bayyinaat

Published time: 06 ,February ,2018      18:46:18
News ID: 223

Na Salum Bendera-Tehran

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitokea 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (radhiallahu anhu) na kuhitimisha utawala wa kiimla wa mfalme Shah. Wakati Imam Khomeini (ra) aliporejea Tehran kwa kishindo mwanzoni mwa mwezi Februari 1979 na baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka mingi, hakuna mtu yoyote aliyedhani kwamba mapinduzi hayo yangefikia ushindi kwa kasi kubwa na katika kipindi cha siku kumi tu baada ya yeye kuwasili nchini. Watawala wa kitaghuti wa Iran katika kipindi hicho wakishirikiana na waungaji mkono wao wa kigeni walidhani kwamba, ingekuwa kazi rahisi kwao kukandamiza harakati ya mapinduzi hayo ya Kiislamu. Miezi michache kabla ya kurejea Imam Khomeini kutoka uhamishoni Ufaransa, watawala hao wa kitaghuti hawakudhani kwamba kungetokea harakati kama hiyo ya kimapinduzi nchini humo. Baada ya kufanya uchunguzi na kutathmini hali ya mambo mwezi Agosti 1978, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilisema kuwa jamii ya Iran haikuwa katika hali ya mapinduzi wala kukaribia kushuhudia hali kama hiyo. Shirika jingine la habari za kiulinzi la Marekani DIA lilidai kwamba Shah wa Iran angeendelea kutawala kwa udhibiti mkubwa kwa muda wa miaka mingine 10. Katika upande wa pili, George Ball mwanafikra na mwanasiasa mashuhuri wa Marekani alitoa mapendekezo saba ya kuzuia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Licha ya njama hizo zote lakini harakati ya Mapinduzi taratibu ilitoka kwenye hatua moja na kuingia nyingine bila kupata madhara makubwa. Harakati hiyo iliendelea hadi tarehe 22 Bahman au 11 Februari 1979 ambapo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na uongozi shupavu wa Imam Khomeini (MA) Mapinduzi ya Kiislamu yalifikia ushindi kwa mshangao mkubwa wa walimwengu.
Ama kwa kweli kurejea nchini Iran kwa kishindo Imam Khomeini na kupokelewa kwake kwa shangwe na nderemo na mamilioni ya wananchi kulikuwa na nafasi muhimu na ya kihistoria iliyoweka wazi nafasi muhimu ya wanazuoni katika kuongoza wanadamu katika njia nyoofu. Jambo hilo lilionyesha wazi kuwa wananchi wa Iran walikuwa na irada thabiti ya kufanya mapinduzi chini ya uongozi wa kidini ili kufikia malengo waliyokusudia. Mapinduzhi hayo yaliweza kufikia ushindi katika kipindi kifupi mno. Imam Khomeini alisema kuhusiana na mapinduzi hayo kwamba ulikuwa ni muujiza wa Mwenyezi Mungu.

Taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Miongoni mwa taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kutia nguvu udugu wa Kiislamu na kuleta na kuimarisha mshikamano kati ya Waislamu. Mapinduzi hayo yalifufua hima ya kuzingatia mafundisho ya Qur'ani Tukufu na sira tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kuweka msingi wa umoja wa Kiislamu na kuleta kigezo cha mshikamano na utangamano kati ya Waislamu.
Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, tangu awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa mwito kwa Waislamu wote duniani kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kukabiliana na watawala madikteta na maadui wa Uislamu. Alisisitiza mara nyingi kuwa siri ya kuweza mataifa ya Waislamu kurejesha heshima yao ni kufungamana na kuwa na kauli moja.
Katika moja ya matamshi yake, Imam Khomeini alisikika akisema: Enyi Waislamu duniani ambao mnauamini kikweli Uislamu! Simameni na muungane pamoja chini ya bendera ya tauhidi na chini ya kivuli cha mafundisho ya Uislamu ili kukata mikono ya madola ya kibeberu yanayopora utajiri wa nchi zenu na rejesheni heshima ya Uislamu kwa kujiweka mbali na mizozo na matamanio ya nafsi. Tambueni Waislamu kuwa nyinyi mna kila kitu.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakurubisha madhehebu za Kiislamu

Mapinduzi ya Kiislamu yaliandaa mazingira mazuri ya kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu na kutayarisha uwanja wa kupatika umoja kati ya Waislamu kupitia kuasisi Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu kupitia kupanua wigo wa welewa wa mafundisho ya kinadharia na kivitendo ya umoja na kuishi pamoja kwa salama Waislamu wote. Ni kwa kuzingatia malengo hayo ndio maana katika miaka ya awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikatangaza Wiki ya Umoja wa Kiislamu ambayo ni kipindi cha baina ya mwezi 12 hadi 17 Mfunguo Sita, kutokana na kuweko riwaya mbili tofauti kuhusu siku aliyozaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Kila mwaka, Iran inakuwa mwenyeji wa kongamano la umoja wa Kiislamu kwa mnasaba huo, kongamano ambalo linawakusanya pamoja maulamaa wa madhehebu yote ya Kiislamu kutoka maeneo tofauti duniani.

Msimamo thabiti wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran ambayo yana utambulisho wa kupiga vita mfumo wa kibeberu na dhulma ya aina yoyote ile, ni kikwazo kikubwa kwa madola ya kiistikbari ulimwenguni. Kimsingi, kupambana na uistikbari ni moja ya misingi isiyotetereka ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Fikra za kisiasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu zimesimama juu ya msingi wa mapambano katika njia ya haki na uadilifu na ni kwa sababu hiyo ndio maana historia ya Mapinduzi ya Kiislamu imejaa mapambano na kusimama imara taifa la Iran katika kukabiliana na madhihirisho yote ya dhulma na ukosefu wa uadilifu. Katika moja ya miongozo yake iliyojaa hekima, Imam Khomeini, MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema:

Kama mnataka kuyashinda matatizo yote, mnapaswa kuwa imara mbele ya madola ya kibeberu. Kama ambavyo mnapaswa pia kuwa na msimamo imara katika kulinda uhuru wenu; uhuru wa kiutamaduni, uhuru wa kiuchumi na uhuru wa kijamii. Inabidi yote hayo myalinde kwa nguvu zenu zote. Na hilo linawezekana chini ya kivuli cha kushikamana na mafundisho ya Uislamu, na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mkubwa na kuwa kitu kimoja; sambamba na matabaka yote ya watu kujiona kuwa ni ndugu.

Marekani yaiandama Iran

Unapoangalia historia ya uhusiano wa Iran na Marekani utaona kuwa, katika siasa zake kuhusiana na Iran, siku zote Marekani imekuwa ikifuata mkondo wa kuingilia mambo ya ndani ya Iran; hiyo ikiwa ndiyo ajenda yake kuu. Katika kila kona ya historia ya uhusiano baina ya nchi hizi mbili, unaonekana kwa uwazi sana uingilia wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran.

Watafiti wengi wamefichua kwamba, mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini Iran tarehe 19 Agosti 1953 ulikuwa ndio mwanzo wa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Wakati huo huo tunaweza kuuona pia uingiliaji wa miongo mingi wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran wakati tunapotupia jicho siasa za migawanyo ya kisiasa wakati wa vita baridi. Kwa mfano wakati wa mapinduzi ya mwaka 1917, muungano wa nchi waitifaki uliivamia ardhi ya Iran, na wakati huo Marekani ikaanza kuukodolea macho ya tamaa utajiri wa mafuta wa Iran. Matukio ya Vita vya Pili vya Dunia yaliifanya Marekani iweke mkataba wa kijeshi na Iran. Uhusiano huo ulipelekea kuwekwa mkataba wa dola milioni 10 za kuiuzia silaha Iran. Hata hivyo matukio ya mwanzoni mwa muongo wa 1950 yalileta mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika uhusiano wa Iran na Marekani. Mabadiliko hayo yalikwenda sambamba na uingiliaji mkubwa na wa pande zote wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 19, 1953, yaliandaa uwanja wa kuingilia Marekani masuala ya ndani ya Iran katika miaka mingi ya baadaye.

Mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Marekani na Uingereza mwezi Agosti 1953 yaliyoipindua serikali halali na ya kisheria ya wakati huo, yaani serikali ya Mohammad Mosaddegh, yanakumbushia kipindi kichungu katika historia ya kisiasa ya Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mujibu wa nyaraka za siri ambazo zilisambazwa baadaye, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilikuwa na nafasi kuu katika kupanga na kuongoza mapinduzi hayo na hatimaye kumpindua Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran katika kipindi cha baina ya mwaka 1952 hadi mwezi Agosti 1953.

Mwanzo wa mabadiliko ya kidemokrasia nchini Iran

Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa nukta ya mwanzo wa mabadiliko ya kidemokrasia nchini Iran ambapo yaliweza kuhusisha sekta mnalimbali kama vile za kijamii, kiuchumi na kwa misingi ya katiba. Misingi hiyo ilihusu masuala ya haki za taifa la Iran, haki ya kujitawala na kujiainishia mustakbali, kuchagua mihimili tofauti ya utawala, uhuru wa vyombo vya habari, usawa wa haki za kitaifa, usawa mbele ya sheria, uhuru wa vyama vya siasa na mambo mengine kama hayo ambayo yanawajumuisha raia wote wa taifa hili katika kustawisha demokrasia ya kidini nchini. Ni kwa kutegemea misingi hiyo, ndio maana tangu mwanzo kulipojiri mapinduzi ya Kiislamu, raia wa Iran wakawa wanashiriki kwa wingi katika chaguzi mbalimbali hapa nchini. Hatupaswi kusahau kwamba, baada ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara ya kwanza wananchi walishirikishwa katika kura ya maoni juu ya uainishwaji wa katiba, mnano tarehe 12 Farvardin mwaka 1358, sawa na tarehe Mosi April 1979 Miladia, ambapo asilimia 98.2 ya wananchi waliupigia kura ya ndio mfumo wa Kiislamu. Wito uliotolewa wa 'kesho tokeni nje ya nyumba zenu na mpige kura, lakini kwa uhuru na kuchagua mfumo mnaoutaka,' ilikuwa ni harakati ya kidemokrasia ya wananchi kupitia pendekezo la Imam Ruhullah Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, harakati ambayo iliidhihirishia dunia kwamba wananchi ndio waamuzi wa thamani za Mapinduzi ya Kiislamu nchini kupitia upigaji kura wao.

Kwa muktadha huo tangu awali muundo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukawa umejengeka juu ya msingi wa katiba ambapo wananchi walishirikishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika uchaguzi wa mihimili yote ya utawala. Mfumo huo unajumuisha pia uchaguzi wa Kiongozi Muadhamu katika nafasi ya Walii Mtawala, ambapo naye huchaguliwa na wawakilishi waBaraza la WanazuoniWataalamuwanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamuambao nao huchaguliwa na wananchi.

Muundo wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umejengeka juu ya misingi mikuu miwili ya Jamhuri na Uislamu. Kwa mtazamo wa mfumo wa kidemokrasia, jamhuri ina maana ya utawala unaotokana na wananchi. Kuhusiana na suala hilo, Omar Alaysapahych, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Bosnia anasema: "Tunapotazama kwa ufupi historia za kipindi cha mwisho wa karne za kati yaani karne ya 13 Miladia na kuendelea, na mwanzo wa kudhihiri ulimwengu wa leo, tunaona kuwa zilizama katika lindi la migogoro na hali mbaya inayofanana na ile tunayoishuhudia katika ulimwengu wa leo. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakiwa ni tukio ambalo linafungamana na nara, malengo, nguvuna kiongozi aliye na utambuzi sahihi wa mambo, ni mapinduzi ya kidini. Kwa hakika Iran ni mfano bora wa mapinduzi ya kidini yanayotegemea uamuzi wa wananchi."

Aidha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandikwa kwa kutegemea mfumo wa kiuchaguzi na kibunge, mfumo wa mabaraza na uhuru wa kiraia na kisiasa. Kifungu cha kwanza cha katiba kinasema: "Aina ya serikali nchini Iran ni Jamhuri ya Kiislamu," na hii ina maana ya mfumo wa serikali ya Jamhuri na Uislamu yaani misingi miwili ambayo kwanza ni thamani za dini na pili ni uchaguzi wa wananchi. Mfumo huu wa demokrasia unatekelezwa hapa nchini Iran kama sehemu ya haki za kiraia na kisiasa za wananchi. Hii ni kusema kuwa katika kipindi chote cha miaka 39 ya Mapinduzi ya Kiislamu, karibu kila mwaka wananchi hushiriki kwa uchache katika uchaguzi mmoja, suala ambalo linaonyesha kwamba, raia wa taifa hili ndio marejeo ya serikali, kupitia ustawi wa kisiasa na utawala bora wa demokrasia ya wananchi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kuhusiana na suala hilo, Ahmed Hatit, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa nchini Lebanon anasema: Tawala za kidemokrasia za wananchi katika kipindi cha karne za hivi karibuni, ni tawala ambazo kimsingi utendajikazi wake unatokana na matakwa ya wananchi, Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu imeunda mfumo mpya wa demokrasia ya wananchi ambao asili na dhati yake inatokana tu na matakwa na irada ya wananchi.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: