bayyinaat

Published time: 03 ,December ,2017      18:13:06
na sehemu kama hizi ndizo zinazo mtofautisha mwanadamu na mnyama, Mwenyezi Mungu alipomuumba mwanadamu ha kumpa ukamilifu wote, bali alimpa sehemu ndogo kama kianzio cha kumfikisha kwenye huo ukamilifu, kwa lugha nyingine twaweza kusema kwamba alimpa rasilimali ndogo ya..........
News ID: 138
Assalam alaykum ndugu wasomaji wa makala hii, tumekutana tena ili kuendeleza yale mazuri ambayo yanapatikana katika makala zetu,kubwa ambalo tunalitoa katika makala hizi ni elimu na ndilo letu .katika makala yetu iliyopita  tulizungumzia  akili, na tuliona kwamba akili ni kifaa ambacho amepewa kila mwanadamu ili afikie maendeleo ya juu katika kila nyanja ya elimu, lakini kubwa zaidi aitumie kumtambua mola wake  aliyemuumba na baada ya hapo ajue halali na haramu.na kama huyu mwanadamu ataitumia vizuri atapata thawabu, na kama ataitumia vibaya ,malipo yake ni moto wa jahanamu. na sasa tunataka kuiangalia mada nyingine ambayo ni matunda ya kuwa na akili, nayo si nyingine isipokuwa ni kufikiri( kutafakari).
KUFIKIRI NI NINI?
Ukiangalia katika kamusi nyingi za Kiarabu, wanasema kwamba kufikiri ni kutumia akili katika jambo fulani, au kuwa na mazingatio katika jambo fulani. kwa maana hii, kufikiri ni natija ya kuwa na akili kama kifaa cha kuanzia na kukupelekea kufikiria.
Na Mwenyezi Mungu [swt] amehimiza kufikiria na kuzingatia katika sehemu mbalimbali na mambo mbalimbali .kwa kusema :SEMA,MIMI NAKUNASIHINI TU KWA JAMBO KUWA,MSIMAME KWA AJILI YA MWENYEZI MUNGU,WAWILI WAWILI NA MMOJA MMOJA,KISHA MFIKIRI.(suratu sabai aya ya 46). amewasifu watu ambao mara nyingi ni wenye kufikiri katika kitabu chake kitukufu. sisi tunasema kwamba Quran ni kitabu ambacho kinatoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo basi hakina makosa yoyote ndani yake, Mwenyezi Mungu amekihifadhi tangu alipo kishusha kwa Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w)ili kiwe ni mwongozo kwa watu wote, lakini inabidi tutambue kwamba kitabu hiki hakiongozi mtu mjinga ambaye hana akili wala hafikirii, kwa hiyo Mwenyezi Mungu amekifanya kuwa ni uwanja wa kukitumia kwa kufikiria na kutadabari katika aya zake,hasa hasa yale ambayo yanaelezwa na Qur-an kwa uwazi kabisa, na kwa mantiki hii utapata faida mbili: ya kwanza ni faida ya kiroho, na tukisema faida ya kiroho, tunakusudia itikadi sahihi ya kumtambua na kumjua Mwenyezi Mungu mmoja. ya pili ni faida upande wa kimaada(yaani faida zote zinazoambatana na ulimwengu)mfano utajua mambo ya kisayansi, na ya kiuchumi na ya kihistoria n.k.
  na sehemu kama hizi ndizo zinazo mtofautisha mwanadamu na mnyama, Mwenyezi Mungu alipomuumba mwanadamu ha kumpa ukamilifu wote, bali alimpa sehemu ndogo kama kianzio cha kumfikisha kwenye huo ukamilifu, kwa lugha nyingine twaweza kusema kwamba alimpa rasilimali ndogo ya kuanzia, na kama ataitumia vizuri atafikia kilele cha hali ya juu cha ukamilifu.na rasilmali kubwa aliyopewa mwanadamu ni akili ambayo kama ataitumia vizuri atapata au atafikia faida ambazo tumezitaja hapo juu. lakini ukimchunguza mnyama Mwenyezi Mungu alimuumba na kumpa ukamilifu wake hauzidi wala haupungui, mfano ukamilifu wa nyuki ni kutengeneza asali awe mdogo au mkubwa ,kwa hiyo sekta yake ya ukamilifu ni moja hakuna zaidi ya hapo. lakini mwanadamu yeye anaweza kukamilika katika sekta mbalimbali kwa sharti aitumie akili kwa kufikiria. akikosa hata sekta moja atakuwa anazidiwa ubora na mnyama, na kama atakuwa na sekta moja atakuwa anafanana na mnyama .bali lazima mwanadamu aitumie ile rasilimali aliyopewa kwa kufikiria ili ajiimarishe na kufikia aina mbalimbali za maendeleo ya kidunia na akhera.
Mwenyezi Mungu anasema:" NA WANAOFIKIRI KATIKA UMBO LA MBINGU NA NCHI [WAKASEMA]MOLA WETU! HUKUVIUMBA HIVI BURE, BASI TUEPUSHE NA ADHABU YA MOTO." sura ya 3:191
   Mwenyezi Mungu ameumba kila kitu kwa mpangilio  mzuri usio na shaka! je umewahi kujiuliza juu ya uumbaaji huu? kama ndiyo je umewahi kuona mapungufu? jibu ni hapana!! ametakasika mola wa viumbe wote. pia mwenyezi mungu swt amesema: "JE HAWAZINGATII QURAN NA KAMA INGELITOKA KWA ASIEKUWA MWENYE ZIMUNGU, BILA SHAKA WANGEKUTA NDANI YAKE IKHITILAFU NYINGI." sura ya 4:82
Qur-an ni muujiza hakuna kiumbe yeyote ambaye anaweza kuleta mfano wake, na itaendelea kuwa muujiza mpaka itakaporudi kwa mwenyezi mungu (swt) tatizo tulilonalo sisi ni kutosoma Qur-an kwa mazingatio, ina maana tunaisoma Qur-an ima kwa sauti nzuri tu? au tunasikia Qur-an inasomwa kwa sauti nzuri, lakini hatufikirii zile aya zinazo somwa zinatuambia nini.
katika Qur-an kuna aya za maamrisho kama vile swala, swaum, zaka, khumsi, haji, amru bilmaarufi wa nahy anilmunkar (yaani kuamrisha mema na kukataza maovu),aya zinazotoa hukumu mbalimbali za adhabu kutokana na matendo mbalimbali yanayo fanywa na wanadamu pia aya zinazozungumzia neema mbalimbali kwa watu wanaofanya matendo mema. lakini sisi hatuzingatii wala hatufikirii juu ya aya hizo ,na ukosefu wa kufikiria na kuzingatia hupelekea kufanya mambo bila ya kujali matokeo .Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema: "fikirini katika alivyo viumba Mwenyezi Mungu, na wala msifikiri juu ya mwenyezi Mungu yukoje au yuko vipi? kwani hilo hamtaliweza, Mwenyezi Mungu ametakasika na hilo.
kisha Bwana Mtume (s.a.w.w) alisema :"yapeni macho yenu hadhi yake katika ibada ."masahaba wakamuuliza "ewe mjumbe wa mwenyezi mungu !, ni ipi hiyo hadhi ya ibada ? Mtume (s.a.w.w) alisema :ni kutazama katika mas’hafu ,na kufikiri katika aya unazozisoma, na kunyenyekea, katika maajabu yake ."
Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) yeye amesema :"zindua moyo wako kwa kufikiri, na usimamishe usiku mwili wako (kwa ibada) na mche mola wako.
kutokana na hadithi kama hizi ni wazi kuwa kila mtu analazimika kuwa ni mwenye kufikiri.
kufikiri kunamwelekeza mtu katika matendo mema na kuachana na matendo maovu.kheri zote zipo katika mambo matatu:
1. kutazama kwa mazingatio.
2. kunyamaza kwa mazingatio.
3. na kuzungumza kwa mazingatio.
Imam Jaafar Sadiq (a.s) amesema: "ubora wa ibada ni kufikiri katika vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu, na katika uwezo wake Mwenyezi Mungu." 
Imam Ridhwa (a.s) amesema :"haikuwa ibada ni wingi wa swala , na saumu , isipokua ibada ni kufikiri katika mambo ya Mwenyezi Mungu".
kutokana na hadithi hizi tunatakiwa tuwe na watu wenye kufikiri sana. kabla hujachukua uamuzi wa jambo lolote lile basi unatakiwa kufikiria jambo hilo. Ikiwa ni jema basi  lifanye  na kama si jema liache. 
             



LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: