bayyinaat

Published time: 03 ,December ,2017      18:21:15
Baada ya kufariki dunia Imam Hadi AS, Imam Hassan Askari AS alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 22 na kushikilia wadhifa huo kwa miaka 6 hadi alipuawa shahidi akiwa na umri wa miaka 28. Katika mazingira hayo magumu, mtukufu huyo aliweza kufikisha ujumbe wa mafundisho ya Kiislamu katika nyanja tofauti zikiwemo .........
News ID: 140


Tumo katika siku za kukumbuka kuuawa shahidi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW yaani Imam wa kumi na moja katika silsila ya Maimamu kumi na mbili wa Ahlul-Baiti wa Mtume saw anayejulikana kwa jina la Imam Hassan bin Ali Askari AS. Siku kama ya leo mwaka 260 Hijiria, ulimwengu ulipatwa na huzuni ya kuondokewa na Imam Hassan Askari AS, ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW. Maisha mafupi ya Imam Hassan AS yaliyoendelea kwa kipindi cha miaka 28 yalijaza kurasa za vitabu vya historia.

Kwa hakika maisha ya Maimamu na Ahlul-Baiti wa Mtume SAW, yamejaa maarifa, ibra na mafunzo kwa ajili ya kumlea mtu na jamii ya mwanadamu kwa ujumla. Hata hivyo utawala wa kitaghuti, kidhalimu na halikadhalika kuwepo vizingiti vingi, kulitatiza harakati na shughuli za Ahlul Baiti AS kwa ajili ya kueneza mafundisho asili ya dini Tukufu ya Kiislamu.

Vizingiti hivyo vilishamiri sana katika kipindi cha Imam Muhammad bin Ali Taqi al-Jawad na Imam Ali bin Muhammad al Hadi AS na kushtadi zaidi wakati wa kipindi cha Imam Hassan Askari AS. Watawala wa wakati huo wa Bani Abbas, walimlazimisha Imam Ali al Hadi na mwanawe Imam Hassan Askari aliyekuwa na umri wa miaka minne wakati huo, kuuhama mji wa babu yao, Mtume Muhammad SAW wa Madina na kuelekea mjini Baghdad, Iraq ambako kulikuwa makao makuu ya watawala hao.

Imam Hassan Askari as achukua jukumu la Uimamu

Baada ya kufariki dunia Imam Hadi AS, Imam Hassan Askari AS alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 22 na kushikilia wadhifa huo kwa miaka 6 hadi alipuawa shahidi akiwa na umri wa miaka 28. Katika mazingira hayo magumu, mtukufu huyo aliweza kufikisha ujumbe wa mafundisho ya Kiislamu katika nyanja tofauti zikiwemo za kisiasa na kijamii kwa wanafunzi wake. Hata hivyo vikwazo na vizingiti vya aina mbalimbali vilivyowekwa na watalawa wa Bani Abbas, havikuweza kuzuia upendo wa watu kwa Imam Askari AS. Hali hiyo inaonyesha kuwa, nuru ya Mtume Muhammad SAW na Ahlul-Bayti wake AS, ni nuru ya haki ambayo kamwe haiwezi kuzimwa.

Zama za Uimamu Wake

Kipindi cha Imam Hassan Askari AS kilikuwa kipindi chenye misukosuko mikubwa zaidi cha watawala wa Bani Abbas. Uongozi usiofaa, migogoro ya ndani ya utawala, upinzani wa wananchi, harakati za mara kwa mara dhidi ya watawala na kuenea mafundisho potofu, ni miongoni mwa sababu za machafuko ya kisiasa na kijamii ya kipindi hicho.

Viongozi walikuwa wakiwanyonya raia, huku wakijenga makasri na majumba makubwa ya kifahari na kuwaacha watu wa kawaida katika hali ngumu ya kimaisha. Viongozi hao madhalimu hawakujali umasikini na tabu za raia bali waliendelea kujineemesha katika utawala. Waislamu walikuwa wanatambua kuwa Imam Hassan Askari ndiye atakayezaa mtoto anayesubiriwa kuja kuijaza dunia haki na uadilifu baada ya kuenea dhulma na uonevu.

Hali hiyo, ilizidisha vizingiti na ukandamizaji wa watawala dhidi ya Imam kiasi kwamba, ilimlazimu mtukufu huyo chini ya mpango ulioandaliwa na utawala, kuripoti katika siku maalumu za wiki katika ofisi za watawala wa wakati huo.

Hata hivyo na licha ya kuweko njama kubwa za watawala hao, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mapenzi na utukufu Wake, aliamua mtoto wa Imam Askari, yaani Imam Mahdi AS ambaye ni mwokozi wa ulimwengu, azaliwe salama usalimini. Baada ya kuzaliwa Imam Mahdi AS, Imam Hassan alianza kuiandaa jamii ya wakati huo kukabiliana na hali ngumu itakayoikabili jamii ya baadaye.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: