bayyinaat

Published time: 16 ,December ,2017      20:18:49
Unyenyekevu una vigawanyo vikuu viwili vya kimsingi , na katika vigawanyo hivyo ni kimoja tu ndicho kinachosifika kwa Mwenyezi Mungu na kuwa ni katika sifa zilizokuwa ni njema.........
News ID: 156

Katika tabia na mienendo mizuri inayomlazimu kila mwanadamu kuwa nayo, ni kuwa na unyenyekevu . Kwani kiuhakika unyenyekevu ni katika sifa zinazomfurahisha zaidi Mwenyezi Mungu na zenye faida kemkemu kwa wanadamu .

MAANA YA UNYENYEKEVU

Unyenyekevu ni hali ya kuheshimu na kujali watu kulingana na hali, nafasi, hadhi ama uwezo wao katika jamii na kutojikweza mbele yao. Unyenyekevu ni tabia njema na, ni silika yenye kuvutia , pia huchochea upendo na kuthaminiana baina ya wanajamii .

QUR-ANI NA UNYENYEKEVU

Katika utukufu wa tabia hii itutoshe kwamba Mwenyezi Mungu(swt) mwenye shani alimuamuru kipenzi chake, na Bwana wa Mitume wake kuwa mnyenyekevu . Pale aliposema:

"Na uteremshe ubawa wako {wa rehema} kwa wale waumini wanaokufuata”. Qur-an 26:215

Anaambiwa Mtukufu wa cheo na daraja Bwana wa viumbe vyote Mtume Muhammad (s.a.w.w) kujipamba na sifa tukufu ya unyenyekevu . Kama ambavyo imeamrishwa kwa Mtume kuwa mnyenyekevu kwa masahaba wake , ni hasara ilioje kwa sisi tulio nyuma ya nyayo zake kuipuuzia mbali sifa hii .

VIGAWANYO VYA UNYENYEKEVU

Unyenyekevu una vigawanyo vikuu viwili vya kimsingi , na katika vigawanyo hivyo ni kimoja tu ndicho kinachosifika kwa Mwenyezi Mungu na kuwa ni katika sifa zilizokuwa ni njema.

1. Unyenyekevu wa kupindukia :

Mtu anapokuwa amejishusha kupita kiasi mbele ya madhalimu na mabeberu wa ulimwengu huu , kiasi kwamba akawa hana analolisema wala kulifanya , vyovyote atendewavyo katika mambo mabaya na maovu , hali hii sio unyeyekevu bali ni "UDHALILI” na hiyo haitokuwa ile sifa aliyomtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake kujipamba nayo .

2. Unyenyekevu wa kati na kati , na huu ndiyo unyenyekevu unaokusudiwa .

Hii ni hali ambayo inakuwa kati na kati , yaani ni mtu kutokuwa Mnyenyekevu kupita kiwango , kiasi ambacho ananyenyekea hata mbele ya haki yake endapo itachukuliwa, na tumesema hapo juu kwamba hali hii sio unyenyekevu bali ni udhalili mbele ya jamii ,

na pia kukosa kabisa sifa hii ya unyenyekevu ina maana wewe : ima utakuwa unaelekea katika sifa ya kiburi au kwa lugha nyepesi tunasema kwamba wewe ni mwenye kiburi. Kwa hiyo sifa ya unyenyekevu ni ile hali ambayo hutoonekana kuwa ni dhalili na wala kuonekana kuwa ni mwenye kiburi . na huu ndiyo unyenyekevu ambao aliamrishwa Bwana Mtume kuwa nao mbele ya maswahaba zake na sisi pia tunatakiwa tuwe hivyo .

Kimsingi ni kwamba unyenyekevu ni silika ya kusifiwa pale,inapokuwa ni ya baina baina(yaani kati na kati). Ama ule unyenyekevu wa kumfanya mtu adharaulike mbele ya watu au kuwa na kiburi si katika sifa zenye kupendeza mbele ya Mwenyezi Mungu , lakini pia hata jamii haipendi mtu mwenye kiburi , na tabaani unyenyekevu ni kinyume cha kiburi.

BAADHI YA HADITHI KUNAKO UNYENYEKEVU

Imepokewa kuwa Bwana Mtume (s.a.w.w) alisema: -

" Hakika mpendwa wenu kwangu, na mkaribu wenu zaidi kwangu siku ya Qiyama, ni yule mbora wenu wa kitabia, na mwingi wenu wa unyenyekevu. Na hakika kati yenu aliyembali nami sana siku ya Qiyama ni wenye maneno mengi ambao ndiyo wenye kiburi ”

Imepokewa pia kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) amesema:

" Mbinguni wapo malaika wawili wamekabidhiwa waja wa Mwenyezi mungu, Yeyote anayenyenyekea kwa ajili ya Mwenyezi mungu (swt) basi malaika hao humnyanyua, na anayetakabari basi malaika hao humshusha daraja ” .

Kama inavyo onekana katika hizi riwaya ni kwamba swala zima la unyenyekevu katika maneno ya Mtume {s.a.w.w} na hata Maimamu (a.s) limepewa kipaumbele na hata mahala pengine kupewa dhamana ya kuingia au kutokuingia katika pepo ya Mwenyezi Mungu, kwa maana ukiwa na unyenyekevu ni kama una ruhusa ya kuingia peponi, na kama huna ina maana wewe ni mwenye kiburi ,na kuwa na sifa ya kiburi ni sawa na kuwa na ruhusa ya kuingia motoni .

VISA KUHUSIANA NA UNYENYEKEVU

Imepokelewa kwamba Mtume (s.a.w.w) alikwenda kisimani kuoga. Hudhaifa bin Yamani akamshikia nguo kwajiri ya kumsitiri hadi alipomaliza kuoga. Ilipofika zamu ya Hudhaifa kuoga, Mtume (s.a.w.w) akasimama kumshikia nguo na kumsitiri wakati anaoga , Hudhaifa akakataa kata kata na kusema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tafadhali wewe usifanye hivyo.” Mtume (s.a.w.w) hakukubari kuacha na alimshikia nguo hata alipomaliza kuoga kisha akamwambia "Kamwe hawakuwa marafiki watu wawili ila yule aliye mwema zaidi kwa mwenzie ndiye apendwaye zaidi na Mwenyezi Mungu.” .

Imepokewa pia , kwamba Mtume (s.a.w.w) alikuwa safarini na akaamrisha aandaliwe kondoo. Mmoja katika masahaba akasema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nitamchinja , mwingine akasema: mimi nitamchuna , mwingine akasema mimi nitampika , naye Mtume akasema nami nitakusanya kuni .” Masahaba wakasema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu sisi tutakutosheleza.” Akawajibu "Najua mnatosha lakini nachukia kujitofautisha nanyi kwani Mwenyezi Mungu (swt) anamchukia mja (Mtume ) wake anapojibagua baina ya masahaba wake.” Alisimama na kukusanya kuni .

Ewe ndugu yangu ona ni namna gani aliyekuwa mbora wa viumbe baina ya watu wake na jamii iliyokuwa inamzunguka , hakupatwa na hali ya kiburi kwa kuwa yeye ni Mtume wala kwa kuwa yeye ni kiongozi , bali alikuwa mnyenyekevu kiasi cha kuweza kukusanya kuni kwa ajili ya masahaba wake . kiuhakika tunapaswa kubadilika na kuwa wanyenyekevu mbele ya jamii .

Mwandishi :Alhaj Sheikh Kadhim Abbas


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: