bayyinaat

Published time: 19 ,February ,2018      16:37:00
News ID: 230

Kiongozi wa chama cha Leba cha nchini Uingereza amesema kuwa, chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ni tatizo kwa jamii ya nchi hiyo ya bara Ulaya na kwamba, dini ya Uislamu ni nembo ya amani na kujitolea.
Jeremy Corbyn  amesema hayo katika msikiti wa Finsbury Park kaskazini mwa London katika kampeni ya nchi nzima nchini Uingereza inayoendeshwa na Waislamu na ambayo inajulikana kwa jina la "Siku ya Kutembelea Msikiti Wangu" na kubainisha kwamba, uhalifu unaofanywa kwa sababu ya chuki dhidi ya Uislamu unatia aibu.
Kiongozi huyo wa chama cha Leba ameshambulia vikali kampeni chafu ya chuki dhidi ya Uislamu na kubainisha kwamba, akthari ya wananchi wa Uingereza hawakubaliani na jambo hilo.
Jeremy Corbyn amesisitiza kuwa, katika vikao ambavyo amewahi kufanya na Waislamu hususan wanawake ambao wamekuwa wakivunjiwa heshima kutokana na kuvaa vazi la Hijabu, amewataka warekodi video wakati uhalifu huo unapofanyika na kuwasilisha mashtaka katika vyombo vya sheria.
Kiongozi huyo wa chama cha Leba ameeleza kuwa, njia na majibu bora kabisa ya kukabiliana na vitendo hivyo ni wananchi kuwa na umoja na mshikamano.
Zaidi ya misikiti 200 nchini Uingereza imeshiriki katika kampeni hiyo ya "Siku ya Kutembelea Msikiti Wangu" iliyofanyika Jumapili ya tarehe 18 Februari na lengo la mpango huo ni kuwafahamisha wafuasi wa dini nyingine kuhusu mafundisho ya Uislamu na wakati huo huo kukabiliana na kampeni chafu ya chuki dhidi ya Uislamu. Kituo cha Kiislamu cha Uingereza kilicho chini ya ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nacho kimeshiriki katika kampeni hiyo ya "Siku ya Kutembea Msikiti Wangu".
Miaka iliyotangulia misikiti kadhaa imekuwa ikiwakaribisha wasiokuwa Waislamu lakini mwaka huu ulishuhudia misikiti mingi zaidi ikishiriki katika mpango huo wa kuwakaribisha majirani ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Milango iliyowazi, misikiti iliyowazi na jamii zilizowazi.'

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: