bayyinaat

Published time: 23 ,February ,2018      15:11:58
News ID: 237

Mpenzi msomaji katika sehemu hii ya kwanza ya makala hii ya "umuhimu wa salamu katika Uislamu” nitajaribu kwa kadiri ya tawfiki ya Allah kuzungumzia jinsi suala hili lilivyopewa umuhimu katika Uislamu pamoja na faida zake kijamii. Salamu au kutoleana salamu ni katika ada na tabia njema katika dini tukufu ya Kiislamu. Suala hili limeelezwa katika mafundisho ya Kiislamu kwamba, lina nafasi muhimu katika kujenga na kuongeza huba na mapenzi baina ya wanajamii na hata kuondoa undani na vinyongo vilivyojitokeza baina ya watu wawili. Suala la salamu na kusalimiana limeenea na linaonekana katika mila na tamaduni hata za wasiokuwa Waislamu. Kila jamii yenye watu salama inalitambua suala la salamu na kusalimiana kwamba, linafaa na lenye kupendeza. Mtu yeyote ambaye hasalimii kwa hakika huonekana katika jamii kwamba, ni mwenye mapungufu na si hasha hata wanajamii wakamtenga na kumkosoa wakisema: "achana nae yule hasalimiagi watu”. Hata hivyo baya zaidi ni pale mtu anaposalimiwa na kutojibu salamu. Kimsingi kusalimia sio wajibu lakini kuitikia salamu ni ni wajibu na endapo mtu atajizuia na kukataa kuitikia salamu basi atakuwa ametenda dhambi.

Jambo la kwanza la kufanywa mara watu wanapokutana

Wakati watu wawili wanapokutana, kitu cha kwanza wanachokifanya kwa ajili ya kudhihirisha mapenzi yao, ni kusalimiana na kisha kufuatia hatua zingine kama kupeana mikono na kadhalika. Mtume Muhammad saww amesema:

إذا تَلاقَيتُم فَتَلاقَوا بِالتَّسليمِ و التّصافُحِ ، و إذا تَفَرَّقتُم فَتَفَرَّقُوا بِالاستِغفارِ

Mnapokutana, kutaneni kwa salamu na peaneni mikono; na mnapoatengana, tenganeni kwa kutakiana maghfira. (Kitabu cha Al-ʾAmālī cha Sheikh Tusi).

Kwa hakika moja ya mikakati ya kujenga ubinadamu na kuimarisha mapenzi na huba ya Kiislamu ambayo pia ni suala linaloweza kuondoa vinyongo na badala yake kustawisha mahaba kati ya wanadamu ni kutoleana salamu au kusalimiana. Aidha kupeana mikono sambamba na salamu, ni moja ya mambo yanayowakurubisha pamoja zaidi wanadamu. Tunapomtolea salamu mtu wa upande wa pili, ni wazi kwamba, huwa tunataka kujua hali yake ya kiafya na kadhalika. Kupeana mikono na kuitikisa katika hali ya kusalimiana, ni ishara nyingine ya mapenzi na kutakiana heri kati ya pande mbili. Kitendo hicho huzikurubisha pamoja nyoyo za watu sambamba na kuimarisha mapenzi kati yao. Kuamkiana kwa kupeana mikono huziweka na kuzileta pamoja nyoyo. Halii hii hufanya hali ya huba na mapenzi kutawaliwa katika jamii hali ambayo hufuatiwa na bashasha na tabasamu baina ya wanajamii.

Itaendelea........

Na  Salum Bendera


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: