Umuhimu wa Maswala ya Itikadi katika maneno ya Mtume na Maimamu (as)

SEHEMU YA PILI

KATIKA MANENO YA MAIMAMU

Endapo tutarejea na kuangalia maneno ya maimamu, basi tutakuta kwamba wao pia waliwekea umuhimu mno swala zima la itikadi, ima iwe kwa njia ya wao kuanza moja kwa moja kubainisha au hata wakati mwingine ni kwa njia ya kusahihisha pale wanapoona kwamba kuna makosa. Na kwa kuwa tumeona kwa mtume njia ya kwanza basi itakuwa vyema endapo tukaangalia njia ya pili kwa maimamu zetu ili tuweze kukamilisha njia zote mbili katika jambo hili.

Amepokea Swafwan bin Yahya kutoka kwa Kahiliy ambaye amesema "siku moja nilimwandikia Abul Hassan (imamu Ridha as) barua ambayo niliiambatanisha na dua nikisema : sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu kwa kiwango cha elimu yake”. Akanijibu kwa kusema "Usiseme kwa kiwango cha elimu yake, kwani elimu yake haina kiwango, bali sema kwa kiwango cha ridhaa yake...”[1]

Hakika riwaya hii kutoka kwa imamu Ridha (as) ni riwaya ambayo inatufungulia mlango wa uweza kuuliza, kwanini Imamu amemkataza sahaba wake kusema kwamba sifa za Mwenyezi Mungu ni kwa kiwango cha elimu yake na badala yake asema kwamba sifa zake ni kwa kiwango cha ridhaa yake?, kwani kuna tofauti gani baina ya elimu na ridhaa kihalisia mpaka ifae katika ridhaa na isifae katika elimu?.

Katika kujibu swala hili ni lazima tubainishe kwamba Imamu as alikuwa anataka kuashiria tofauti iliyopo baina ya sifa mbili (elimu na ridhaa), nayo ni kwamba sifa ya elimu ni katika sifa ambazo zinaambatana moja kwa moja na dhati ya Mwenyezi Mungu, yaani huwezi kupata uwili baina ya Mwenyezi Mungu na elimu kisha ukasema kwamba kuna Mungu na kuna elimu, bali ni kwamba Mungu ndiye elimu na hakuna mwachaniko baina yake na sifa ya elimu. Kwa mantiki hii basi endapo utasema kwamba elimu ya Mwenyezi Mungu ina mwisho ujue kabisa kwamba unakuwa unaashiria kwamba hata uwepo wake pia una mwisho, na hili ni swala ambalo kila Mwislamu hakubaliani nalo, hivyo ni kweli kwamba si sahihi kusema kwamba namsifu Mwenyezi Mungu kwa kadiri na kiwango cha elimu yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu hana kiwango.

Ama kuhusiana na sifa ya pili ambayo ni ridhaa ya Mwenyezi Mungu, tunafahamu katika maneno ya Imamu kwamba ni katika zile sifa ambazo si katika dhati ya Mwenyezi Mungu, kwa maana ya kwamba unaweza ukafikiria ridhaa ya Mwenyezi Mungu bila ya kumfikiria yeye mwenyewe, au pia ukamfikiria Mwenyezi Mungu bila ya kufikiria ridhaa yake. Ndio, kwani huoni kwamba kuna wakati mwingine unamfikiria Mwenyezi Mungu wakati ambao anakuwa amewakasirikia makafiri? Je unadhani wakati huo ridhaa inakuwa na nafasi kwake?, lakini haiwezekani hata wakati mmoja ukamfikiria Mwenyezi Mungu bila ya elimu yake, hii ni moja ya dalili kwamba ridhaa sio katika sifa zinazoambatana na dhati yake daima kama ilivyo kwa elimu. Ndio maana ikawa sahihi kusema kwamba unamsifu kwa kiwango cha ridhaa yake, kwa sababu ridhaa ina kiwango kweli.

Kwahiyo tunafikia katika natija ya kwamba maimamu pia walikuwa wapo katika jukumu la kuhakikisha kwamba swala la itikadi katika nyoyo za Waislamu linakuwa na thabiti tena lenye kuambatana na uelewa wa kile ambacho wanakiamini.

IMAMU ALLY AS

Amepokea imamu Sadiq as kwamba siku moja imamu Ally as aliulizwa "Je, mola wako anaweza kuingiza dunia katika yai bila ya yai kupasuka wala dunia kupungua ukubwa wake?”, imamu akajibu kwa kusema "Hakika Mwenyezi Mungu hashindwi na jambo, isipokuwa ulilolisema haliwezekani”.[2]

Hakika riwaya hii pia inatuwekea wazi kwamba imamu Ally alikuwa ni katika ambao wapo mstari wa mbele katika kujibu na kurekebisha maswala mbalimbali ya kiitikadi, na hapa ilikuwa ni kwa njia ya kujibu baadhi ya maswali ambayo walikuwa wakimuuliza juu ya muumba wa ulimwengu. Na msingi wa swali hili ni pale ambapo dini ya Kiislamu imekuja na kunadi kwamba mola wake ni muweza wa kila kitu na hakuna ashindwalo, sasa je, ana uwezo wa kuingiza dunia katika yai na kila kitu kitu kikabakia katika hali yake?, yaani yai liwe dogo vilevile na dunia iwe kubwa hivihivi?.

Jibu ambalo tunaona imamu amekuja nalo ndio msingi wa itikadi, kwanza kabisa ameanza kuashiria kwamba Mwenyezi Mungu hashindwi na jambo, akiwa na maana kwamba yale ambayo Uislamu unafundisha ni kweli, ila akaja akaashiria nukta nyingine kuhusiana na swali lile ya kwamba hilo uliloniuliza ndio haliwezekani. Nini maana ya haya maneno? Kama hashindwi kitu kwanini hili lishindikane?.

Hapa ndipo tunapofikia hatua ya kusema kwamba imamu amebainisha mambo mawili ya muhimu sana katika ulimwengu wa kuwezekana au kutowezekana kwa vitu, na mambo yenyewe ni:

1. Ili jambo litokee ni lazima lenyewe liwe na uwezekano wa kutokea.

Tuchukue mfano kunako maswala ya hesabu, sote tunajua kwamba moja ongeza moja ni mbili, na wala si tatu, kwa sababu yenyewe kama yenyewe inasema kwamba siwezi kuwa tatu endapo utaniongeza na moja. Hivyo hata ukimchukua mtaalamu wa mambo ya hesabu na kumwambia kwamba kwa utaalamu wake afanye moja ongeza moja iwe tatu hatoweza kufanya hivyo. Lakini je, unaweza kusema kwamba huyu mtaalamu hajui kitu? Bila shaka huwezi kusema hivyo, kwa sababu kanuni iliyopo ndio kizuizi na si kwamba yeye hajui, kwa maana ya kwamba moja ongeza moja haiwezekani kuwa tatu.

2. Uwezo huambatana na mambo yanayowezekana

Hii ni natija ya jambo la kwanza, ikiwa na maana kwamba kama unataka kumpima mtu kwamba ana uwezo wa jambo fulani ni lazima lile jambo liwe na asili ya kuwezekana, kama inawezekana kilo 5 kuinuka kisha mtu akashindwa kuinua hapa tuna haki ya kumwita yule mtu kwamba hana uwezo, lakini kama haiwezekani pakacha kujaa maji, kisha mtu akashindwa kujaza maji si busara kumwambia kwamba ameshindwa.

Vivyo hivyo kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na kwamba ana uwezo wa kila jambo, lakini ni lazima ifahamike kwamba uwezo wake huambatana na yale ambayo yanawezekana, je, yai kama yai lina uwezo wa kuipokea dunia na ukubwa wake?, kama hapana, kwanini unasema kwamba Mwenyezi Mungu ndie aliyeshindwa?. Ndio maana imamu akasema "hili uliloniuliza ndio haliwezekani” hakusema kwamba Mwenyezi Mungu haliwezi, ikiwa anaashiria kwamba kutowezekana na katika asili ya jambo hilo, na si busara kuhukumu kwamba mola hawezi katika sura hii.

Hapa pia tunaona jinsi gani imamu ameweza kujenga msingi wa itikadi kwa Waislamu, kwani huenda tungetetereka na kusema kwamba mola wetu kuna ambayo hayawezi.

Wasalaam alaykum

Sh Abdul Razaq Rashid.[1] Usul kafi juz 1 uk 107

[2] Biharul anwar juz 43 uk 21