bayyinaat

Published time: 19 ,February ,2018      00:00:23
News ID: 228

Amani iwe juu yako Ewe Fatma Zahra mwanamke bora wa duniani na Akhera, Bibi (kiongozi) wa wanawake wa peponi, Mtukufu as-Sidiqah at-Tahirah Fatimatuz Zahra (Salaamullahi Alayha).

Siku tisini zilikuwa ndio zinamalizika tangu alipotangulia mbele ya haki mbora wa viumbe Bwana Mtume Muhammad SAW. Lakini pamoja na hayo mitaa na vichochoro vya mji mtakatifu wa Madina vilikuwa bado vinanukia harufu nzuri ya uturi wa uwepo wa Bwana Mtume huku Masjidun Nabi ikibakisha kumbukumbu zisizosahaulika za mtukufu huyo. Pembeni mwa msikiti huo wa Bwana Mtume ilikuwepo nyumba ya Fatima (Alayhas Salaam) na Ali (Alayhis Salaam). Majonzi yalikuwa yametanda ndani ya nyumba hiyo. Kutengana na Bwana Mtume SAW kwa upande mmoja na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua binti yake mtoharifu kwa upande wa pili, ni hali ambayo iliingiza daghadagha na huzuni kubwa katika moyo wa Ali bin Abi Talib AS na wanawe. Wakati huo Bibi Fatima alikuwa katika lahadha na dakika za mwisho za uhai wake hapa duniani. Majonzi makubwa ya kuondokewa na baba yake yalimkosesha furaha kabisa Fatima Zahraa. Matukio yaliyotokea baada ya kufariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW pia yaliongeza ghamu huzuni. Ingawa hata hivyo, moyo wa mtukufu huyo ulifarijika kila alipokumbuka maneno ya baba yake mtukufu wakati anarejea mbele ya haki alipomwambia: "Binti yangu kipenzi! Wewe utakuwa mtu wa kwanza kabisa wa Ahlul Bayt wangu atakayejiunga nami mbele ya haki baada yangu."

Katika lahadha na sekunde za mwisho wa uhai wa Bibi Fatima Zahraa, Ali na wanawe wanne walikuwa wameketi pembeni mwa mto wa kulalia wa mtukufu huyo. Jicho la Ali bin Abi Twalib lilikuwa halibanduki kwenye sura ya mkewe huku akili yake ikifikiria maisha mafupi ya mkewe lakini yaliyojaa baraka. Imam Ali alikumbuka maneno ya Bwana Mtume SAW aliposema: "Ewe Ali! Fatima ni tunda la moyo wangu. Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakuna hata mara moja ambapo Fatima amepata kuniudhi na kunikasirisha."

Dakika zilikuwa zinapita pole pole na kwa kimya kizito. Ali AS aliichukua mikono ya moto yenye homa ya mkewe Fatima na kukumbuka siku Fatima alipokuwa anamwambia:

Ali mume wangu! Mimi nitakuwa pamoja nawe katika hali yoyote ile. Kama utakuwa katika raha nitakuwa pamoja na wewe na iwapo utakuwa katika shida na mabalaa pia nitakuwa pamoja nawe, wakati wote, na hivyo ndivyo alivyotenda.

Watoto wadogo wa Fatima nao walikuwa wanamwangalia mama yao kwa macho yaliyojaa machozi huku wakikumbuka nyakati azizi na adhimu walizoishi na mama yao. Zaynab alishuhudia kwa macho yake namna mama yake alivyokuwa akihakikisha hamrudishi mikono mitupu mtu yeyote aliyemuomba msaada. Imam Hassan AS alikumbuka dua za usiku wa manane za mama yake wakati alipokuwa akikesha kwa ibada huku akiwaombea dua watu wote. Imam Hussein AS nayo alishuhudia mwenyewe jinsi mama yake alivyokuwa fasaha wa maneno na mbora wa matendo mbele ya watu wakati alipokuwa akiwalingania haki kwa maneno na matendo yake mema.

Ali AS aliinama sikioni mwa mkewe na kumnog'oneza kitu akimwambia: Ewe Fatima! Kuwepo kwako kunaufanya moyo wangu utulie. Kamwe hujawahi kunisumbua wala kunikasirisha na kila ninapokuangalia, simanzi zangu zinaondoka. Kwa hakika wewe ni mwanamke bora kabisa wa umati wa Muhammad.

Fatima AS alifungua macho yake. Akamwangalia mumewe na wanawe kwa jicho lililojaa huruma. Kana kwamba alitaka kutoa wasia wake wa mwisho. Alimkumbusha mumewe kuwa awatunze vizuri wanawe na ahakikishe anamzika katika kiza cha usiku mbali na macho ya watu, na asiruhusu mtu yeyote kuliona kaburi lake. Mtukufu huyo alikimbilia haraka msikitini kwenda kulia kwa Mola wake. Muda haukupita ila ukawadia wakati wa roho toharifu ya Fatima kurejea kwa Mola wake. Mtukufu huyo alifungua macho yake akaangalia mbinguni na kusema: Assalaamu Alayka Yaa Jibril. Assalaamu Alayka Yaa Rasulallah! Amani iwe juu yako Ewe Jibril. Amani iwe juu yako Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Huyu hapa Malaika Mwenyezi Mungu amenijia na baba yangu ananiambia: Binti yangu, fanya haraka kuja kwangu. Kinachokusubiri huku ni kitu bora kabisa. Amani iwe juu yako Ewe baba yangu. Amani iwe juu ya watenda mema.

Hapo hapo Fatima akaingia kwenye mabawa na malaika na kuelekea mbele ya Haki. Wakati Ali AS alipoingia nyumbani kutoka msikitini aliona roho ya Fatima imeshatoka. Alipouona mwili usio na roho wa mkewe alimukhutubu akimwambia: Baada yako wewe hakuna kheri yoyote katika maisha yangu hapa duniani na mimi ninalia kwa sababu naogopa, maisha yangu yatakuwa marefu baada yako.

Mapokezi ya kihistoria yanasema kuwa, Bibi Fatimatuz Zahra SA alifariki dunia mwezi tatu Mfunguo Tisa, Jamadu Thani, mwaka wa 11 Hijria akiwa amewabakishia walimwengu urithi wenye thamani kubwa sana. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu na wapenzi wote wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW kwa mnasaba wa kukumbuka siku hii ya kuhuzunisha sana.

Bibi Fatimatuz Zahra SA ni bibi mtukufu ambaye sira na mienendo yake itabakia hai milele na itaendelea kuwa ruwaza njema kwa kila mpigania haki. Bibi Fatima SA hakuishi kwa zaidi ya miaka 18, lakini alikusanya fadhail na matukufu yote ya kibinadamu. Mtukufu huyo alifikia daraja kubwa ya kumtambua Muumba wake kiasi kwamba hadi leo hii amekuwa ni kigezo bora cha maisha yaliyojaa ufanisi. Dhati yake yote ilijaa welewa na utambuzi wa Muumba wake kadiri kwamba, hakuwa akifikiria kitu chochote katika maisha yake yote isipokuwa kumridhisha Muumba wake. Bwana Mtume Muhammad SAW anatoa ushahidi wa mapenzi hayo ya kweli aliyokuwa nayo Fatima SA kwa Muumba wake kwa kumwambia mmoja wa masahaba wake wakubwa Salman kwamba: Ewe Salman! Mwenyezi Mungu amemimina na kutia imani thabiti katika moyo na roho na dhati yote ya Fatima ya kumuabudu Muumba wake kiasi kwamba hakujabakia sehemu hata ndogo tupu ya kuingia kitu kingine chochote katika moyo wake ghairi ya kumuabudu Mola wake.

Roho tukufu ya Fatima haikupenda kabisa mapambo na urembo wa dunia. Nyumba ya Ali na Fatima Zahraa haikuwa kabisa na vifaa vya nyongeza na vya thamani kubwa. Lakini badala yake ilikuwa ni nyumba iliyojaa imani, mapenzi na unyofu wa moyo hali ambayo iliongeza moyo wa kutekeleza vizuri majukumu, kupigania uadilifu na kusimamisha haki. Fatima alikuwa mbora wa wanawake wacha Mungu, lakini si kwa maana ya kuachana kikamilifu na dunia bali kwa maana ya kwamba dunia haikuiteka roho yake na wala kuifanya mtumwa wake. Kwa kweli hakuna mwanamke aliyemfikia Fatima kwa ubora. Chochote alichokipata alikitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu na alikuwa mstari wa mbele wakati wote kujitolea kwa ajili ya kutafuta radhi za Muumba wake.

Maneno na matendo ya Fatima yalipambika kwa adabu na heshimu kiasi kwamba mmoja wa watu waliokuwa wakimuhudumia mtukufu huyo anayejulikana kwa jina la Asmaa anasema: Mimi sijawahi kumuona mwanamke mwenye adabu na heshima kama Fatima. Yeye amejifunza adabu na heshima kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wakati Mwenyezi Mungu aliposhusha aya na kuwataka Waislamu na waumini wasimwite Bwana Mtume kwa jina lake, Bibi Fatima Zahra naye aliacha kutumia neno "baba" kumwita baba yake, bali alianza kumwita Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hadi Bwana Mtume akalazimika kusema, aya hiyo haimuhusu mwanangu Fatima.

Katika maisha yake ya kifamilia pia, heshima na adabu pamoja na mapenzi ya Fatima yalijenga mfungamano mkubwa na mtukufu sana kati yake na mumewe Ali AS.

Itaendelea ......


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: