bayyinaat

Published time: 28 ,December ,2017      21:02:15
Safari ya Imam Ridha ya kubaidishwa kutoka mji wa Madina na kupelekwa Marw nchini Iran mwaka 200 Hijiria, ilifanyika kutokana na sisitizo na vitisho vya Maamun mtawala wa Kiabbasi, na mtukufu huyo alielekea katika mji wa Khorasan
News ID: 169

MAISHA YAKE

Bibi Maasuma alipitisha maisha yake yaliyojaa saada akiwa anajishughulisha na kutoa mafunzo ya Kiislamu na kuifasiri Qur'ani. Aidha alitumia wakati wake wote akijikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kutokana na mwenendo wake huu wa kufuata dini kikamilifu na kutotoka katika mkondo wa uongozi aliweza kufika daraja ya juu ya ukamilifu na ubora wa mwanaadamu. Imam Ridha AS katika kubainisha takuwa ya juu pamoja na utakasifu wa dada yake na uchaji Mungu aliokuwa nao alimtaja kuwa ni 'Maasuma' yaani mwanamke aliyetakasika na asiyekuwa na dhambi.

SAFARI YA KUMFUATA KAKA YAKE

Safari ya Imam Ridha ya kubaidishwa kutoka mji wa Madina na kupelekwa Marw nchini Iran mwaka 200 Hijiria, ilifanyika kutokana na sisitizo na vitisho vya Maamun mtawala wa Kiabbasi, na mtukufu huyo alielekea katika mji wa Khorasan nchini Iran pia bila kufuatana na mtu yoyote wa familia yake au watu wa nyumbani kwake. Mwaka mmoja baada ya kuhama kaka yake, Bibi Fatima al Maasuma huku akifuatana na baadhi ya kaka zake na watoto wa kaka zake alianza safari ya kuelekea Khorasan kwa ajili ya kumuona kaka yake huyo na muhimu zaidi kutekeleza jukumu la kutetea nafasi ya wilaya na uongozi.

Msafara wake ulipokelewa na kulakiwa na watu wengi katika kila mji waliopita. Bibi huyo mtukufu pia alifikisha ujumbe wa kudhulumiwa na kuachwa peke yake kaka yake kwa waumini na Waislamu wa sehemu alizopitia, kama alivyofanya Bibi Zainab (A.S), na kuonyesha upinzani wake na wa Watu wa Nyumba ya Mtume (A.S) dhidi ya utawala uliokuwa umejaa hila wa Bani Abbas. Kwa ajili hiyo, msafara wa bibi huyo mtukufu ulipofika katika mji wa Saveh, baadhi ya watu waliokuwa wakiwapinga Ahlul-Baiti waliokuwa wakiungwa mkono na vibaraka wa utawala huo waliuzuia msafara huo, na kupigana na waliofutana na bibi huyo suala ambalo lilisababisha karibu wanaume wote wa msafara huo kuuawa shahidi. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya Bibi Fatima Maasuma pia alipewa sumu na waovu hao. Alaa Kulli hal Bibi Fatima al Maasuma (SA) aliugua, labda kutokana na majonzi na huzuni kubwa iliyotokana na tukio hilo au kutokana na athari ya sumu aliyopewa, na kwa kuwa hakuweza tena kuendelea na safari yake kuelekea Khorasan, aliamua kwenda katika mji wa Qom. Alisema: ' Nipelekeni katika mji wa Qum, kwani nilimsikia baba yangu akisema kwamba, mji wa Qum ni kituo cha wafuasi wetu.'

Wakuu wa mji wa Qum walipofahamu kuhusu ujio wake waliharakisha kwenda kumlaki. Mussa bin Khazraj mmoja wa wazee wa mji huo aliwatangulia watu wote kwenda kumlaki bibi huyo mtukufu. Tarehe 23 Rabiul Awwal mwaka 201 Hijiria Bibi Fatima Maasuma aliwasili katika mji mtukufu wa Qum. Aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitun-Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW).

Mwishowe katika siku kama ya leo yaani tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake Imam Ridha (A.S), Bibi Fatima al Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Watu wa Qum na wapenzi wa Ahlul-Baiti waliuzika mwili wa bibi huyo mtukufu katika eneo ambalo wakati huo lilikuwa nje ya mji lililojulikana kama 'Bustani ya Babol'. Baada ya kuzikwa Mussa bin Khazraj aliweka juu ya kaburi la mtukufu huyo mikeka mingi. Hali hiyo ilibaki hivyo hadi mwaka 256 Hijiria ambapo Bibi Zainab binti wa Imam Jawad (A.S) alijenga kuba la kwanza juu ya kaburi la shangazi yake huyo mtukufu, na kwa utaratibu huo eneo hilo alikozikwa mtukufu huyo wa Kiislamu, likawa kivutio cha nyoyo za wapenzi na maashiki wa Ahlul Baiti (A.S) na wafuasi wa Maimamu Watoharifu. Kutokana na baraka ya eneo hilo, hadi hii leo mji wa Qum ni moja ya vituo vikubwa vya elimu ya Ahlul-Baiti na dini tukufu ya Uislamu.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: