bayyinaat

Published time: 20 ,December ,2017      20:17:53
Katika ulimwengu wa leo bila shaka hakuna mtu anayeweza kusema kuwa, hataki maendeleo. Na kama akitokea mtu wa aina hiyo basi atakuwa kituko na kioja kwa watu na wanajamii anaoishi nao. Kwani ili aende na..................
News ID: 158

Katika ulimwengu wa leo bila shaka hakuna mtu anayeweza kusema kuwa, hataki maendeleo. Na kama akitokea mtu wa aina hiyo basi atakuwa kituko na kioja kwa watu na wanajamii anaoishi nao. Kwani ili aende na wakati hana budi kuyakubali na kuyapokea maendeleo pamoja na utandawazi (globalization). Kwa maana kwamba, kama atatokea mtu katika zama zetu hizi na atake kuishi kwa mujibu wa miaka 100 iliyopita, bila shaka ataonekana kituko na kioja. Kwani kwa mfano vyombo vya usafiri zamani vilikuwa punda na farasi kwa wenye uwezo. Hii leo kuna kuna gari, treni, meli na ndege. Safari ambayo zamani mtu akitumia miezi kadhaa kufika, leo anaweza kukata masafa yake kwa masaa kadhaa tu kwa kutumia usafiri wa anga. Hivyo, kiujumla maendeleo ni jambo linalofurahiwa na kupokewa kwa mikono miwili na kila mtu mwenye akili timamu. Maendeleo bila shaka yamerahisisha maisha ya watu katika kila uga, iwe ni mawasiliano, usafiri na kadhalika. Tab’ani kila mtu anayapokea maendeleo kulingana na haja na matumizi yake. Hasa kama maendeleo yenyewe yatakuwa ni ya teknolojia na mawasiliano. Hii leo sote tunaishi katika ulimwengu ambao tumezungukwa na anuwai kwa anuwai ya vyombo vya habari na vya mawasiliano. Redio, televisheni, satalaiti, intaneti, simu ya mkononi na kadhalika. Zamani, tena hata sio zamani sana, mtu alikuwa akiandika barua mathalani Dar es Salaam na kuituma kwa posta, kufika kwake ilikuwa ikichukua wiki moja na hata zaidi. Simu wakati huo ilikuwa ni taabu mno. Nyumba zilizokuwa na simu za mezani (landline) zilikuwa zikihesabika kama pale mtaani au pengine baadhi ya wengine walikuwa wakilazimika kwenda kwa jirani mtaa wa pili kusubiria simu ya mtoto wake aliyeko Uarabuni aliyeahidi kwamba angepiga simu majira ya jioni. Siku zikapita na kusonga mbele, ambapo taratibu simu za mkononi zikaanza kuingia na adha ya mtoto kutumwa kila siku kwenda kumuita jirani aje kuzungumza na simu yake ikaanza kupungua. Hii leo pengine ni watu wachache mno ambao katika maisha yao ya kila siku hawatumii masaa kadhaa wakiwa wanashughulishwa na simu, kuanzia facebook, twitter, Whatsapp, viber, tango, line, talkbox, talkray, telegram, instagram na huduma nyingine nyingi za mawasiliano zinazopatikana katika hizi simu za kisasa zinazojulikana kama smartphone (simu erevu) ambapo baadhi wanapenda kuziita "Simu za Tachi” na nyinginezo. 
Bila shaka kutumia suhula na nyenzo za kisasa kwa ajili ya mawasiliano baina ya watu, ni jambo lenye taathira kubwa kwa familia na jamii na hata kubadilisha mtindo wa maisha (life style) wa mtu. Hii leo ukipanda basi, ni mara chache kusikia mijadala ya kisiasa kama zamani, au ubishi wa mpira wa Simba na Yanga. Ligi ya Uingereza, Laliga au mambo ya siasa ya CUF na CCM; kwani kila mtu ameshughulishwa na simu yake. Hata wengine wanasema, simu hizi zimesaidia kumshughulisha mtu anapokuwa katika foleni na hivyo kumpunguzia presha na maumivu ya foleni hasa katika jiji la Dar es Salaam. Baadhi ya nyumba baba, mama, na watoto kila mmoja ana simu yake au tablet hivyo ameshughulishwa na kuchati. Wanafamilia hawana tena muda wa kuongea kwa muda mrefu kama zamani. Zamani itapoingia magharibi watoto walikuwa wakikaa karibu na babu au bibi na kupigiwa hadithi au kusimuliwa visa vya kale vilivyokuwa vimejaa mafunzo. La kusikitisha ni kwamba, baadhi wanaghafilika na hata kusahau majukumu yao ndani ya nyumba kwa sababu ya simu. Katika hili sio akina mama tu, bali hata akina baba nao pia wamo. 
Itaendelea……
Na Maalim Salum Bendera


non-publishable: 0
Under Review: 1
Published: 1
2639/03/16 - 20:13
|
Iran, Islamic Republic of
|
Rashid Ali
0
0
mashallah. makala nuzri sana
Administrator Karibu
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: