bayyinaat

Published time: 03 ,December ,2017      18:17:19
Kuna aya tukufu na hadithi nyingi zinazohusu fadhila za akili. kwa mfano nitataja hadithi ya Imam Musa ibun Jaafar Al-kadhim(a.s)katika mambo ambayo alimuhusia sahaba wake Hisham Ibun Hakam,alimwambia:ewe Hisham kama mtu anataka kutajirika bila kuwa na mali,au kama anataka kuwa huru........
News ID: 139


Assalam alaykum ndugu wasomaji na wapenzi wa makala zetu, bila shaka mnaendelea kufaidika kwa kiwango cha hali ya juu. ila napenda kukupa ushauri ndugu yangu ukielimika usimfiche mwenzako kile ambacho umejaaliwa, hakikisha unamwelimisha hata yule ambaye hajabahatika kusoma makala zetu, kwani lengo ni kuweka wazi masiala za kielimu, itakuwa sio uungwana kuficha kile ambacho Allah amekupa katika elimu ,kwani mtu wa namna hii, Mungu anamlaani, na malaika wake, na analaaniwa na kila mwenye kulaani.na tuna hadithi maarufu ya Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w.)anasema :zaka ya elimu ni kuifundisha.

katika makala yetu iliyopita tulielezea umuhimu wa kufikiri na tuliona kwamba, kukaa na kufikiri ndiyo sababu ambayo, inamfikisha mwanadamu katika maendeleo makubwa, na katika sekta mbalimbali .tutaendelea na mada yetu ambayo inahusiana na akili na utukufu wa kufikiria.

ALAMA ZA UKAMILIFU WA AKILI NA UBORA WA AKILI.

Kuna aya tukufu na hadithi nyingi zinazohusu fadhila za akili. kwa mfano nitataja hadithi ya Imam Musa ibun Jaafar Al-kadhim(a.s)katika mambo ambayo alimuhusia sahaba wake Hisham Ibun Hakam,alimwambia:ewe Hisham kama mtu anataka kutajirika bila kuwa na mali,au kama anataka kuwa huru(asiwe na husda)na kuwa makini katika dini yake, basi amlilie Mola wake ili amkamilishe akili yake. akili yake mara tu itakapokamilika ,ataridhika na kutosheka na kiasi kidogo anachokipata cha mahitaji ya maisha yake. yoyote atakayetosheka kwa kiasi hicho kidogo cha mahitaji ya maisha, basi mtu huyo atakuwa ni tajiri. lakini kama mtu hatosheki na kiasi hicho kidogo cha mahitaji muhimu ya maisha yake, basi mtu huyo kamwe hataridhika wala hatotosheka na kamwe hatotajirika.

Hii ina maana ya kwamba kama mtu hatosheki,na akawa ni mbinafsi na mchoyo na mlafi, basi mtu huyo hatofikia hali ya kukinai na kutosheka.

KUKINAI NI ALAMA YA UKAMILIFU WA AKILI.

Katika hadithi nyingine imesimuliwa kwamba, Amirul-muuminina Ali bin Abi twalib (a.s)alisema: yoyote mwenye kukinai(kutosheka)ni mtukufu na mwenye kuheshimika, na mtu yoyote ambaye ni mbinafsi na asiyetosheka, basi mtu huyo ni dhalili.na akasema tena kukinai ni aina ya utajiri usiokwisha.

SIFA NA DALILI ZINAZOONYESHA UKAMILIFU WA AKILI.

Katika hadithi nyingine imesimuliwa kwamba Imam Musa Al-kadhim (a.s)alimwambia sahaba wake Hisham kwamba: ewe Hisham, Amirul-muuminina Ali (a.s) alikuwa akisema "Mungu hajapata kuabudiwa kwa njia nzuri na bora zaidi kuliko pale anapoabudiwa kwa akili, akili ya mtu haiwezi kukamilika mpaka pale atakapokuwa na tabia na mwenendo mwema" .pia Imam Swadiq (a.s) anasema: akili ni ule uwezo ambao kwao Mungu mwenye rehema huabudiwa na kwa uwezo huo pepo tukufu ya Mwenyezi Mungu hupatikana.

Hata hivyo sifa za mtu mwenye hekima na busara ni kutokana na akili iliyosalimika na vitendo viovu, kama kufuru na shirki. vile vile mtu huyo siku zote anatarajiwa kupiga hatua za kimaendeleo na kuwa mtu mzuri aliyekamilika. mtu huyo huepuka mazungumzo yasio na faida ,bali huzungumza lile ambalo linasitahiki kuzungumzwa. mtu mwenye akili na busara daima hachoki kujifunza.akili yake humlazimisha kutafuta elimu na maarifa ,kwa umakini hufanya juhudi kubwa kwa kusoma, na siku zote hujitahidi kutafuta maarifa mapya. mwenendo mwema humfikisha katika daraja la juu sana la kuheshimiwa. bila shaka ni dhahiri kwamba lengo la mwenye kutafuta maarifa lazima liwe ni kufikia utambuzi wa sifa tukufu za Mwenyezi Mungu na kupata radhi zake. asifanye juhudi hiyo ya kutafuta elimu, kwa ajili ya kutavuta fahari ya dunia na nafasi au vyeo vya kupita vya kidunia.

Tunasoma aya ya Qur-an tukufu kuhusu jambo hili: kwa hakika wanao muogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale tu wenye ujuzi. bila shaka Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwingi wa kusamehe.(35:28)

Kwa hiyo hekima ya kweli ni kumuogopa Mwenyezi Mungu(swt)kwa ukweli ,na pia kuogopa kumuasi yeye. Imamu Muhammad Baqir (a.s)a nasema: ukamilifu na kutimia kisawasawa ni kuelewa na kuwa na hekima(busara)katika dini, kwa maana ya kujaribu kuelewa dini kiukamilifu, na kuwa na subira katika kukabiliana na balaa, shida na changamoto za maisha, na pia kuwa mwangalifu na makini kimatumizi(uchumi)katika masuala mbalimbali ya kimaisha.

KUISHI NA WATU VIZURI

Miongoni mwa mambo ambayo yanaonyesha, ukamilifu wa akili ni kuishi na watu vizuri, bila kuwabughudhi na kuwabagua kwa misingi ya ukabila na udini n.k ,na kujiepusha na hali yoyote ambayo inaweza kuwa chanzo cha utengano, kama kuwateta, kuwa na kiburi, kujifaharisha kwao, kugonganisha jamii, kuwatukana, kuwadhulumu, kujikweza, na kuwa nduli mkubwa na kadhalika. kwani haya yote yanaonyesha upungufu wa akili ya mtu, mbali na hayo, inaonyesha ukosefu wa tabia nzuri kwa mwenye tabia hizi. tuliwambia kwamba akili ni kifaa ambacho mwanadamu amepewa na Allah, kikiwa safi, sasa ili kibakie na usafi wake ni lazima mwanadamu ajiepushe na kila aina ya madhambi ili aendelee kuhifadhi kifaa hiki. mfano ndani ya Qur-an Mwenyezi Mungu amemuita msengenyaji kuwa ni mwana haramu, na ni kwa sababu ya ubaya wa jambo hili, na huenda yeye kazaliwa kwa njia za kisheria ,lakini kulingana na tendo lake chafu ndiyo maana kapewa sifa hii. mwingine ni msengenyaji kapewa sifa ya mla nyama za maiti ,kwa sababu ya tendo lake ovu. kwa hiyo ili uishi na watu vizuri ni sharti ujiepushe na tabia ambazo zinavuruga akili, na hatimaye itaharibika akili yako. na itakosa ule utukufu wake wa asili, ambao Mwenyezi Mungu aliuelezea pale alipomuumba mwanadamu, alisema "sikuumba kiumbe ambaye ni bora na mtukufu kuliko wewe(yaani akili)".


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: