutajia katika swala zima la kuanguka kwa tamaduni, ni khiyana na udanganyifu katika mambo, ambapo endapo wanadamu wanakuwa ni wenye kupambika na sifa kama hizi basi tamaduni zao zinakuwa katika hatari ya kupotea na kuanguka.

Mfano mkubwa ambao inatupatia Quran tukufu ni umma wa watu Madyan, ambao walikuwa ni maarufu sana kwa sifa hizi za udanganyifu katika biashara zao, na hiyo ikawa sababu y awao kuangamia na tamaduni zao kwa ujumla.

(5)KUJIONA NA KUJIPENDELEA

Pia miongoni mwa sababu za kuanguka kwa tamaduni ni kujikweza na kujiona na kujipendelea nafsi yako pasi na wengine, na miongoni mwa mifano iliyokuwa hai na ambayo Quran pia imeiashiria ni Wayahudi, jinsi gani wanasifika na sifa kama hii na jinsi gani imepelekea kupotea kwa tamaduni zao kwa ujumla.

Sasa hizi ni baadhi ya sababu ambazo zinapatikana katika Quran tukufu, ambazo zote tukiziangalia tutakuta ni kweli zinaendana na hali halisi ya kuanguka kwa tamaduni yoyote ile, kuanzia zile zilizopita na mpaka ambazo zitakuja kujipamba na sifa kama hizo. Na hapo ndipo tunapokuja kutambua kwamba kitabu hiki kitukufu kimekuja kwa lengo la uongofu wa tamaduni za wanadamu, kwani kimeanza kumtahadharisha na kisha kumpa maelekezo juu ya nini afanye ili tamaduni yake ibaki, au mambo gani akiyafanya basi tamaduni yake itapotea.

NATIJA NA HITIMISHO

Mwisho kabisa baada ya kuelezea hayo yote tunaweza kufikia katika baadhi ya nukta muhimu na ambazo ndizo tulikuwa tukiziangalia katika makala yetu hii, nazo ni kama ifuatavyo:

1. Mwanadamu pamoja na mazingira ni viungo muhimu sana katika kutengeneza jamii na tamaduni yoyote kwa ujumla.

2. Maana halisi ya tamaduni tunaweza kuipata kwa kuangalia neno lenyewe lina maana gani, na hapo haitakuwa na haja ya kuweka baadhi ya masharti yasiyokuwa ya muhimu katika kuelezea maana yake.

3. Sababu ya msingi kabisa katika kupatikana kwa tamaduni ni mwanadamu mwenyewe, kwa maana ya kwamba maumbile ya mwanadamu ndiyo ambayo yanamuhitajia kwamba awe na tamaduni, na ndio maana tukasema kwamba mwanadamu ni mwana tamaduni kwa maumbile. Na kwa msingi huu kila sababu ambayo imejaribu kutajwa na wa wataalamu inakuwa ni katika nafasi ya pili au ni katika mambo yanayopelekea pia lakini sio kwa anuani ya kwamba yenyewe ni mambo ya asili na msingi.

4. Sababu halisi ya kuanguka kwa tamaduni pia inapatikana kwa mwanadamu mwenyewe na mfumo wake wa maisha anaouchagua, ikiwa atachagua mfumo wa kumtii muumba wake basi tamaduni yake itakuwa ni yenye kudumu, na kama atakuwa ni mwenye kumkufuru pamoja na neema zake basi asitegemee tamaduni zake kudumu. Na hakuna sababu za msingi kabisa kuliko ambazo zimetajwa na Quran tukufu, kwani zenyewe zimeweza kwanza kuangalia umma zilizoita zilifanya mambo gani ambayo yalipelekea kupotea kwa tamaduni zao, na kisha ndio ikaja na misingi ambayo tumeitaja katika makala hii. Ama kuhusu sababu ambazo wataalamu wamejaribu kutaja kuwa ni sababu na asili ya kupotea kwa tamaduni, tumegundua kuwa sababu hizo zinakuwa ni athari za kuharibika kwa tamaduni, na si sababu ya kuharibika kwa tamaduni yenyewe, kwani sisi tulikuwa katika mada ya kubainisha sababu za asili na msingi kabisa, na si athari.

Mwisho kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu (swt) ambaye amenipa uwezo wa kuweza kuandika haya ambayo nimefanikiwa kuyaandika, na kwa uwezo wake yawe ni katika ambayo yataweza kufaidisha na kunufaisha jamii yetu kwa ujumla, ili mwisho wa siku tuwe ni wenye kubakia katika tamaduni zetu na si wenye kuzipoteza kwa sababu tu ya kufuata ambayo yanapelekea huko. Kwani kuanguka kwa tamaduni bila shaka ni kuwa na mwisho mbaya kwa mwanadamu, kwa sababu kama tulivyoona kwamba hakuna tamaduni iliyoanguka ila itakuwa imeshikamana na mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu (swt).[1] Suratul ahzaab aya 67