bayyinaat

Published time: 15 ,December ,2017      12:37:03
1. Kuna kujiona na kujikweza kwa sababu unajiona una elimu na maarifa makubwa kuliko wote , na hali hii inawakumba wale watu ambao wanaposoma na kufikia daraja fulani la elimu , watadhani kwamba wao wanamiliki kila kitu upande wa elimu , na wanafikia hatua ya........
News ID: 152

Katika sehemu iliyopita tulizungumzia maradhi mabaya ya nafsi nayo ni kujiona na kujikweza , tuliona tafsiri yake , na maana yake kwa upana , na sasa tunataka tuangalie sababu ambazo zinamfanya mwenye kujiona na kujikweza afanye hivyo .

Wametaja maulama wa elimu ya akh'laq (elimu ya tabia) kwamba kujikweza na kujiona ni katika sifa mbaya , ambazo ni kama mtihani aliwonawo yule ambaye amechagua kujivisha sifa hizi (kama tutazihesabu kuwa kila moja inajitegemea ) mbovu na chafu. maulama wanasema sifa hizi zinatofautiana , mtu na mtu , kuna ambaye imekwishaota mizizi , na kuwa sugu , na kuna ambaye bado ni changa , na kuna ambaye ni ya kati na kati , hivyo basi kutofautiana daraja ndiyo sababu ya kutofautiana madhara . maulama wametaja sababu nyingi za kuwa na sifa hizi kiasi kwamba hatuwezi kuzitaja zote hapa , tutataja baadhi yake .

1. Kuna kujiona na kujikweza kwa sababu unajiona una elimu na maarifa makubwa kuliko wote , na hali hii inawakumba wale watu ambao wanaposoma na kufikia daraja fulani la elimu , watadhani kwamba wao wanamiliki kila kitu upande wa elimu , na wanafikia hatua ya kuona kuwa fikira zao ziko juu kuliko wengine kiasi kwamba hawasikii ushauri wa mtu yoyote , na sababu ni hii kwa vile wao wanajiona kuwa wao ndiyo wenye fikra sahihi , vile vile wanajiona kwa kudhani elimu yao ndiyo kubwa kuliko wote , na kudharau elimu za wengine na kuwaona kuwa hawana thamani , hata kama watu wengine wanawachukulia kuwa ni wasomi , lakini kwa vile yeye anasifa ya kujiona na kujikweza na sifa hizi zimekomaa kwake , hataki kukubaliana na uhalisia wa jambo .

2. Na wakati mwingine kujiona kunatokana na mtu kujiona kuwa yeye ni mchamungu na hakuna mwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu kama yeye . na mtu wa namna hii mara nyinyi anafanya ibada zake kwa kujionesha ili apate heshima , kwa kuwa eti yeye ni mchamungu , sasa ili kujua kwamba mtu huyu ni mwovu na mbaya , ni pale atakapobishiwa na baadhi ya watu kwa jambo fulani na dogo , basi atafanya makubwa , kama kupayuka na kuropoka maneno ambayo hayana maana , kwasababu siku zote anataka aheshimiwe na akubaliwe kila anachokisema.

Katika hadithi ya Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w)alimwambia ibn Masuud, akisema: ewe mtoto wa Masuud usijikweze mbele ya Mwenyezi Mungu na wala usijikweze kwa yale mazuri unayoyafanya ,wala kwa elimu yako, wala kwa matendo yako ,wala kwa wema wako ,wala kwa ibada zako .

Kwa uhakika watu ambao wanadanganywa na ibada wanazozifanya , kiasi kwamba zinawapelekea kujiona na kujikweza , na kuwadharau wengine , mara nyingi wanaangamia na kuangukia kwenye shimo la upotevu .

Iblis alifanya ibada nyingi sana, kiasi kwamba katika hadithi mbalimbali tunasoma kwamba , hakuna sehemu yoyote ya ardhi isipokuwa alisujudu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu , kutokana na ibada zake alipata daraja kubwa na kuishi na malaika . lakini ibada zake sote ziliporomoka kwa muda mfupi alipo amrishwa kumsujudia nabii Adam , akakataa eti yeye ni bora . hivyo basi ibada ambazo sitakufanya ujione kwamba wewe ni bora kuliko wengine hazina tofauti na ibada za Ibilisi.

3.sababu nyingine ambayo inawafanya watu wajione na kujikweza , ni pale wanapofanya maovu na kusema Allah karimu na ni mwenye kusamehe na mwenye huruma , kwa hiyo mwenye sifa hizi chafu atasema mimi najua kwamba Mwenyezi Mungu mkubwa hawezi kuniadhibu kwa haya ninayoyafanya , kwa sababu tusipofanya uovu na madhambi , na Mungu akawa hajatusamehe na wala kutuhurumia , itakuwa haina maana kwa Mwenyezi Mungu kuitwa majina kama haya ,yaani mwenye kusamehe na mwenye huruma na kadhalika . na ndiyo maana tumesema kwamba hizi sifa zinampelekea yule ambaye amejipamba nazo kuangukia kwenye shimo la moto mkubwa na kuangamia humo milele . Mwenyezi Mungu anasema:ewe mwanadamu! Kitu gani kinakufanya ujikweze mbele na mola wako mkarimu ,aliyekuumba, akakuweka sawa, akakulinganisha ?

4. na katika sababu nyingine ambazo zinampelekea mtu kujiona na kujikweza, ni ujinga wa kutokuwa na maarifa , kama tulivyosema kwamba kuwa na elimu inaweza kuwa sababu ya kuwa na sifa hizi , kadhalika kukosa elimu inaweza kuwa sababu ya kujiona na kujikweza katika baadhi ya watu . Imam Ali(a.s)anasema: ambaye ni mjinga(yaani hana elimu)mara nyingi anajiona na kujikweza , na siku yake ni hatari, kuliko ya jana iliyopita . na hapa Imam anataka kutufundisha kwamba mtu mjinga hatari yake inaongezeka kila siku , na kuzidiana kiasi kwamba siku ya leo inakuwa ni mbaya kuliko ya jana .

5. miongoni mwa sababu ambazo zinampelekea mtu kujiona na kujikweza , ni kudanganywa na dunia na mapambo yake , na kuwa na mali , na cheo, au kujiona kuwa yeye ni kijana, au yeye ni mzuri, au ana nguvu kuliko wote na kadhalika … hakika watu wengi wanapojihusisha sana na dunia inawadanganya, na kuwavutia na kuipenda mno, na wanaghururika nayo na inakuwa sababu ya kuwa na sifa ambazo tunazizungumzia . au wanajiona kwa mali walizonazo na kusahau kuwa mali hizo ni kama wameazimwa na Mwenyezi Mungu, na zinaweza kurudi kwake . na kusahau huku kunampelekea kuwa na ghururi na kijiona na kujikweza, na haya yote yanamfanya awe mbali na Mwenyezi Mungu na kuwa karibu na shetani.na hapa tujalie labda amezipata kwa njia ya halali, na ndiyo maana tukasema kwamba huyo ni kama ameazimwa na Mwenyezi Mungu, lakini yupo ambaye amezipata kwa njia ya haramu, bila shaka inatutosha kufahamu kwamba huyo ni shetani aliyekamilika, na kuwa nasifa kama hizi siyo jambo geni, kwani hizi ndizo sifa za Iblis . au mali hizi ambazo zinamfanya ajione na kujikweza, huenda hazitolei hata haki ya kisheria kama kuzitolea zaka na khumsi na kadhalika ... na mfano wake ni kama Qaruun ambaye alikuwa na mali nyingi, na alizipata kwa dua aliyeombewa na Nabii Mussa, na baada ya kuwa tajiri mkubwa akajiona, na akakataa kutoa haki za kisheria na kudai kwamba mali hizo amezipata kwa ujanja wake, na kisha Mwenyezi Mungu akamuangamiza .

Na kama tulivyosema kwamba kuna kujiona na kujikweza kwasababu eti wewe ni mzuri,naam kwa kipimo unaweza kujiona kuwa wewe ni mzuri,na ikawa ndiyo sababu ya kuwa na sifa hizi mbaya, tambua kuwa wewe hujajiumba angetaka Allah angekufanya kama mnyama fulani tena dhalili na mbaya na hatuna haja ya kukupigia mfano katika hilo . lakini tukumbuke kwamba uzuri ni jambo la mtu mwenyewe, siyo kila unapohukumu kuwa wewe ni mzuri, ndiyo sababu ya watu wote kuhukumu hivyo . na ingekuwa hivyo basi watu wasingeoa wala wasingeolewa, kwani unaweza kumuona mtu Fulani ukahukumu kuwa ni mbaya, lakini ameolewa au ameoa, kwani yule aliyemuoa au aliyeolewa naye hawakuona ubaya ila wewe? kwa hiyo kuhukumu kuwa wewe ni mzuri ikawa sababu ya kujiona , bali ni kukosa shukurani maana kama utajiona kuwa wewe ni mzuri basi mshukuru Mwenyezi Mungu na umwombe akuingize katika pepo yake , na itakuwa hakuna maana yoyote, kwa yule aliyejiona kuwa ni mzuri, siku ya kiyama akaingia ndani ya moto wa Jahanamu .

6. kujiona kwa sababu una cheo, haina maana kwani kuna watu ambao walitumwa na Mwenyezi Mungu na wakawa na vyeo, na wakaimiliki dunia lakini katu hawakuwahi kuwa na sifa hizi, mfano nabii Muhammad(s.a.w.w),nabii Sulaimani na wengineo, na hawa wote wamemiliki dunia, lakini wewe huenda cheo chako ni kumiliki nchi, au mkoa au wilaya ,au nyumba kumi, au kikundi cha watu, kiasi kwamba wakiamua wanaweza kukupindua, na kukutia korokoroni .

Mwandishi: Alhaj Sheikh Kadhim Abbas


LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: