bayyinaat

Published time: 20 ,December ,2017      20:19:57
Karibuni hivi nilikuwa nikizungumza na swahiba wangu mmoja kuhusiana na hili, akaniambia lakini unajua bora hivyo kuliko zamani watu walikuwa wakikaa na kusengenya. Kushibana kwetu.......
News ID: 159


Karibuni hivi nilikuwa nikizungumza na swahiba wangu mmoja kuhusiana na hili, akaniambia lakini unajua bora hivyo kuliko zamani watu walikuwa wakikaa na kusengenya. Kushibana kwetu hakukuwa sababu ya mimi kutopinga hoja yake hiyo. Nilimwambia kwamba, hilo kwa upande mmoja yawezekana kulitazama hivyo lakini katika upande wa pili, usisahahu kwamba, watu siku hizi wanasengenya pia kwa simu. Si hayo tu, mko kwenye chombo cha usafiri mtu anapigiwa simu utamsikia anasema "Niko Muhimbili” ilhali mko Kimara mnaelekea Mbezi. Uongo wa wazi tena mbele ya kadamnasi, bila ya haya wala soni. Kwa hakika simu kama ilivyo satalaiti, ina mambo mengi mazuri na mabaya. Unaweza kupata programu nzuri za Kiislamu, Qur’ani kwa maandishi, sauti za wasomaji Qur’ani mashuhuri na tofauti duniani na mengineyo. Si hayo tu, Makala mbalimbali za kielimu, masomo na mengi mengineyo yenye faida nyingi. Hivyo inategemea na jinsi mwenyewe unavyoitumia simu yako. Kwenye vikao na hata mihadhara ya kidini nje na ndani ya misikiti, baadhi ya watu hushughulishwa na simu zaidi kuliko kinachozungumzwa pale. Au wengine unazungumza naye huku anachati. Kasi na ongezeko la simu pamoja na matumizi yake kwa namna fulani ni tishio kwa mfungano na hali ya ukaribu baina ya wanafamilia.

Jarida moja liliandika hivi karibuni kwamba, hii leo kuna simu za mkononi zaidi ya bilioni moja. Katika baadhi ya nchi, zaidi ya nusu ya wakaazi wake wana simu za mkononi. Jarida The Bulletin la Australia linaripoti hivi: "Idadi ya simu za mkononi zinazotumiwa inakaribia jumla ya idadi ya televisheni na kompyuta.” Katika nchi zaidi ya 20, idadi ya simu za mkononi inapita idadi ya simu za waya (Landline). Mtaalamu mmoja amesema kwamba, zaidi ya kuwa ni hatua kubwa ya kiteknolojia, lakini simu za mkononi "zimebadili jamii.” Tukiachana na faida na madhara ya matumizi ya simu kijamii, kwa upande wa kiuchumi na kurahisha miamala, teknolojia ya simu imekuwa na nafasi muhimu sana na hata baadhi ya nchi zimekuza uchumi kupitia teknolojia hii. Wafanyabiashara wengi wanafaidika kwa kuwa simu nyingi za mkononi zinauzwa. Shirika moja kubwa lilisema hivi: "Simu ya mkononi ndicho kifaa cha elektroniki kinachouzwa kwa wingi zaidi.” Basi, leo watu wanatumia pesa nyingi zaidi kununua simu za mkononi ikilinganishwa na pesa walizotumia zamani kununua kifaa chochote kile cha elektroniki.

Hivyo basi, teknolojia hii ya mawasiliano ina faida nyingi na mambo mabaya pia isipokuwa la msingi ni kuwa makini juu ya namna tunavyoitumia. Tutumie simu kwa mujibu wa mahitaji na kwa njia sahihi kulingana na mafundisho ya dini yetu. Wazazi jukumu lao hapa ni zito kwani hiki kizazi kinachoinukia "kizazi cha teknolojia na mitandao” kinapaswa kuandaliwa mazingira mazuri na ramani ya njia ya namna ya kutumia nyenzo hizi za mawasiliano. Njia bora kabisa ni malezi bora kwa misingi ya Uislamu. Baadhi ya waume simu imekuwa mke wa pili na hivyo hivyo kwa wanawake. Hivi umewahi kujiuliza tangu uamke leo umesoma Qur'ani? Na je umeshika simu yako na kuperuzi mara ngapi? Mwisho tunamuomba Allah atujaalie tuwe ni wenye kutumia vizuri teknolojia mpya na wakati huo huo huo, maendeleo yasitupumbaze na Mwenyezi Mungu na mambo mengine mazuri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh

Na Maalim Salum Bendera


non-publishable: 0
Under Review: 0
Published: 1
2639/03/16 - 20:12
|
Iran, Islamic Republic of
|
Anonymous
0
0
makala nzuri sana.
Administrator Karibu
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: