bayyinaat

Published time: 29 ,January ,2024      09:08:37
Nasaha ya Uislamu kwa Anayetaka Kuoa (sehemu ya 1)
Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu chake kitukufu; وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanao fikiri. Bwana Mtume naye pia (s.a.w.a) anasema: النِّکَاحُ سُنَّتِی فَمَنْ رَغِبَ عَنْ سُنَّتِی فَلَیْسَ مِنِّی ‏ “Kuoa ni moja katika sunna zangu na atakaye acha sunna yangu sio miongoni mwangu.”
News ID: 451

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu

Nasaha ya Uislamu kwa Anayetaka Kuoa

Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu chake kitukufu;

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي

ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ [1]

Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanao fikiri.

Bwana Mtume naye pia (s.a.w.a) anasema:

النِّکَاحُ سُنَّتِی فَمَنْ رَغِبَ عَنْ سُنَّتِی فَلَیْسَ مِنِّی[2]

"Kuoa ni moja katika sunna zangu na atakaye acha sunna yangu sio miongoni mwangu.”

Kama tunavyoona katika aya na hadithi hapo juu ni kuwa suala la kuoa katika Uislamu ni moja katika vitu vilivyopigiwa debe mno. Hata hivyo, moja katika sifa nzuri ya dini tukufu ya Uislamu ni kuwa huwa haiachi mfuasi wake bila muongozo. Yaani hakuna kitu au swali lolote utakalo kuwa nalo ambalo utakosa jibu lake katika dini yetu. Na hii ni moja katika sifa za kutofautisha dini yetu na dini zote zilizobaki. Kuusia watu kuoa haikutosha, bali dini yetu vilevile imetoa maelezo kabambe panapo hili suala muhimu, kuanzia pale mja anapotaka kuoa, atakapooa na hata maisha yake katika ndoa yaweje.

Leo hii katika makala yetu, tutaangazia kinaga ubaga vipengele vya kutilia maanani kwa mja anayetaka kuingia katika ulimwengu wa ndoa. Hivyo basi, ewe mpenzi msomaji, iwapo wewe ni mvulana au binti, baba au mama, kaka au dada, mjomba au shangazi, babu au bibi, vipengele vifuatavyo vinakuhusu kwa njia moja au nyingine. Iwapo mtu atakufuata kuomba nasaha na ushauri kwa ajili ya ndoa, basi ifuatayo ndio ushauri ambao utampa kwa mujibu wa dini yetu tukufu. Na iwapo ni wewe mwenyewe unataka kuingia katika maisha ya ndoa, basi utachunguza vipengele vifuatavyo katika nafsi yako kabla hujachukua hatua yoyote ile ya kuanza maisha ya ndoa. Kwa hivyo mfumo wetu katika makala hii ni kukuwezesha ewe mpenzi msomaji, uwe na maarifa ya kuweza kutoa ushauri kwa anayetaka kuoa au kuolewa. Kabla hujamshauri, hivi ndivyo vipengele utakavyotumia ili umpe ushauri mwanana wenye kuzaa matunda mema:

1. Chunguza upeo wa akili wa anayetaka kuoa

Hakuna nguvu kubwa alopewa mwanadamu kama akili. Zipo hadithi chungu nzima kuhusu akili na moja katika hadithi hizi inasema kuwa Mola humruzuku mja wake akili katika hatua tatu tofauti na kutokana na hili, tunakuwa na makundi matatu ya watu. Kundi la kwanza ni la wale ambao huruzukiwa riziki hii (akili) pale ambapo wazazi wao wanapokutana kijinsia. Watu walioruzukiwa akili katika hatua hii huwa ni wepesi sana wa kuelewa na unapozungumza nao, huwa wanaelewa mazungumzo yako hata kabla hujamaliza. Bila shaka utakuwa umekutana na watu wa kundi hili.

Kundi la pili ni wale ambao hujaaliwa riziki hii katika tumbo ya mama zao. Watu wa kundi hili ni wale ambao huelewa mambo baada ya kuambiwa mara moja na wala msemaji hahitaji kukariri maneno yake. Kundi la tatu ni la wale ambao hujaaliwa riziki hii wanapozaliwa. Hili ni kundi la watu ambao mnenaji anahitaji kukariri mazungumzo yake ili aeleweke. Yaani kwa kusema mara moja haitoshi. Kwa ibara nyingine ni kuwa usiporudia uliyosema, basi watu wa kundi hili hawatakuelewa na iwapo ikatokea amekuelewa bila kurudia, kuna uwezekano wa kukuelewa kimakosa! Ewe mpenzi msomaji, hadi hapa, je wewe unahisi upo katika kundi lipi?!

Kwa hiyo nukta ya kwanza ambayo mwenye kutoa ushauri anapaswa kuzingatia ni hii hapa. Je msemezwa wake yupo katika kundi lipi la watu? Je ni mwenye kuelewa upesi, au ni lazima mazungumzo yakaririwe ili aelewe? Hivyo basi, anayetaka kuoa lazima awe na uwezo wa kudadavua na kung’amua mambo maana ndoa haitaki mchezo, bali akili lazima ifanye kazi tena kazi haswa!

Njia ya pili ambayo maimamu wanatuusia katika kujua upeo wa akili wa mtu ni kumuambia kitu ambacho haikubaliki kiakili kisha uone kama ataafiki suala hilo au atapinga. Ukiona anaafiki jambo hilo basi tambua kuwa upeo wake ni mdogo, lakini ukiona kuwa amepinga jambo hilo basi tambua kuwa upeo wake ni mkubwa au mzuri. Baada ya kupima na kutambua upeo wa akili wa muomba ushauri, basi tunakwenda katika hatua ya pili.

2. Chunguza ukomavu wake wa kijamii

Ukomavu wa kijamii[3] ni hatua ya mtu kufikia uwezo wa kujisimamia mwenyewe, kuwa huru wa kufanya maamuzi, kujitambua na kutambua watu wengine na kuanzisha uhusiano unaolingana nao. Ukomavu ni uwezo wa kukabiliana na mazingira kwa njia inayofaa. Na hili ni jambo la kujifunza na wala sio kitu cha kurithi au asili ya mwanadamu. Vilevile, haliamuliwi na umri wa mtu. Ukomavu pia unajumuisha kufahamu wakati na mahali sahihi pa kuwepo na kujua wakati wa kutenda ipasavyo, kulingana na mazingira na utamaduni wa jamii anayoishi mtu.

Sifa muhimu za mtu aliyekomaa kijamii ni kama zifuatazo:

1- Ni mtu aliyejisimamia na ana uwezo wa kuendesha maisha yake mwenyewe.

2- Ni mtu aliye tayari kutekeleza nyadhifa zake mbalimbali bila kusukumwa na mtu yeyote.

3- Ni mtu mwenye kuelewa hali za kimaisha kwa mfano kuna kufanikiwa na kufeli.

4- Ana mtazamo juu ya mustakabali wa maisha yake. Ni mtu mwenye mipango na malengo katika maisha. Sio mtu wa kukata tamaa katika maisha.

5-Ni mtu msamehevu na anakubali upungufu wake na wa watu wengine.

6-Ni mtu mwenye kufanya ushirikiano na wenzake na sio mtu wa kuamini kuwa yeye mwenyewe anajitosheleza katika kila kitu.

7-Ni mtu mwenye shukrani katika kila sehemu.

8-Ni mtu mwenye kukubali nasaha, kukosolewa na muongozo kutoka kwa watu wengine.

9-Ni mtu mwenye subira na mvumilivu anapokumbana na matatizo ya kimaisha.

10-Ni mtu mwenye tabia njema kwa watu wote.



[1] Suurat ar-Ruum: 21

[2] Jaamiu al-Akhbaar, uk. 101

[3] Social maturity

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: