Ni jambo lililo wazi
kabisa kwamba watu wawili wanapoamua kuingia katika mahusiano ya ndoa, basi
kila mmoja alikuwa ameweka vigezo vya mwenza amtakaye ili aweze kuwa naye
katika maisha hayo ya pamoja. Jambo la muhimu hapa na ambalo watu wengi sana
huwa wanaghafilika nalo ni kuhusiana na kwamba je, unapoweka vigezo kwa ajili
ya kupata mke au mume wa maisha yako, na ikatokea umempata, ndio huwa mwisho wa
kila mmoja wenu kupambika na vigezo vile au la?.
Bila shaka jawabu la kila mmoja wetu
litakuwa ni hapana, kwa maana ya kwamba unapokuwa umechaguliwa na mwenza wako
kwa ajili ya maisha ya pamoja basi huna budi kuendelea kujipamba na vile vigezo
ambavyo kwavyo alikuchagua, kwa maana ikitokea akaona umebadilika n a huna tena
yale mambo ambayo alikupendea basi itakuwa ndio mwanzo wa matatizo ndani y a
ndoa yako.
Naomba nieleweke
jambo moja hapa nisemapo kwamba inatakiwa uendelee kuwa na vigezo ambavyo
kwavyo ulichaguliwa na mwenza wako, sina maana vigezo ambavyo sio msingi sahihi
wa kuchagua, bali nakusudia vile vigezo sahihi ambavyo dini yetu ya Uislamu
imetuambia tuviangalie kwa wenza wetu, kama vile dini, tabia njema na mfano wa
hayo.
Sasa basi katika
kuhakikisha kwamba mwanandoa anabakia katika vile vigezo vyake ambavyo
vilifanya aweze kuchaguliwa, Uislamu haukubakia nyuma katika kuendelea kumpa
nasaha huyu mwanandoa ili tu asije kughafilika.
Na leo tutachambua
riwaya moja kutoka kwa Imamu Sadiq (as) ambayo anatuhusia kwamba tusije
kudhania kwamba mume au mke baada tu ya kuwa pamoja na mweza wake basi anakuwa
amekamilisha kila kitu, n a hana jambo lingine analotakiwa kulifanya katika
ndoa yake hiyo, kwa maana hana hitajio lingine zaidi tu ya kuchukua mwenza.
Hivyo basi msingi mzima wa mada hii ni kuhusiana na mambo ambayo kila mmoja
kati ya mume na mke wanahitajia katika mahusiano yao haya yaliyobarikiwa.
Imamu Sadiq (as)
anaanza kwa kusema:
لا غنى بالزوج عن ثلاثة أشياء فيما بينه وبين زوجته وهي:
الموافقة ليجتلب بها موافقتها ومحبتها وهواها .
وحسن خلقه معها
واستعماله استمالة قبلها بالهيئة الحسنة في
عينها وتوسعته عليها
"......Mume hatakiwi
kujitosheleza mambo matatu kwa mke wake,
kuafikiana naye, ili tu aweze kuvuta mapenzi yake na pia awze kumfanya naye aafikiane
naye, kuishi naye kwa tabia njema, na kuutawala moyo wake kwa njia ambayo
itampendeza katika macho yake kama vile kumuhudumia kadri ya uwezo......”[1]
Ufafanuzi:
·
Hapa tunakuta Imamu (as) ameanza nasaha na wanaume
kwanza, ikiwa na maana ya kwamba wasiwe ni vifua mbele tu katika mambo ambayo
yanaelekea sana upande wao, bali hata kama si upande wao basi ni kwa kuwa wao
ndio nguzo ya familia basi inatakiwa wayafanye kwa lengo la kuimarisha misingi
ya mahusiano yao. Hivyo basi anatakiwa asiachane na mambo yafuatayo:
1.
Kuafikiana na Mke wake
Kwa
maana ya kwamba ni lazima kuwe na maafikiano na kuendana baina ya wana
mahusiano, na kuendana huku si tu katika mambo ya kidhahiri, bali pia iwe
katika mambo ya kifikra, kiasi kwamba mume ajihisi yeye na mke wake ni kama
mwili mmoja. Na faida ambayo imamu ameitaj akatika jambo hili ni kwamba bila
shaka mke atakapoona kwamba mume wake ni mwenye kujipamba na hali kama hiyo,
anamjali, anamchukulia kama mwili wake, anahuzunika na kufurahi naye, basi mke
huyu naye atajibu mapigo kwa namna nzuri zaidi ambayo ni kumpenda na kuendana
na mume wake kama ambavyo mume kaujenga msingi huu.
2.
Kuishi naye kwa mwenendo ulio mwema
Matatizo
mengi sana katika mahusiano ya wana ndoa huanzia hapa, kwamba mume anaishi na
mke wake kwa namna ambayo mwanamke hawezi kuhimili. Ukali, tabia mbaya n a
mfano wa hayo. Inafika kipindi tukubali kwamba mke kama mke ameumbwa kwa
kupenda kudekezwa, kuishi kwa upole na hali kadhalika, sasa mume anapokuwa
hajachunga mambo haya, na akamfanya mke wake kama kijakazi wake na akaamua
kuishi naye kwa hali ambayo mke ataihesabu ni kama ukali, hapo kutakuwa na
tatizo bila shaka.
3.
Kuutawala moyo wa mke
Jambo
hili kwa kweli linahitajia uelewa kwanza wa njia ambazo mke wako unaweza
kuutawala moyo wake kwazo. Lakini Imamu hapa anaashiria jambo ambalo
tukiliangalia basi bila shaka utakuta ni lenye kushirikiana kwa wanawake wote,
hivyo basi kama wanaume watatumia jambo hili basi itakuwa ni silaha kubwa mno
katika kuutawala moyo wa mke wake. Jambo lenyewe ni kumuhudumia mke wako, ndio,
hakuna mwanamke ambaye hapendi kuhudumiwa na mumewe, kama ambavyo pia hakuna
mwanaume ambaye anapenda kumuona mke wake akiwa rafu bila ya mpangilio mzuri wa
kupendeza, hivyo basi mume inatakiwa ajitume kwa kadri ya uwezo wake ili tu
aweze kufanikisha haya yote mawili, kwanza amuone mke wake katika hali nzuri ya
kupendeza macho, n a kisha aweze kuuteka moyo wa mke wake kwa jambo hilo.
Na katika swala hili
kuna maulama ambao wametoa fatwa kwamba ni Suna kwa mume kujipinda kwa ajili ya
familia yake, pia hata Mtume (saww) ana maneno yake yasemayo "....Mwenye
kufanya juhudi kwa ajili ya familia yake, ni sawa na mpiganaji jihadi katika njia
ya Mwenyezi Mungu (swt)”.
Hivyo basi mume hana
budi kushikamana na haya mambo ili tu aweze kudumisha na kuweka misingi mizuri
ya maisha ya ndoa yake.
Ungana nami katika wakati ujao ili
tuweze kuona nasaha au mambo ambayo mke pia anatakiwa kushikamana nayo katika
mahusiano yake na mumewe.
Sh Abdul Razaq Bilal.